Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Bi. Nyakaho Mahemba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita leo tarehe 28 Februari, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
MAFANIKIO YA MFUKO KATIKA KIPINDI CHA AWAMU YA SITA
Mafanikio ya utendaji wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chake cha miaka minne (4) akiwa madarakani ni kama ifuatavyo:-
Kuongezeka kwa Mtaji
Kwa kuzingatia umuhimu wa Mfuko katika ukuzaji na uendelezaji wa miradi ya Sanaa ili iweze kuzalisha bidhaa bora na shindani kulingana na viwango na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuongeza bajeti ya Mfuko ili uweze kutekeleza majukumu yake ya Msingi hususani katika kuzalisha ajira na kuongeza fedha za kigeni. Miongoni mwa hatua hizo ni:-
Kuongezeka kwa bajeti ya Mfuko katika kila mwaka wa Fedha ambapo katika mwaka wa fedha 2023/24 bajeti ya Mfuko iliyoidhinishwa ilikuwa ni shilingi bilioni 1.6 ambapo katika mwaka wa fedha 2024/25 bajeti imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 3. Aidha, kiasi kilichoongezeka ni Shilingi Bilioni 1.4 ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 87.5
Serikali imeongeza chanzo kipya na endelevu cha mapato ya Mfuko kinachotozwa katika vibebeo tupu vya Kazi za Sanaa (Tozo ya Hakimiliki – Copyright Levy). Aidha, kupitia chanzo hichi, Mfuko hupata gawio la asilimia 10 ya mapato yote yanayokusanywa. Chanzo hiki kimeanza kutekelezwa Mwezi Septemba, 2023.
Utoaji wa Mikopo
Mfuko unatoa mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na NBC. Lengo la ushirikiano huu ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kutumia utaalamu na uzoefu wao katika eneo la utoaji wa mikopo, usimamizi wa marejesho pamoja na ufuatiliaji wa miradi iliyowezeshwa n.k
Kupitia uongozi mahiri na madhubuti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko umefanikiwa katika maeneo yafuatayo:-
Mikopo yenye thamani ya Shilingi 5,250,070,500.89 kwa miradi 359 ya Sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213
Mchanganuo wa maeneo ya miradi ya iliyowezeshwa ni muziki (miradi 78), filamu (miradi 90), maonesho (miradi 65), Ufundi (miradi 103) na Lugha na Fasihi (23) ; na
Mikoa iliyofikiwa ni 18 ambayo ni Dar- Es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi,
Uwezeshaji wa mikopo kisekta
Sekta ya Muziki
Mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 1,246,215,189 kwa miradi ya 78 ya muziki ambapo kiasi hiki kimetekeleza yafuatayo kwa wasanii
Kununua vifaa vya kisasa kwa studio 42 za kuzalishia muziki ambapo uwepo wa studio hizi umesaidia kuondoa adha na gharama kwa wanamuziki kuzalishia kazi zao nje ya nchi. Studio hizi za kisasa zimewahamasisha wasanii mbalimbali kutoka nje ya nchi kuja nchini kwetu kwa ajili ya kuzalisha kazi zao. Hivyo, zimekuwa ni chanzo cha mapato ya fedha za kigeni na kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu na wasanii nchini.
Kununua vifaa vya kisasa kwa bendi 18 za muziki wa injili, bendi 13 za muziki wa dansi na Bendi 3 za muziki wa Taarabu
Kuendesha matamasha 16 ya muziki wa nyimbo za injili yaliyoshirikisha wasanii wa ndani na nje ya nchi, matamasha 18 ya muziki wa nyimbo za Singeli yaliyoibua vipaji vipya kwa wasanii 117;
Kutengeza jumla ya nyimbo za Audio 124 na video 36;
Kununua majukwaa ya kisasa matatu (3) kwa ajili ya kazi za Sanaa
Kuwezesha Chuo kimoja cha UD-J ambacho kimezalisha ma- DJ 288 ambapo wengi wao wameajiriwa katika Vituo vya Redio, Luninga, Kumbi za Burudani na Starehe na wengine wamefanikiwa kujiajiri wenyewe.
Sekta la Filamu
Mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 1,329,007,342.00 kwa miradi 90 katika sekta ya Filamu. Kiasi kilichotolewa kimewezesha maeneo yafuatayo:-
Kununua vifaa vya kisasa kwa Studio 61 za kuzalishia filamu na tamthiliya ambapo vifaa hivi vimeongeza ubora na mwonekano wa kazi hivyo kuzifanya kukubalika ndani na nje ya nchi.
