KISWAGA ATAJA MANUFAA TANZANIA KURIDHIA MKATABA WA WA KIMATAIFA WA MAZINGIRA WA GGGI

Na Richard Mwaikenda, Dodoma

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, amesema Tanzania itanufaika kwa kiasi kikubwa katika sekta ya mazingira na uchumi wa kijani iwapo Bunge litaridhia mkataba wa kimataifa wa Taasisi ya Global Green Growth Institute (GGGI).

Kiswaga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga, aliyasema hayo jana, Agosti 15, 2026, mjini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kamati yake kuhitimisha kikao cha kukusanya maoni ya wadau mbalimbali kuhusu mazingira, kilichofanyika katika Ukumbi wa Philip Marmo, Bungeni.

Alisema miongoni mwa manufaa yanayoweza kupatikana ni kuimarika kwa uwezo wa Tanzania kuibua na kuandaa miradi ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hatua ambayo itaongeza fursa za nchi kunufaika na mipango ya kimataifa ya mazingira.

Kiswaga alisema kuridhiwa kwa mkataba huo pia kutasaidia kuongeza taasisi za ndani zenye ithibati na uwezo wa kusimamia fedha kutoka mifuko ya kimataifa inayolenga mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutakuwa na fursa kubwa zaidi ya kupata fedha za misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mazingira na uchumi wa kijani,” alisema Kiswaga.

Aliongeza kuwa Tanzania inaweza pia kunufaika kwa kuongezeka kwa uwekezaji katika hatifungani za kijamii, pamoja na kuimarika kwa nafasi ya nchi katika diplomasia na ushawishi wake katika medani za kisiasa, kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Kiswaga, fursa nyingine ni kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania, hususan kupitia miradi na programu mbalimbali zitakazotekelezwa katika maeneo ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na uchumi wa kijani.

Alisema ushiriki katika taasisi hiyo utawezesha pia kuimarika kwa mbinu za kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia tafiti, huku wataalamu wa ndani wakipata nafasi ya kuongeza ujuzi, uzoefu na tija katika masuala ya ukuaji wa uchumi wa kijani.

“Ni muhimu kuona namna nchi yetu inavyoweza kutumia fursa hizi kuimarisha uwezo wa ndani, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

GGGI ni taasisi ya kimataifa inayolenga kukuza ukuaji wa uchumi wa kijani unaojumuisha ustahimilivu, shirikishi na endelevu kwa nchi wanachama.

Taasisi hiyo hushirikiana na nchi zinazoendelea na zinazoibukia kiuchumi katika kuandaa sera, mikakati na miradi inayolenga kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kililenga pia kupata maoni ya wadau kuhusu mkataba huo kabla ya hatua zaidi za Bunge katika mchakato wa kuuridhia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga


Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa pamoja na wadau wakati wa kikao hicho.



Mmmoja wa wadau akiuliza swali kwamba ni faida zipi za ziada Tanzania itapata ikijiunga na Taasisi hiyo?

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

KOCHA WA MC ALGERS AIHOFIA YANGA

VIONGOZI NA WATENDAJI WA MATAWI UVCCM PANGANI WANOLEWA

MAMBO 16 USIYOYAJUA KUHUSU RAIS MSTAAFU DKT. JAKAYA KIKWETE

NMB YAWAUNGANISHA WANANCHI NA HUDUMA, FURSA ZANZIBAR

HIZI HAPA TAKWIMU ZA PETER SHALULILE MCHEZAJI MPYA WA YANGA SC 🔰 🔥