Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima y Afya Deogratius Ntunkamazina akisisitiza umuhimu wa kuutumia Mfuko huo kwa manufaa ya Watanzania wote kwenye Mkutano wa wadau uliofanyika mkoani Lindi.
Na Grace Michael, Lindi
MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Deogratius Ntunkamazina amewataka watoa huduma za afya nchini kuutumia Mfuko huo kwa uzalendo ili uweze kunufaisha Watanzania wote.
Amesema kuwa endapo Mfuko huo watautumia kwa ulafi na kwa kughubikwa na udanganyifu utafilisika na kushindwa kufikia malengo yanayokusudiwa na Serikali ya kuhakikisha asilimia kubwa ya wananchi wanakuwa kwenye utaratibu wa Bima ya Afya.
Bw. Ntunkamazina aliyasema hayo jana wakati akitoa salaam za Bodi ya Mfuko huo kwenye Mkutano wa Wadau uliofanyika mkoani Lindi uliokutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakitoa huduma, wanachama, viongozi wa kiserikali, kidini na wadau wengine.
"Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni fursa nzuri ya kuboresha huduma za afya nchini hivyo tumieni fursa hii kwa uzalendo mkubwa sana ili baadae wananchi wote waweze kunufaika na Mfuko huu. Mkiwa walafi na kuweka udanganyifu mwingi katika kuandaa madai yenu mtaufilisi Mfuko huu," alisema Ntunkamazina.
Mwenyekiti huyo wa Bodi alitumia maneno ya Kiongozi shupavu na mwana Falsafa Mahtma Gandhi kiongozi wa India, ambaye alinukuu maneno yake aliyowahi kusema kuwa “Dunia hii ina raslimali za kutosha mahitaji muhimu ya kila mtu lakini haina raslimali za kutosha ulafi wa kila mtu” mwisho wa kunukuu. Hivyo kwa kauli hiyo alisisitiza uzalendo katika kuutumia Mfuko huo.
Alisema kuwa endapo Mfuko huo utatumika ipasavyo Watanzania wote watanufaika lakini ukitumika isivyo utafilisika.
"Jamani hata Rais wetu ana ndoto kubwa na angependa kabisa aondokapo madarakani mwaka 2015 aache Watanzania asilimia 50 wakiwa chini ya utaratibu wa Bima ya Afya hivyo tumuungeni mkono kwa kila mdau kutimiza wajibu wake," alisema.
Naye Kaimu Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Magalula Said naye aliwasisitiza viongozi wote wa Halmashauri kuhakikisha wanaongeza juhudi katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii.
"Nimejaribu kupitia takwimu za hapa Lindi na nimegundua kuwa tunazidi kuporomoka katika suala hili la CHF hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ajipange kuhakikisha hali hii inaondoka na wananchi wetu wanajiunga na Bima kwani ndio mkombozi wa afya kwa wote hivyo ni lazima tuiweke kama agenda ya kudumu katika vikao vyetu,' alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba aliwaomba viongozi wa kisiasa wakiwemo madiwani kuhakikisha wanasimamia vyema fedha zitokanazo na mifuko hiyo ili ziweze kutumika katika matumizi sahihi hasa ya dawa.
Comments