MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Abdulrahman Kinana anapumzika baada ya kukitumikia Chama hicho kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema Kinana amekuwa akikitumikia Chama tangu wakati wa TANU hadi CCM; kabla ya mfumo wa vyama vingi na hata baada ya mfumo huo kurejeshwa nchini.
Rais Samia amesema hayo alipokuwa akizungumza na wana CCM kupitia Mkutano Mkuu maalum uliokutana kwa ajili ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyokuwa wazi baada ya Kinana kustaafu siasa.
“Katika kipindi chote hicho hadi leo, Ndugu Kinana amekuwa mmoja wa makada watiifu wa CCM na mwenye uzalendo usiotiliwa shaka kwa nchi yake. Amekuwawa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, mjumbe wa Kamati Kuu, Katibu Mkuu wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara.”
Rais Samia amesema kuwa mbali na utumishi wake ndani ya CCM, Kinana pia alikuwa ni mmoja wa Maaskari hodari aliyetumikia nchi yake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hadi kufikia cheo cha “Kanali”. Ndugu Kinana pia aliitumikia nchi kwa nafasi mbalimbali Serikalini ikiwemo Waziri wa Ulinzi na JKT.
“Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa inamshukuru sana na kumpongeza kwa dhati Ndugu Abdulrahman Kinana kwa uongozi wake thabiti katika utumishi wake ndani ya CCM na Serikalini.Tunamtakia mapumziko yenye furaha, afya njema na umri mrefu, pamoja na kumhakikishia ushirikiano wetu kwake.”
Kwa upande wake Kinana amesema akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano huo ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa kupewa nafasi ya kukitukia chama hicho kwa nafasi mbalimbali.
Ametoa shukrani kwa Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais kwa kumuamini na kumteua katika awamu mbili tofauti kumteua kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwashukuru wana CCM wote wakiwemo watangulizi wake katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti huku akimpongeza Stephen Wasira kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwani ni mtu sahihi katika nafasi hiyo,amefanya naye kazi anafahamu uhodari na uchapakazi wake.”Nimepata nafasi ya kufanya kazi na mzee Wasira,ni mtu mwadilifu na mchapakazi hodari.”
Comments