Kuboresha mandhari/mwonekano wa Ofisi za Studio 9;
Kuzalisha filamu 241, tamthiliya 9 zinazorushwa katika vituo mbalimbali vya habari pamoja na mitandao ya kijamii
Umekuwa kichocheo kwa wasanii wa nje ya nchi kushirikiana na wasanii wa ndani ikiwa pamoja na kutumia vifaa vya uzalishaji vya kisasa vilivyowezeshwa na Mfuko; na
Umewezesha kukarabati Ofisi kwa Maktaba za Video 11 na ununuzi laptop za kisasa 6
Sekta ya Sanaa za Ufundi
Mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 1,550,060,050.00 kwa miradi ya Sanaa 103 nchini. Aidha, miradi hii imekuwa kichocheo kikubwa cha utalii nchini. Maeneo yaliyowezeshwa ni pamoja na :-
Soko la Maasai Market lenye wasanii wazalishaji 383 wa bidhaa mbalimbali kama vile Nguo za Asili na Utamaduni, Bidhaa za ngozi, Shanga, uchoraji, uchongaji, nguo za batiki na vikoi nk kwa ujumla wamewezeshwa kiasi cha Shilingi 645,700,800 ambapo maombi mengine yanaendelea kufanyiwa kazi
Hili ni soko la Kipekee Afrika Masharariki na Kati lenye kutoa huduma bora na kwa gharama nafuu na lisilo na udalali
Soko linatoa fursa kwa wasanii wachanga kujifunza na kukua kisanii na kibiashara;
Wasanii katika soko hili wamefanikiwa kutembelea nchi 19 kwa ajili ya kutangaza na kuuza bidhaa ambapo nchi walizotembelea ni Ufaransa, italia, ujerumani, Kongo, Burundi, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudani ya kusini, Madagascar, Zimbabwe, Nigeria, Uingireza, marekani, Msumbiji, Zambia, Dubai, China na Afrika ya Kusini. Pamoja na mambo mengine, wasanii hawa wamejifunza mbinu mbalimbali za kibiashara kutoka kwa wasanii wengine;
Soko linatembelewa na wastani wa raia wa kigeni 100- 150 wanaokuja kununua bidhaa kwa siku hivyo kuwa sehemu ya chanzo cha kuingiza fedha za kigeni nchini
Umewezesha vyuo vitano (5) vya kati vilivyosajiliwa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu ya ujuzi kwa fani mbalimbali kama vile ushonaji, mapambo, ususi, upishi nk katika ngazi ya Cheti, Diploma na kozi fupi. Vyuo hivi tangu viwezeshwe mwaka 2023 vimefanikiwa kuzalisha jumla ya wasanii 1,978 ambapo baadhi yao wamejiajiri na kuajiriwa katika Ofisi mbalimbali.
Sanaa za Maonesho
Katika eneo hili, Mfuko umetoa mikopo ya shilingi 759,087,719.00 kwa miradi 65. Waliowezeshwa katika eneo hili
Waongoza Shughuli (MC) 33,
Watoa huduma katika hafla mbalimbali 32 (Meza, Viti, Mahemba, Keki, Mifumo ya Muziki, Majukwaa ya mikutano na burudani nk)
Lugha na Fasihi
Aidha, Mfuko umewezesha miradi 23 yenye thamani ya Shilingi 365,700,200.00 katika eneo la Lugha na Fasihi
Miradi iliyowezeshwa ni
Uchapishaji wa vitabu 6,000 vyenye maudhui ya mada mbalimbali kama vile hadithi za watoto, vitabu vya ziada, vitabu vya kutoa elimu ya jamii, maudhui ya historia ya matukio ya kale, ngonjera na mashairi;
Kuwezesha kampuni 13 za uchapishani wa vitabu, tisheti nk
Uwezeshaji wa Mikopo kimakundi
Kati ya mikopo yenye thamani ya shilingi 5,250,070,501.89 iliyotolewa kwa miradi 359, Shilingi 1,470,019,740 zilikopeshwa kwa makampuni 54, shilingi 525,007,050 zilikopeshwa kwa vikundi/Bendi 31, Shilingi 1,312,517,625 zilikopeshwa kwa miradi 109 inayomilikiwa wanawake na shilingi 1,942,526,085. 89 kwa miradi 165 inayomilikiwa na wanaume.
Comments