Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania (UWT), Ndg. Mary Chatanda amewaonya wabunge wateule wa viti maalumu kuacha kubweteka kwa kudhani tayari wameshinda, bali wanatakiwa kupambania kwa nguvu zote ushindi wa CCM ili wajihakikishie ubunge wao, ama sivyo wataukosa.
Amesema wasijihesabu kuwa washindi hadi watakapofanikisha ushindi mkubwa wa wagombea wa chama hicho.
"Mpaka sasa msijihesabu kuwa washindi hadi mtakapopambana kwenye kampeni na kufanikisha ushindi mkubwa kwa mgombea wetu wa kiti cha rais Dkt Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani,"amesisitiza Chatanda.
Chatanda ametoa onyo hilo wakati wa kikao cha ndani kilichohudhuriwa na wateule hao wa ubunge wa Viti Maalumu cha kupanga mikakati ya ushindi wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Aidha, katika kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba, Dar es Salaam Agosti 29, 2025, Chatanda amewataka wabunge hao wateule kuvunja haraka makundi yaliyojitokeza wakati wa mchakato wa kura za maoni, ili kujenga umoja utakaoihakikishia CCM ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
Amesema kuwa kwa namna moja ama nyingine katika harakati za kutafuta kura za maoni kuna baadhi ya wagombea walioshindwa walijeruhiwa, hivyo inatakiwa kwenda kuzungumza nao kurejesha mioyo na imani zao kwa lengo la kuumpatia ushindi mkubwa mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wateule wa ubunge wa Viti Maalumu kupitia mikoa, vijana na makundi maalumu. Kimehudhuriwa pia na Spika wa Bunge ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson.
Kampeni zimeanza jana Agosti 28, 2025 kwa CCM kufanya uzinduzi uliofana kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe Jijini Dar es Salaam. Zitahitimishwa Oktoba 28, 2025 siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Chatanda akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya wateule wakiwa katika kikao hicho.
Comments