YANGA KUTUMIA BIL 4.5 KWA UKARABATI

 OAfisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu
KLABU ya Yanga inatarajia kutumia shilingi 4.5 Bilioni  kwa ajili kukarabati Uwanja wao wa Kaunda na kukarabati jengo lao la  mtaa wa Mafia Jijini Dar es Salaam ili liwe la kisasa zaidi, ukarabati ambao utachukua miaka miwili.

Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kwa sasa wameshaingia mkataba na Kampuni ya Nedco ambayo imeshaanza uchoraji ramani wa Jengo hilo ambalo litakuwa na gorofa 10 pamoja na ukaguzi wa uwanja kabla hawajaanza kazi rasmi.

Alisema kuwa makubaliano hayo ya kuanza kwa ujenzi huo yamefikiwa baada ya Kamati ya kuendeleza Miradi ya Yanga kukutana ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Baraka Igangula na ikiwa na wajumbe nane.

Alisema uwanja huo wanataka kuutengeneza na kuwa wa kisasa zaidi ambao utachukua mashabiki elfu 25.

Alisema kwa sasa klabu yao haina fedha, ila kampuni ya uchoraji itakapokamilisha uchoraji wa ramani, klabu ya Yanga itakuwa ikifanya tafrija mbali mbali kama kuandaa chakula na kuwaarika waheshimiwa na makampuni mbali mbali kwa ajili ya kuchangia na kufanya matamasha ambayo yataiingizia Yanga fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Wakati Sendeu akisema hivyo mwanzoni mwa mwaka jana uongozi wa Yanga chini ya mwenyekiti wake Iman Madega kwa kushirikiana na mfadhili wao mkuu Yusuf Manji waliahidi kujenga uwanja huo na kufanya ukarabati mkubwa wa makao makuu ya klabu hiyo.

Katika hatua ya awali, akishirikiana na uongozi wa Yanga, Manji alianza ukarabati wa jengo ikiwamo kupakwa rangi ili liendane na hadhi yake na baada ya hapo, aligeukia ukarabati wa Uwanja wa Kaunda na jengo, ili kuifanya klabu kuwa ya kisasa kwa gharama ya zaidi ya Shs 900m.

Kwa mujibu wa Madega, uwanja huo ulitakiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 15, 000 waliokaa, ili baadhi ya mechi za Ligi Kuu kuanzia mzunguko wa pili wa msimu huu zichezewe uwanja wa Kaunda.

Lakini hadi sasa ukarabati wa jengo na uwanja bado haujakamilika hali iliyosababisha Manji kutishia kujitoa kuifadhili klabu hiyo mwishoni mwa mwezi Novemba huku akiwalalamikia watendaji wa Yanga kwamba wamekuwa wazito katika kuchangamkia vitu vya maendeleo akitolea mfano duka la klabu hiyo ambalo mpaka leo halijapangishwa pamoja na watu ambao walipewa jukumu la kuhakikisha watu waliovamia kiwanja cha Yanga, Mtaa wa Twiga na Jangwani wanaondolewa ili ujenzi wa uwanja uanze mara moja, lakini watu hao wamekuwa wazito kitu ambacho kinamkatisha tamaa.

Pia Sendeu aliongelea kuhusu suala la mchezaji wao Abdi Kassim ambaye anatakiwa na klabu ya Dong Long Ham ya Vietnam.

Sendeu alisema wamekuwa wakiendelea na mazungumzo na timu ya Dong Long Ham ya Vietnam mpaka sasa, ambapo klabu ya Dong Long Ham inataka kutoa dola 35,000 lakini Yanga inataka Dola 40,000 hivyo bado wanaendelea na mazungumzo na endapo watakubaliana basi watamuuza mchezaji huyo.

Kwa upande wa ushiriki wao katika michuano ya Mapinduzi, Sendeu alisema Yanga itaondoka Dar es Salaam siku ya  Jumapili ikiwa na wachezaji 22 na viongozi watano.

Alisema wachezaji watakaobaki ni wale watano waliopo kwenye timu ya Taifa na wengine wawili ambao ni majeruhi Athuman Idd 'Chuji' anayesumbuliwa na kuchanika kwa misuli na Shamte Ally ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni.

Afisa Habari wa Yanga alisema kabla timu hiyo haijaondoka kesho itacheza mechi ya kirafiki na JKT Ruvu kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo ya kombe la Mapinduzi. .

Sendeu alitaja viingilio katika mchezo huo kuwa VIP sh7,000, Jukwaa kuu sh 5,000, Kijani sh 3,000 na Mzunguko ni sh 2,000.

Katika Hatua nyingine Sendeu alizungumzia usajili wa mchezaji wao Green Atupele kutoka kikosi cha pili ambaye amepandishwa kikosi cha kwanza kuwa hakusajiliwa kwa sh 15 milioni, ila Atupele na mwenzake John Simbeya walisajiliwa kwa 3.5 milioni.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

DKT NCHIMBI AKARIBISHWA KIMILA NYUMBANI RUVUMA