CHANGAMKIENI UJIO WA KAMPUNI YA BAJAJI

Bajaji juu
na Nasra Abdallah wa Tanzania Daima
WAJASIRIAMALI wanaojishughulisha na utengenezaji wa vipuri vya magari wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa kampuni ya bajaji kutoka nchini India itakayoanza kazi zake baadaye mwaka huu hapa nchini.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda na Masoko, Cyrill Chami, katika ziara yake ya siku moja ya kukutana na wajasiriamali hao wanaosimamiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo nchini (SIDO).
Chami alisema Januari 3 hadi 9 mwaka huu walipokwenda ziarani nchini India kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji hapa nchini, mojawapo ya kampuni kubwa zilizoahidi kuja kuwekeza ni kampuni hiyo ya bajaji ambayo ilisema ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa itakuwa ishawasili hapa nchini.
Katika uwekezaji huo,waziri huyo alisema hataki kuona fursa za ajira zikienda kwa wananchi wa nchi nyingine na badala yake alitaka ajira hizo zibakie hapahapa nchini.
Chami alisema, kampuni hiyo katika bajaji kifaa kilicho chake ni injini tu huku vifaa vingine kama matairi vipuri na bati za kumalizia hupelekewa na wajasiriamali wa nchini humo.
“Tulipotembelea kampuni hiyo, ambayo inaaminika kuwa ni ya tatu kwa ukubwa katika kampuni zilizopo India, tulishuhudia magari makubwa yakitoka maeneo mbalimbali yakifika kiwandani hapo kila moja likiwa na aina yake ya bidhaa kwa ajili ya kutengenezea bajaji, hivyo Watanzania wenzangu naomba msiniangushe katika hili,” alisema waziri huyo.
Mbali na kuanzisha kiwanda, pia mwekezaji huyo aliahidi kujitolea kuwapa mafunzo wajasiriamli hao ya namna ya kuweza kutengeneza vipuri vyenye ubora, ambapo mbali na kuuzia kiwanda pia wataweza kuuza nchi za nje.
Kwa upande wake, wajasirimali hao walizitaja baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kuwa ni pamoja na kodi kubwa ambazo wamekuwa wakitozwa pindi wanapoagiza mashine za kutengenezea vipuri hivyo jambo linalowakatisha tamaa.
Probi Salakana mmoja wa wajasiriamali hao alisema changamoto nyingine ni ugumu wa upatikanaji wa vyuma jambo ambalo walidai limechangiwa na uuzaji holela wa vyuma chakavu na hivyo kupandisha thamani ya vyuma ambapo walishauri ni vyema biashara hiyo ikapigwa marufuku.
Mathias Mbunda, yeye alisema utumiaji wa teknolojia ya kizamani umekuwa ukiwagharimu kwa kiasi kikubwa kwani wengi wao hutumia gesi au makaa ya mawe katika kuyeyusha au kukatia vyuma ambayo kwa sasa nishati hizo hupatikana kwa tabu na hata pale zinapopatikana basi bei yake huwa kubwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwanda Vidogo vidogo ,Pius Wenga, alisema lengo la shirika hilo ni kuona jinsi gani wataweza kuwatoa wajasiriamali hao huko waliko na kuwa wajasiriamali wakubwa kimtaji na hata kimasoko.
Alisema moja ya malalamiko ambayo wamekwa wakikumbana nayo kutoka kwa wajasiriamali hao ni suala la upatikanaji wa mikopo ambayo ina masharti magumu kwao.
Katika ziara hiyo,Waziri Chami ambaye alikuwa ameongozana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mauzo Nje (APZA), Dk. Adelhelm Meru, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA), Allan Kiula, waliweza kuwatembelea wajasiriamali wa Gerezani Kariakoo, Tabata Dampo na SIDO Vingunguti.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

CHAMA KIPYA CHA WALIMU WAMUOMBA RAIS SAMIA AINGILE KATI MAKATO YA WANACHAMA WAO

TOFAUTI YA WATU WA DAR NA WA MKOANI NI HUU

IBENGE: YANGA SC WATAFUZU HATUA YA ROBO FAINALI.

NILIYOYABAINI KATIKA TRENI YA SGR DAR ,MORO HADI DODOMA … KADOGOSA REKEBISHENI MAMBO HAYA MTANIKUMBUKA