WAKUU WA SHULE NA WALIMU WA TAALUMA WILAYA YA SAME WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MTAALA ULIOBORESHWA
Na Ashrack Miraji,
Halmashauri ya Wilaya ya Same,Mkoani Kilimanjaro, imewajengea uwezo kuhusu Mtaala wa Elimu ulioboreshwa Wakuu wa shule na walimu wa taaluma 165 kutoka shule 46 za Serikali na 19 za binafsi ili kuwawezesha walimu hao kutekeleza Mtaala huo kwa ufanisi.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mwalimu Neema Lemunge, amesema baada ya mtaala wa elimu kuboreshwa Wilaya imeona kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wakuu wa shule na walimu ili waweze kuelewa na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Mbali na kuwajengea uwezo kuhusu mtaala mpya, tumefanya tathmini ya matokeo ya kidato cha pili, tumejipima, tukaona tulipo hivyo tumekubaliana na kuwekeana mikakati ya kuboresha utendaji na kuondoa matokeo duni kama division zero na division four,” alisema Mwalimu Neema Lemunge.
Afisa Elimu huyo aliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu. Alisema Serikali imejizatiti katika kujenga miundombinu ya shule ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Awali akufungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Dkt.Cainan Kiswaga aliwataka walimu kutumia muda vizuri wawapo shuleni.
"Lengo letu ni kuongeza ufaulu hivyo lazima tuhakikishe kuwa tunatumia muda vizuri na tusipoteze kipindi hata kimoja"alisema Dkt.Cainan
Akifafanua kuhusu Mtaala ulioboreshwa, Mthibiti ubora wa Shule Wilaya ya Same Bw.Furahini Lubua alisema kidato cha I hadi IV kutakuwa na masomo 27 ambapo haitamlazimu mwanafunzi kusoma masomo yote hayo kwani kutakuwa na uchaguzi (option) kwa baadhi ya masomo.
Aliyataja masomo ya lazima kidato cha I hadi IV yanakuwa sita na sio Saba kama ilivyokuwa mwanzo,Masomo hayo ya lazima ni:
1. Mathematics
2. Kiswahili
3. English Language
4. Business Studies
5. Geography
6. Historia ya Tanzania na Maadili
Alisema somo la Bailojia na Historia yameongezwa kuwa masomo chaguzi (optional). yakiungana na yale ya zamani ya Fizikia na Kemia.
"Zamani Masomo chaguzi (option) yalifanyika kwa wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne lakini kwa sasa wanafunzi wanachagua toka kidato cha kwanza" alifafanua Mthibiti Ubora.
Jumla mwanafunzi anatakiwa asome masomo yasiyo pungua 8 na yasiyozidi 10.
Mtaala huo mpya utaanza Utekelezaji Januari 2025.
Comments