CHENGE KUPOTEZA UBUNGE MWAKA 2015?



HUKUMU ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya Sh700,000 aliyopata mbunge wa Bariad Magharibi Andrew Chenge kwa kosa la matumizi mabaya ya barabara na kusababisha vifo vya watu wawili, inaweza kumkwamisha kugombea tena ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Chenge ambaye ni Mwansheria Mkuu wa zamani wa Serikali na Waziri katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alitiwa hatiani juzi na mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kivukoni-Kinondoni jijini Dar es Salaam, katika hukumu iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kwey Rusema.

Hata hivyo Chenge alifanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kukwepa kwenda gerezani na akachiwa huru.  Katiba ya Tanzania kifungu cha 67 kifungu kidogo cha (2) (c) kinabainishakuwa mtu hatateuliwa kuwa mbunge:
 "Ikiwa mtu huyo amehukumiwa na mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu.

"  Kinafungu hicho kinatafsiriwa na baadhi ya wadau wa masuala ya siasa kuwa kimemwondolea sifa Chenge kugombea ubunge mwaka 2015.  Mbali na kuwa mbunge wa jimbo la Bariad Magharibi, Chenge ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM. 
Hata hivyo mbali na maoni ya wadau hao, kitendo cha Mahakama kumwona Chenge ana kosa la kuendesha gari lisilokuwa na bima, linamfanya mwanasheria huyo wa zamani wa serikali kukosa sifa ya uaminifu inayowazuia watu kuteuliwa kuwa wabunge.  Lakini watalaamu kadhaa wa sheria waliochambua kifungu hicho cha Katiba, wameeleza kuwa kosa alilohukumiwa Chenge halimwondolei sifa za kuendelea kuwa mbunge au kuteuliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Sengondo Mvungi alisema kwa mujibu wa sheria Chenge  ataendelea kuwa mbunge kwa sababu  hajatumikia kifungo na badala yake amelipa faini.

Mvungi ambaye ni mtaalamu wa Katiba alisema,  “Kama angeenda moja kwa moja kutumikia kifungo asingekuwa na sifa ya kuitwa mbunge na hata uchaguzi ujao asingeweza kugombea tena lakini, kwa sababu kalipa faini tu, hajapoteza ubunge wake.”  
Mtalaamu mwingine wa Sheria Profesa Abdallah Safari alifafanua kwamba kama zingekuwa zinatumika sheria za zamani, kwa hukumu hiyo, Chenge asingeweza kugombea tena ubunge.  “Unajua hata sheria mpya ya uchaguzi sijaipitia kuona inasemaje kuhusu suala hili lakini, ninachoweza kukumbuka ni kwamba sheria ya zamani ya makosa yote yaliyokuwa yakihusu ‘mortality’ ulikuwa huwezi kugombea tena. Sasa sijui kwa sheria hii ya sasa,”alisema Profesa Safari.

 Wakili wa Mahakama Kuu, Harlod Sungusia alisema hukumu ya Chenge haina madhara yeyote kwake katika nafasi zake kisasa.  Sungusia ambaye alitumia muda wake kukosoa sheria na katiba za Tanzania kuwa ni mbovu alisema kwa mujibu wa sheria, hakimu alifanya kazi yake bila ya tatizo lolote.  “Hukumu ilikuwa sahihi wala hakimu hakukosea kuitoa. Kilichopo pale ni kwamba makosa aliyokutwa nayo Chenge si ya kukosa uaminifu hivyo, hayamfutia nafasi yake ya kuendelea kuwa Mbunge,”alisema Sungusia ambaye alisema hakimu pia alitakiwa kuongeza kipengele cha fidia kwa wafiwa. 
Katika maoni yake hayo Sungusia aliishukia katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akisema ina matatizo na hilo ndilo zao la sheria mbovu zenye kutoa hukumu kama hiyo.  “Ndugu zangu tunaposema sheria zetu ni mbovu ni pamoja na hii.

Katika hilo hakimu alifanya kazi yake kwani yeye hufanya kazi ya kutafisili sheri tu. Lakini ukitazama uhalisia ndipo utagundua kuwa sheria zetu zina matatizo,”alieleza Sungusia.  Sungusia alitoa mfano wa mtu aliyeiba Shati kuwa anaweza kutupwa jela hata miaka saba lakini, kosa kama alilokutwa nalo Chenge, likabaki na adhabu ndogo.  Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema Erasto Tumbo alisema hukumu iliyotolewa dhidi ya ya change haina matatizo ingawa alisema imeongeza kilio kwa wafiwa.

