NENO AU JINA BONGO FLAVA;CHANZO CHAKE NINI AU NANI?


Historia ya muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava kama unavyojulikana miongoni mwa wengi hivi leo una historia ndefu. Ni historia ndefu kiasi kwamba hivi leo wengi hatukumbuki tena hata muziki huu ambao hivi leo umetokea kuwa kipenzi cha wengi ulianzaje,ukapitia hatua na harakati gani mpaka kufikia hapa ulipo hivi leo.

Miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo wa harakati za mwanzo kabisa za muziki wa bongo flava ni aliyewahi kuwa DJ maarufu nchini Tanzania kwa jina Mike Pesambili Mhagama(pichani).Mike sio tu miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo bali pia ni miongoni mwa watu wachache walioamini katika muziki wa kizazi kipya tokea mwanzo.Kumbuka hizo ni zile enzi ambapo muziki huo ulikuwa ukichukuliwa kama “uhuni” tu na sio aina mpya ya muziki au burudani.Ni watu wachache sana walioweza kutabiri hatua ambazo muziki huo ungepiga miaka kumi au kumi na tano baadaye.
Lakini pia Mike amekuwa akikerwa na jinsi ambavyo kumekuwepo na upotoshwaji au upindishwaji wa vipengele fulani fulani muhimu vya historia ya muziki huo. Katika kujaribu kuiweka vyema historia hiyo,Mike Mhagama ameandika kwa mapana na utulivu wa kina kuhusu harakati za mwanzo za muziki wa kizazi kipya,suluba walizopitia yeye na watangazaji wenzake katika kuutambulisha muziki huo,wadau mbalimbali anaowakumbuka katika harakati hizo,wanamuziki wenyewe,promoters wa muziki nk.


Pia Mike Mhagama,anaweka wazi kitu ambacho watu wengi wamekuwa wakijiuliza;Nini chanzo cha neno Bongo Flava? Nani mwanzilishi wake?Kwa jibu hilo na historia nzima,kwa jinsi anavyoikumbuka Mhagama, msome kuanzia hapo chini,kwa maneno yake mwenyewe, kama tulivyoyanakili kutoka katika blog yake(kwa ruhusa na baraka maalumu).Habari imegawanyika katika sehemu nne ili iwe rahisi kwako kuzisoma na kuelewa vyema anachokizungumzia Mike Mhagama. Mwenyewe anasema yawezekana kabisa asiwe sahihi kwa asilimia zote na ndio maana anapenda kukaribisha hoja,maoni na masahihisho yoyote kutoka kwako msomaji.Mike Mhagama hivi sasa anaishi huko Los Angeles,California nchini Marekani.
CHIMBUKO LA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA NA MAANA HALISI YA NENO BONGO FLAVA.
Na Mike Mhagama-Los Angeles,Marekani.
SEHEMU YA KWANZA

M
oja kati ya mambo niyapendayo mno maishani ni muziki.Nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa muziki si tu ule wa nje lakini kwa karibu ule wa nyumbani hasa muziki wa dansi na ule wenye umaarufu sana hivi sasa ujulikanao kama Bongo Flava (Muziki wa Kizazi Kipya).Katika mapenzi hayo imekuwa kama bahati kuwa mmoja wa vijana wengi tuliobahatika kuuona muziki huu wa kizazi kipya ukizaliwa na pengine bahati zaidi bila kusita kusema;kuwa mmoja kati ya wale tulioanzisha kusukuma gurudumu la muziki huu kufikia hapa ulipo na nafasi yake kutambulika si tu Afrika Mashariki bali pia kwa sasa duniani kwa ujumla.
Kama ilivyo kwa aina zingine za muziki Tanzania,mfano muziki wa dansi basi utakuwa mkosefu wa fadhila bila kujumuisha majina kama Patrick Balisidya,Mbaraka Mwaruka Mwinshehe,Salum Abdalah na hata Remmy Ongara.Hawa ni vinara na walifanya kila wawezalo kuja na ubunifu si tu kuvutia wateja wao bali kuutangaza muziki wao ndani na nje ya nchi na kuipa Tanzania kitambulisho chake kwenye jukwaa la sanaa ya muziki.Kazi za wanamuziki hawa zilifana sana kwa ushirikiano mkubwa na chombo ambacho kwa Tanzania ni muhimu sana katika kueneza au kutambulisha kitu kipya,RADIO.Watangazaji kama Mzee Ibrahim Chimgege,Enock Ngombale,Timothy Pata,Abisai Stephen,Seif Salum Nkamba na Julius Nyaisangah chini ya ma-bwana mitambo mahiri kama akina James Mhilu na Crispin Lugongo wanastahili pongezi kwa kiasi kikubwa katika kurekodi na kusimamia mitambo wakati wanamuziki hawa wakitafuta majina na namna ya kujitambulisha kwa jamii itakayosikiliza muziki wao.Bahati mbaya huwasikii sana watu hawa katika zinazoitwa historia kwa sababu wengi ni rahisi kuwasahau lakini mchango wao ni mkubwa sana na unastahili heshima hasa unapoandika au kuizungumzia historia ya muziki wa dansi Tanzania.Chanzo Bongo Clebrity

Comments

Anonymous said…
hivi huyu mike mhagama jamaa yuko wapi siku hizi alikuwa anatisha sana na sauti yake nzito na ufundi wa kuzungumza lugha na vitu vya kueleweka kwenye vipindi vyake,vijana wa siku hizi inabidi wajifunze walaahi.tumaizie hiyo historia kamanda.

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU