Kauli hiyo inakuja baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuharakisha ujenzi wa Arena ili wasanii wapate ukumbi wa kufanya shughuli zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amesema baada ya Rais Samia kufanya ziara Korea, amepata mkopo wa masharti nafuu wa Dola bilioni 2.5.
Advertisement
“Kati ya fedha hizo ameamua kukata Sh bilioni 450 kwa ajili ya kuzileta Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujenga Arena kwanza halafu itafuatia kijiji cha filamu,”amesema.
Amesema fedha zitakapotoka Korea na kufika kwao wataanza ujenzi wa Arena mara moja ili uwanja huo uanze kutumika kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani.
“Arena inakuja, ndugu zangu wasanii tumshukuru sana Rais Samia, hili jambo lilikuwa linamuumiza kichwa, tutajenga pale Kawe na eneo lilikuwa linaandaliwa linatusubiri sisi,”amesema.
Amesema:”Namuelewa Diamond, mimi ameniambia mara nyingi aliniambia nyie mnajenga viwanja lakini sisi mnatusahau, hatimaye tumepata fedha za kujenga. Niwapongeze wasanii wote kwa kufanya vizuri,”
Msigwa amesema uwanja huo utakuwa unatumika kwa shughuli nyingine mbalimbali ikiwemo maombi ya kitaifa, mashindano ya Quran na mambo mengine.
Amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) hawapendezwi wanavyotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya shughuli za nje ya michezo.
“Inawaudhi kwasababu wanaona viwango vya ubora wa uwanja vinaharibiwa. Lakini kwasababu hatuna mahali pengine pa kufanyia shughuli hizi, Arena itasaidia kuondokana na haya,”amesema.
Comments