“Hukumu hiyo haina tatizo lolote na hakimu alitimiza wajibu wake lakini, imeongeza kilio mara mbili kwa wafikiwa kwa kuwa watu hao hawatalipwa fidia,”alisema Tumbo.  Tumbo alifafanua kwa wafiwa hawatalipwa fidia kwa kuwa gari lililowagonga halikuwa na bima.  Mwanasheria maarifu hapa nchini  Alex Mgongolwa,  alisema kwa sheria zilizopo, Chenge ataendelea kuwa Mbunge kwa sababu ametiwa hatiani kwa makosa ambayo hayahusiani na uaminifu.

Alisema kama angehukumiwa kwa kosa linalohusiana na uaminifu kama vile wizi au rushwa, nafasi yake ya ubunge katika jimbo la Bariadi Magharibi angeipoteza.  Katika kesi hiyo Chenge alishtakiwa kwa makosa manne; kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha vifo vya watu wawili, kuharibu mali na kuendesha gari isiyokuwa na bima. 

Awali hukumu dhidi ya kiongozi huyo ilikuwa isomwe Desemba 16, mwaka huu, lakini iliahirishwa hadi jana kutokana na kile ambacho hakimu Rusema alisema kuwa ni Chenge kuwa safarini jijini Mwanza alikoenda kuhudhuria msiba.
Hatimaye kesi hiyo ilifikia tamati yake rasmi jana baada ya machakato wa kusikilizwa kwake uliochukua karibu miaka miwili kukamilika.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba Machi 27 mwaka 2009 katika makutano ya barabara ya Haileselasie na Ali Hassan Mwinyi eneo la Morogoro Store jijini Dar es Salaam, Chenge aliigonga bajaji na kuwaua wasichana wawili waliokuwa abiria kwenye bajaji hiyo; Beatrice Constantine na Victoria George.  Kesi hiyo ilifunguliwa mahakama hapo kwa mara ya kwanza Machi 31 mwaka 2009 na kuanza kusikilizwa mwezi Aprili mwaka 2010. 

Akitoa hukumu ya kesi hiyo juzi, hakimu Rusema alisema mahakama imeona Chenge ana hatia katika makosa yote manne na hivyo kumtoza faini ya Sh700,000 ama kifungo cha miaka mitatu jela.  "Katika kosa la kwanza na la pili, mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh 250,000 kwa kila kosa au kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kila kosa hilo," alisema Hakimu Rusema.  Aliongeza "Katika kosa la tatu na kosa la nne, mshtakiwa atalipa Sh 100,000 kwa kila kosa au kifungo cha miezi 6 kwa kila kosa hilo.

Hivyo, atatakiwa kulipa jumla ya Sh 700,000 kwa makosa yote au kwenda jela miaka mitatu."   Kabla ya kusoma hukumu hiyo hakimu Rusema alimpa Chenge ambaye alikuwapo mahakamani hapo nafasi ya kujitetea, lakini badala yake alisimama wakili wake.  Akitoa utetezi wa mtuhumiwa huyo wakili Senen Mponda alisema," Hili ni kosa la kwanza kwa mshtakiwa. Mshtakiwa ni kiongozi wa umma na kuhusu bima ilikuwa bahati mbaya.

"  "Naomba apunguziwe adhabu ili apate kuendelea na shughuli zake za kuutumikia umma."  Awali ilielezwa mahakamani hapo kuwa Machi 27 mwaka 2009 kati ya saa 8.15 na 8.30 usiku katika eneo la Oyesterbay, makutano ya barabara ya Haile Selasie na Ally Hassan Mwinyi,  Chenge akiwa anandesha gari binafsi aliigonga bajaji hiyo na kusababisha vifo vya watu wawili.  Ilielezwa kuwa Chenge aliigonja bajaji hiyo akiwa na gari aina ya Toyota Hillux Double Cabin wakati akirudi nyumbani kwake akitokea klabu ya British Legion akiwa kwenye mwendo wa kati ya ya kilomita 70 hadi 100 kwa saa.    


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

DKT NCHIMBI AKARIBISHWA KIMILA NYUMBANI RUVUMA