PIGA UA SIMBA LEO LAZIMA ISHINDE;KOCHA

KOCHA wa Simba Curkovic Milovan amesema haipo sababu kwanini kikosi chake kishindwe kupata mabao ya mapema kwenye mechi ya kwanza raundi ya tatu, Kombe la Shirikisho dhidi ya Al-ahly Shandy ya Sudan kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Milovan anaamini kuwa, ushindi wa mapema na mabao ya kutosha kwenye mchezo huo, utakuwa mhimili muhimu wa kuvuka kikwazo katika mchezo wa marudiano, nchini Sudan wiki mbili baadaye.

Simba ilifika hatua hiyo baada ya kutumia nguvu nyingi kuziondoa kwenye mashindano miongoni mwa timu bora na ngumu katika kinyang'anyiro hicho, Kiyovu ya Rwanda na ES Setif ya Algeria.

Ilitoka sare ya bao 1-1 na wawakilishi wa Rwanda katika mchezo walioanza ugenini, na kisha kuja kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.

Raundi ya pili, iliifunga ES Setif 2-0 kwenye mechi ya nyumbani, na kisha kufungwa mabao 3-1 ugenini, kipigo ambacho hakikuwakwaza kusogeza mguu mbele kwa mzani wa sheria ya faida ya bao la ugenini.

Milovan atawategemea washambuliaji wake mahiri, akiwemo Emmanuel Okwi, Felix Sunzu, Patrick Mafisango na Haruna Moshi 'Boban' kuipenya na kufunga mabao ya kutosha dhidi ya ngome ya wapinzani wao, ambao sehemu kubwa ni vijana.

Simba imekuwa ikijifua vya kutosha kwenye viwanja wa Sigara, na kocha Milovan anaamini robo ya kwanza ya dakika 45, tayari watakuwa wameshazigusa kamba za wapinzani wao mara kadhaa.

"Nataka washambuaji wawe na kazi mbili, kwanza wahakikishe wanafunga magoli mapema, hii itasaidia kuwachanganya wapinzani wetu, pili wawe makini na washirikiane vyema na wenzao ili kuwanyima mwanya wa kupata bao la ugenini," alisema Milovan.

Pengine kama kuna kitu kinamnyima raha Milovan, basi ni kukosekana kwa beki wake wa kati, Juma Nyoso ambaye kadi nyekundu aliyopewa ugenini, Algeria inamuweka kando kwenye mchezo wa kesho.

"Nafikiria kumchezesha Mafisango katikati, halafu nafasi yake acheze Kapombe, lakini bado sina jibu la mwisho kwani nafasi ya Kapombe itaelemewa. Nina mashaka bado, naangalia nini cha kufanya," alisema Milovan.

Wakati Milovan akikuna kichwa kuelekea mchezo huo, wachezaji wa Simba wamesema watacheza kufa na kupona kupata ushindi mzuri utakaosindikiza furaha za mwisho wa wiki.

Wakizungumza mara baada ya mazoezi yao jana walisema: "Haipo nafasi ya kubweteka, huu ni wakati wetu wa kucheza kufa na kupona kuhakikisha tunashinda mchezo tena kwa mabao mengi. Heshima ni kucheza fainali," walisema.

"Tumejipanga vizuri lengo hasa ni kuhakikisha tunafika mbali, tumeanza vizuri na ni imani yetu tutaendelea kupata ushirikiano toka kwa mashabiki na wadau wa michezo," alisema Kelvin Yondan kwa niaba ya wenzake.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

MONGELLA AKABIDHIWA ‘MIKOBA’ RASMI YA NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA*

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI