Moja ya sababu inayochangia watu wengi wabaki vilevile kila siku ni pamoja na kung'ang'ania mazingira yaleyale na kuogopa kwenda kwenye mazingira mapya wakihofia kuonekana watu wa hali ya chini na kudhalilika.
Binafsi pia nilikuwa mtu wa kujishtukia na kujichukulia mimi ni masikini ambaye sistahili kujua au kuingia kwenye baadhi ya maeneo kwa kuhofia kutengwa, kupuuzwa au kuonekana mwizi.
Kama na wewe ni mmoja wa watu ambao una mtazamo kama niliowahi kuwa nao hapo kabla na unapambana kuja kuwa tajiri, hakikisha unakwenda maeneo yafuatayo kwa ajili ya kuua saikolojia ya kimasikini ili usiipe nafasi hofu ambayo ni moja ya kikwazo kikubwa kwenye mafanikio.
1. ENEO LA KWANZA
Kama unaamini maeneo masafi, yenye milango ya vioo, mabango ya kuwaka, vitaataa kila sehemu, wateja wachache na wahudumu ambao kwa mtazamo wa kimasikini huwa wanaonekana kama wana nyodo ni maeneo ya gharama sana na ya matajiri peke'ao kiasi kwamba hupaswi kwenda hata kusogea kuulizia bei, Mwaka huu hakikisha umeulizia bidhaa nyingi na kununua angalau chache mpaka wakukariri jina na kukuita Bosi.
2. ENEO LA PILI
Kama huwa unakwepa kula maeneo wanayouza chakula kizuri, kiduchu kama cha mtoto halafu kitamu, sehemu ambayo wahudumu wanavaa sare safi na wanakunyenyekea kama vile wanakutaka, muziki wao ni wa taratibu na umefunguliwa kwa mbali, walaji hawana kelele, tishu sio za kuhesabu, vyombo vyao sio vya plastiki, viti na meza ni visafi muda wote, kula hapo angalau mara moja kwa mwezi ila usiagize chochote kabla hujasoma menyu usije ukasema Mwalimu Victor nimekutuma.
3. ENEO LA TATU
Kama kwa mwaka unanyoa zaidi ya mara tano lakini huwa unapeleka kichwa chako kwa wahuni wanakizungusha kama gia boksi, anayekunyoa na mashine anayokunyolea vyote vinapiga kelele, muziki mpaka hamuelewani mwaka huu badilisha eneo.
Mwaka huu nenda sehemu ambayo kumsubiri tu uliyemkuta unapewa soda, ukinyolewa unakoshwa kichwa na kupakwa vitu vya maana ambavyo vinanukia na kama haitoshi bado unaulizwa kama unahitaji huduma nyingine za ziada.
4. ENEO LA NNE
Ni sawa kumuabudu Mungu lakini kumuabudu Mungu eneo lilelile na watu walewale ambao wote hali zinaendana wakati mwingine inadumaza na kuua imani kiasi kwamba unakuwa kama vile mtu hujibiwi maombi yako.
Katika siku nne za ibada kwenye mwezi sio mbaya ukatoa siku moja ya kwenda kuchangamana kwenye nyumba ya ibada ambayo kuanzia nje tu unaanza kuziona baraka za Mungu kwa waja wake kupitia mikebe iliyopaki.
5. ENEO LA TANO
Sio dhambi kutenga siku moja au mbili katika mwezi/miezi kadhaa na kwenda kuzurura mitaa ambayo kila unapopita ni mbwa tu ndiyo wanakupigia kelele huku vitu pekee unavyopishana navyo njiani ni magari ambayo mtaani kwenu kuyaona ni mara moja kwa mwaka.
SOMO LITAENDELEA
Mwl. Victor Ramadhan Kalinga
0620 443 048
Ilala - Dsm Tanzania
Comments