DK SLAA; TUTAJIBU MAPIGO YA POLISI

Katibu Mkuu wa CHADEMA.Dk. Slaa:

na Betty Kangonga wa Tanzania Daima
 CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinaandaa mikanda ya video itakayoonyesha matukio yote yaliyotokea wakati wa vurugu zilizozaa maafa wakati wa maandamano ya wanachama wa chama hicho katika Jiji la Arusha mwanzoni mwa mwezi huu.
Hatua hiyo ya Chadema kuandaa mikanda ya tukio hilo inakuja kama majibu ya kile kilichofanywa na Jeshi la Polisi ambalo kwa siku kadhaa wiki iliyopita lilisambaza katika vituo vya televisheni video za matukio ya Arusha ambazo zimezusha manung’uniko ya chini kwa chini kutoka kwa wananchi wa Arusha na ndani ya chama hicho cha upinzani.
Katika kujibu mapigo ya polisi, chama hicho kimesema hakina la kuficha kama walivyofanya viongozi wa jeshi hilo, badala yake wataonyesha tukio zima kabla, wakati na baada ya mkutano wao uliofanyika kwenye viwanja vya NMC Januari 5 mwaka huu.
Mgogoro kati ya polisi na Chadema ulitokana na maelekezo tofauti ya kutofanya maandamano kwa mujibu wa amri ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) iliyotolewa saa chache kabla ya kuanza kwa maandamano hayo yaliyosababisha jeshi kutumia risasi za moto na mabomu kuwatawanya waandamanaji hao.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Willibrod Slaa alisema kwa sasa wanakamilisha mkanda huo ambapo utatolewa kwa waandishi wa habari na umma wakati wowote kuanzia leo.
Dk. Slaa alisema ingawa Jeshi la Polisi limetoa mkanda wao bado wana nafasi ya kuufahamisha umma kwa kutoa mkanda ambao haujahaririwa ili umma ufahamu kilichotokea.
“Kama lilivyofanya Jeshi la Polisi sisi hatutaki kuzungumzia lolote juu ya mkanda wao… ila tunategemea kuonyesha ‘documentary’ ya tukio zima hatua kwa hatua bila kuhariri kisha hapo ndiyo tutatoa kauli yetu,” alisema Dk. Slaa ambaye alionyesha dhahiri kukerwa na video za polisi ambazo zinalalamikiwa kwa ‘kuchakachuliwa’.
Alisema kwa sasa timu nzima ya viongozi wa chama hicho iko mikoani na inatarajia kurudi ili kuhakikisha inatoa taarifa yenye uhakika ya vurugu za maandamano hayo yaliyosababisha watu watatu kupoteza maisha na wengine 29 wakijeruhiwa kwa risasi na mabomu.
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi lilivitangazia vyombo vya habari kuwa IGP Said Mwema angekuwa na mkutano na waandishi wa habari lakini waandishi walipofika ofisini kwake alijitokeza Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja ambaye alitoa tamko akiwatuhumu wafuasi na viongozi wa Chadema kwa vurugu zilizosababisha mauaji kwenye mji huo wa kitalii.
Kamishna huyo aliwawekea waandishi wa habari mkanda wao wa video ambao haukuonyesha namna viongozi wakuu wa Chadema walivyokamatwa huku pia ukiwa hauna picha za matukio mengine ambayo yalionyeshwa katika vituo tofauti vya televisheni siku ya tukio na siku moja baadaye.
Kamishna Chagonja alitumia maelezo ya mdomo, maandishi na picha za video kuwaeleza wanahabari kile alichokiita “taarifa ambazo wananchi hawajaambiwa kuhusu vurugu za Arusha zilizotokea Januari 5 mwaka huu” ambazo kimsingi zilibeba tuhuma dhidi ya viongozi wa Chadema kuwa chanzo cha vurugu.
Hata hivyo, picha za video zilizoonyeshwa kwa wanahabari zilionekana dhahiri kupingana kwa kiasi kikubwa na maelezo na sababu zilizotolewa kama kigezo cha kuyasambaratisha maandamano hayo kwa silaha.
Picha hizo zilionyesha kundi moja tu la viongozi na wafuasi wa Chadema lililoanza maandamano kwa amani kutoka eneo ilipo Hoteli ya Mount Meru likitumia njia moja kuelekea Sanawari Mataa na hakukuonekana makundi mengine yaliyokuwa yakitumia njia nyingine kuandamana ambayo yangeleta bugudha na kuwapa polisi shida ya kulinda kama alivyodai kamishna huyo.
Aidha, picha hizo za video pia hazikuonyesha waandamanaji walioanza kufanya fujo au kuashiria kufanya fujo mpaka walipofika eneo la Sanawari Mataa ndipo Jeshi la Polisi lilipovuruga hali ya amani kwa kuanza kufyatua mabomu ya machozi.
Kwa upande mwingine, sinema hiyo iliyorekodiwa na Jeshi la Polisi kuhusu matukio yaliyotokea Arusha haikuonyesha mazingira ya kujeruhiwa kwa Josephine Mushumbusi ambaye ni mchumba wa Dk. Slaa.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

CHAMA KIPYA CHA WALIMU WAMUOMBA RAIS SAMIA AINGILE KATI MAKATO YA WANACHAMA WAO

NILIYOYABAINI KATIKA TRENI YA SGR DAR ,MORO HADI DODOMA … KADOGOSA REKEBISHENI MAMBO HAYA MTANIKUMBUKA

DK. KIKWETE AZINDUA KITUO CHA AFYA KIZIMKAZI, APONGEZA MAENDELEO ZANZIBAR

KOCHA WA MAMELODI ASIMAMISHWA KWA KUWAPIGA CHABO WACHEZAJI WAKE WA KIKE