TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD YATUA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

 



Na Mwandishi    Wetu - Mbeya 

16/8/2027 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI)Dkt. Diwani Msemo amesema kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Saratani ORCI Mbeya kutakuwa ni hatua muhimu katika kutimiza azma ya Serikali ya kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi za saratani karibu na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani.


Dkt. Msemo amesema Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 11 katika ujenzi wa kituo hicho ambacho kinatarajiwa kukamilika Januari 2027 na kuongeza uwezo wa kutoa huduma za uchunguzi, tiba na ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani katika ukanda huo.


Akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya ORCI katika mradi huo jijini Mbeya, Dkt. Msemo amesema ujenzi wa vituo vya kikanda ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupanua huduma za saratani nchini huku ORCI ikiwa na jukumu la kusaidia kusambaza huduma za kibingwa na kibobezi katika maeneo mbalimbali.


Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza mzigo kwa wagonjwa wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam kupata huduma maalumu za saratani.


“Tunapopanua huduma hizi kwenda katika kanda, tunamsogezea huduma mgonjwa badala ya kumlazimisha mgonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma",  amesema Dkt. Msemo.


Kwa mujibu wa Dkt. Msemo kituo hicho kina umuhimu wa kimkakati zaidi kutokana na nafasi ya Mbeya kama lango la Tanzania kuelekea nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Amesema uwepo wa huduma za saratani katika eneo hilo utatoa fursa kwa wagonjwa kutoka nchi hizo jirani kupata huduma ndani ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam hatua ambayo pia inaweza kuchochea utalii wa tiba.


“Kituo hiki kitakuwa na nafasi kubwa katika kutoa huduma kwa Watanzania na pia wagonjwa kutoka nchi jirani. Hii ni fursa ya kuimarisha utalii wa tiba katika ukanda huu", amesema.


Dkt. Msemo amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kupanua huduma za saratani nchini huku akibainisha kuwa kupitia mpango wa kudhibiti saratani wa mwaka 2012, ORCI ilipewa jukumu la kusambaza huduma za kibingwa na kibobezi katika maeneo mbalimbali nchini.


Amesema hadi sasa Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 60 kupitia ORCI katika kuboresha miundombinu ya huduma za saratani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na ongezeko la mzigo wa ugonjwa huo.


Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea, amesema saratani bado ni changamoto kubwa duniani na Tanzania.


Amesema takwimu za mwaka 2024 zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 20 duniani waligundulika kuwa na saratani, huku milioni 9.7 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.


Kwa Tanzania amesema inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya wa saratani wanafikia takribani 45,000 kwa mwaka huku karibu 30,000 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.


Dkt. Nyembea amesema sehemu ya saratani inaweza kuzuilika na nyingine kugundulika mapema hivyo Serikali inaendelea kuwekeza katika upanuzi wa huduma pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.


“Takribani asilimia 50 ya saratani zinaweza kuzuilika, na nyingine zinaweza kugundulika mapema”,  amesema.

Amesema uwepo wa vituo vya kikanda kama Mbeya utasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza safari ndefu kwa wagonjwa, huku Serikali ikiendelea na mpango wa kujenga vituo vingine katika maeneo mbalimbali nchini.



Kwa mujibu wa Dkt. Nyembea kituo kingine cha saratani kinatarajiwa kuanza kujengwa Arusha  huku mipango ikiendelea kwa ajili ya vituo vya Kigoma na Mtwara.


Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo, Ally Mtigita amesema ujenzi wa Kituo cha Saratani Mbeya ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Januari mwaka 2027.


Amesema mradi huo wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 10.4 umefikia asilimia 57 ya utekelezaji huku kazi zikiendelea kwa kasi ili kuhakikisha kituo kinakamilika kwa wakati.

Kituo hicho kinatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.


Uwekezaji huu unaashiria mabadiliko makubwa katika mfumo wa utoaji wa huduma za saratani nchini kutoka kutegemea zaidi vituo vichache vya kitaifa kuelekea mfumo wa huduma za kibingwa unaosogezwa karibu na wananchi.


Kituo cha Saratani cha ORCI  Mbeya kinapokamilika safari ya mgonjwa kutafuta huduma za saratani haitakuwa tena ndefu kama ilivyokuwa hapo awali; huduma zitakuwa karibu zaidi na matumaini ya kugundua na kutibu saratani mapema yataongezeka.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

KOCHA WA MC ALGERS AIHOFIA YANGA

VIONGOZI NA WATENDAJI WA MATAWI UVCCM PANGANI WANOLEWA

NMB YAWAUNGANISHA WANANCHI NA HUDUMA, FURSA ZANZIBAR

HIZI HAPA TAKWIMU ZA PETER SHALULILE MCHEZAJI MPYA WA YANGA SC 🔰 🔥