NGELEJA ABEZA MSIMAMO WA TUCTA

Na John Daniel wa gazeti la Majira

WAZIRI wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja amekejeli tishio la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), kutaka kuandamana kupinga ongezeko la bei ya umeme na kueleza kuwa Watanzania si wajinga kuburuzwa na watu wenye
maslahi binafsi.
Alisema kiwango cha juu kilichoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (UWURA) ni sh. 28 kwa kila uniti moja katika matumizi ya kawaida, kiasi ambacho kwa mujibu wa Bw. Ngeleja si kikubwa kama inavyotafsiriwa na TUCTA na baadhi ya watu.
Kwa kiwango hicho, mteja wa TANESCO alikuwa anatumia uniti 100 za umeme kwa mwezi, kuanzia Jumapili atalazimika kutoa sh 2,800 zaidi ya bei aliyokuwa anatoa awali.
"Nilichoelewa ni kuwa TUCTA walikurupuka kutoa kauli bila kujua ukweli wa kiwango gani kilichoidhinishwa, kilichoongezeka kwa kila uniti ni sh. tano, sh. tisa, sh. 11 na kiwango cha juu kabisa ni sh. 28, kutegemea na aina ya matumizi.
“Hivi ni nani akipewa sh. 28 anaweza kununua chochote kwa dunia ya leo, wasidhani Watanzania ni wajinga wanaweza kuburuzwa tu na fikra binafsi za watu kujitafutia umaarufu hapana tutafute ukweli jamani," alihoji Bw. Ngeleja.
Alisema TANESCO iliomba ongezeko hilo kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na kwamba mara ya mwisho bei hizo ziliongezwa Januari 2008.
"Serikali kwa maana ya TANESCO inatambua uwezo wa wateja wake ndio maana inajitadi kubeba sehemu kubwa ya gharama za umeme, ukiangalia tangu mwaka 2008 bei ya vitu ikiwemo mitambo imepanda kwa kiasi kikubwa," alisema Waziri Ngeleja.
Tanesco ilikuwa imeomba ongezeko la asilimia 34.6 lakini EWURA baada ya kusikiliza hoja za wadau ikapitisha asilimia 18.5.Wakati huo huo TANESCO imetoa taarifa inayoonesha mchanganuo wa ongezeko la bei mpya ya umeme kwa watumiaji kulingana na matumizi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kundi la watumiaji wadogo majumbani (D1) itapanda kwa sh. 11 kwa uniti moja hivyo kuwa sh. 60 kwa uniti badala ya sh.49 za awali.
Kundi la watumiaji wa kawaida (T1) ambao ndio wamepanda zaidi watalipa sh 157 kwa uniti moja kutoka sh. 129 za awali, sawa na ongezeko la sh. 28 kwa uniti moja.
Taarifa hiyo ya TANESCO imetaja kundi la mahitaji ya juu ya msongo mdogo (T2) kuwa na ongezeko la sh. tisa kwa kila hivyo na kufikia bei ya 94 kutoka sh. 85 za awali.Kundi la mahitaji ya juu ya msongo mkubwa (T3/T3a) ongezeko ni sh. tano kwa uniti, hivyo kupanda kutoka sh. 79 ya awali hadi sh. 84.
Kundi la mwisho linalohusu Tanzania visiwani (T5/T3b) ongezeko ni sh. nane kwa uniti moja hivyo gharama zitapanda kutoka sh. 75 hadi 83 kwa kila uniti moja.Wiki iliyopita Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nicholas Mgaya, aliitaka Serikali kufuta uamuzi wa kupanda kwa bei ya umeme na kutishia kuandaa maandamano ya amani nchi nzima kupinga hoja hiyo.
Bw. Mgaya alisema Kamati ya Utendaji ya TUCTA ilifikia maamuzi hayo kwa maelezo kuwa ongezeko hilo ni kubwa na haliendani na hali ya Mtanzania na hivyo litazidisha ugumu wa maisha kwa wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

DKT NCHIMBI AKARIBISHWA KIMILA NYUMBANI RUVUMA