RIDHIWANI AKEMEA WANAOTUMIA UDINI KATIKA KAMPENI

Na Richard Mwaikenda,Tunduru.

MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza  Kuu la  Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Ridhiwani Kikwete, amekemea tabia ya baadhi waumini wa dini ya kiislamu kudhihaki dini zingine kwa kuwaita makafiri baadhi ya wagombea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea nchini.

Ridhiwani,alikemea tabia hiyo katika mkutano wa kampeni juzi mjini Tunduru, baada ya kupata taarifa kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wanatumia udini katika mikutano yao ya kampeni kwa kuwaambia wananchi kuwa wasimchague Mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinguzi (CCM), Injinia Ramo Makani kwa kumuita kafiri, kwa vile yeye ni mkristo.

"Jamani mimi pia ni mwislamu, si vizuri kumwita mwenzio kafiri, si neno zuri, kwani kila mmoja anayo haki ya kufuata imani ya dini anayoitaka na isitoshe katika uchaguzi huu hatutafuti Imamu wala Sheikh wa kutuongoza bali tunatafuta kiongozi imara wa kuleta maendeleo ya jimbo na nchi kwa ujumla,"alisema Ridhiwani huku akishangiliwa na umati wa watu katika mkutano uliofanyika Lindi mjini.

Alisema kuwa hata wakiamua kumchagua Imamu ama Sheikh kuwa mbunge, kwa hali ya kawaida hatokuwa na muda wa kwenda kuswalisha msikitini, kwani muda wake mwingi ikiwezekana hata kufikia miezi  sita ataupoteza kwa kuhudhuria vikao vya bunge Dodoma, hivyo kwenda tofauti na maadili ya kazi hiyo ya kiroho.

"Tusikubali kupenyeza chuki na fitina katika maisha yetu, tukiruhusu mambo hayo tutaangamia, hivyo tunatakiwa tuwaache maimamu na masheikh wafanye kazi ya dini na wanasiasa wafanye kazi  za kuiletea nchi maendeleo," alisema Ridhiwani.

Pia katika mkutano huo, Ridhiwani, alisifia kitendo cha mgombea wa CCM, Injinia Makani kujali imani ya dini ya kiislamu kwa kutoendesha kampeni katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kuwapa fursa waumini wa dini hiyo kuendelea na mfungo huo bila bughudha, tofauti na mgombea ubunge wa CUF ambaye ni muislamu kutojali jambo hilo muhimu kwa waislamu kwa kuendelea na kampeni wakati wa mfungo.

Licha ya Tunduru mjini, kugubikwa na ushindani mkubwa wa vyama vya CUF na CCM, lakini ujio wa Ridhiwani katika eneo hilo ulibadilisha hali na kuonesha uhai kwa CCM, kutokana na jinsi watu lukuki walivyojitokeza katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na  kiongozi huyo wa UVCCM Taifa, karibu na Soko la Azimio mjini humo.

Katika ziara hiyo ya kampeni ya kuweka mikakati ya ushindi mkubwa kwa CCM, Ridhiwani ameongozana na makada wengine wa chama hicho, miongoni mwao akiwemo mlemavu wa viungo, Haruna Mbeyu kutoka tawi la CCM, London Uingereza na Amon Anastas mlemavu wa macho ambaye kitaaluma ni wakili.

Tayari makada hao wameshafanya mikutano ya kampeni ya ndani, katika wilaya zote za mikoa ya Lindi,Mtwara na baadhi ya wilaya za mkoa wa Ruvuma. Wataendelea kuwasha moto katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Pwani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

DKT NCHIMBI AKARIBISHWA KIMILA NYUMBANI RUVUMA