TUME YA MADINI YAAINISHA MIPANGO YA KUWAWEZESHA WACHIMBAJI WADOGO WA MADIN











_Uanzishwaji wa masoko ya madini wapunguza utoroshwaji wa madini_


_Elimu yatolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini_


*CHUNYA*


Ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha Tume ya Madini inavuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli la shilingi Trilioni Moja kwa mwaka 2024-2025 lililowekwa na Serikali, mikakati mbalimbali imeendelea kuwekwa na Tume ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa usimamizi katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, utoaji wa leseni za madini na utoaji wa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini.


Hayo yamesemwa leo Januari 27, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na TEHAMA, Mhandisi Aziza Swedi kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya wachimbaji wa madini katika mikoa ya kimadini ya Chunya na Songwe yaliyofanyika Chunya Mjini.


Amesema kuwa, kwa kutambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo wa madini nchini, Serikali kupitia Tume ya Madini imepanga kuwapatia elimu kuhusu uchimbaji salama na endelevu sambamba na kuwaunganisha na Taasisi za Kifedha na kupata mikopo ili uchimbaji wao uwe na manufaa huku Serikali ikipata kodi na tozo mbalimbali.


“Sambamba na kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wanaendelea kunufaika bila kuathiri mazingira, suala la usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ni endelevu na tumelipa kipaumbele ambapo kwa sasa tumeendelea kutoa mafunzo katika mikoa mbalimbali ikiwepo mikoa ya kimadini ya Songwe na Chunya,” amesema Mhandisi Swedi.


Akielezea mchango wa wachimbaji wa madini kwenye Sekta ya Madini, Mhandisi Swedi ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini mwaka 2019, kasi ya utoroshaji wa madini imepungua nchini kwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini kwa sasa wanauza madini yao katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini hivyo kupelekea makusanyo ya maduhuli kuongezeka.


“Kwa mfano kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2024 katika mwaka wa fedha 2024-2025 mkoa wa kimadini wa Chunya umekusanya kiasi cha shilingi bilioni 30 sawa na asilimia 50 ya makusanyo ya shilingi bilioni 60 katika mwaka wa fedha 2024-2025.


Katika hatua nyingine, Mhandisi Swedi amewataka wachimbaji wa madini kuwa wazalendo kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali sambamba na kufuata Sheria za Madini na Kanuni zake.


Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando ameongeza kuwa lengo la Tume ya Madini kutoa mafunzo hayo hasa kwenye masuala ya usalama kwenye shughuli za madini ni kuhakikisha kuwa uwepo wa migodi ya madini hauathiri afya na mazingira kwa wachimbaji na jamii inayozunguka.


“Sisi kama wataalam kutoka Tume ya Madini tunatamani kuona wachimbaji wa madini wanaendesha shughuli zao kwa kufuata Sheria na Kanuni za Mazingira na kuepusha ajali zinazoweza kutokea na kupoteza nguvu kazi ya nchi.


Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kukusanya maoni na kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini na kuendelea kuvutia ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini.


Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo wamepongeza uwepo wa mafunzo na kusisitiza elimu hii kuendelea kutolewa kwenye majukwaa, makongamano na maonesho mbalimbali.


Mashaka Fungameza ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Chunya mkoani Mbeya amesema kuwa, uwepo wa mafunzo hayo utawawezesha kuboresha shughuli za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia kanuni za usalama na kupunguza ajali zinazoweza kujitokeza hasa kipindi cha mvua na kupunguza vifo.


Naye Masunga Mapalala kutoka kampuni ya Apex Resources Limited kutoka Chunya amewataka wachimbaji wa madini kutumia elimu inayotolewa na Tume ya Madini kwa kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.



Mada zinazotolewa katika mafunzo hayo ya siku mbili yanayotarajiwa kumalizika kesho Januari 28, 2025 ni pamoja na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kanuni zake na mabadiliko yake ya mwaka 2017; utoaji na usimamizi wa leseni za madini; afya na usalama kwenye migodi na utunzaji na uhifadhi wa mazingira migodini.


Mada nyingine ni pamoja na biashara ya madini na masoko, usimamizi wa fedha na kodi, ushirikishwaji wa watanzania katika shughuli za madini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

CHAMA KIPYA CHA WALIMU WAMUOMBA RAIS SAMIA AINGILE KATI MAKATO YA WANACHAMA WAO

TOFAUTI YA WATU WA DAR NA WA MKOANI NI HUU

IBENGE: YANGA SC WATAFUZU HATUA YA ROBO FAINALI.

NILIYOYABAINI KATIKA TRENI YA SGR DAR ,MORO HADI DODOMA … KADOGOSA REKEBISHENI MAMBO HAYA MTANIKUMBUKA

NOTI MPYA KUANZA KUSAMBAZWA MWEZI UJAO