MAWAZIRI WOTE WAITWA DODOMA

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete (PICHANI) kutangaza Baraza jipya la Mawaziri, mawaziri wote wameitwa mjini Dodoma, huku taarifa zikisema pamoja na mambo mengine, wanatarajiwa kujadili Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13.

Tangu Rais alipotangaza Baraza hilo Mei 4, mwaka huu timu hiyo nzima haijawahi kukutana na hicho ni kikao cha kwanza kwa mawaziri wote chini ya uenyekiti wa mkuu huyo wa nchi.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amethibitisha kuwepo kwa kikao hicho akisema ni cha kwanza tangu kuteuliwa kwao.

“Ni kikao cha kawaida cha Baraza la Mawaziri. Ndiyo ni cha kwanza kwani tangu kuteuliwa kwa mawaziri hakuna kikao ambacho kimewahi kufanyika. Ni cha kawaida tu katika utendaji kazi wa baraza,” alisema Balozi Sefue.

Habari zaidi zinasema kuwa karibu mawaziri wote waliondoka jana kuelekea Dodoma kwa ajili ya kikao hicho ambacho kinafanyika kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti mnamo Juni 12, mwaka huu.

“Wapo ambao wanaweza wakawa Dar es Salaam au nje kwa kazi maalumu. Hawa wanaweza kupata kibali cha Waziri Mkuu. Lakini, karibu mawaziri wote waliondoka jana kuelekea Dodoma,” kilidokeza chanzo kingine.

Hoja ya Bajeti
Kikao hicho kinatarajiwa kujadili bajeti hiyo ya mwaka 2012 ambayo pamoja na mambo mengine, inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo namna ya kupunguza mfumuko wa bei.

Ingawa takwimu za mwezi huu kuhusu mfumuko wa bei zilizotolewa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonyesha kupungua kwa mfumuko huo kutoka asilimia 19 hadi 18.7, bado Watanzania wengi wamekuwa wakilalamikia ukali wa maisha.

Mfumuko huo ambao unagusa bidhaa muhimu kama sukari, pia unagusa nishati ya mafuta ikiwemo petroli na mafuta ya taa, hivyo kuongeza gharama za usafiri kuanzia kwa watu binafsi na abiria wanaotumia usafiri wa umma.

Tayari Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), kimepeleka maombi Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), wakitaka ongezeko la nauli kwa kiwango cha asilimia 150.

Lakini, kwa upande wa wafanyakazi, tayari kumekuwa na shinikizo la kutaka nyongeza ya mishahara kwa kiwango kinachoendana na mfumuko wa bei na ukali wa maisha unaotikisa nchi kwa sasa huku Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), likiwa tayari limetoa angalizo kwa Serikali kutopuuza kilio hicho.

Changamoto nyingine ambayo Baraza hilo la Mawaziri inapaswa kukabiliana nayo katika kujadili Bajeti hiyo kabla ya kuwasilishwa bungeni ni kuhusu namna ya kupunguza gharama za uzalishaji wa chakula, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa urahisi wa pembejeo za kilimo, ili kutekeleza kwa kasi Mpango wa Kilimo Kwanza.
Pia, Baraza hilo Mawaziri linapaswa kupitia kwa kina  vyanzo vipya vya mapato ya kodi ambavyo havitajikita katika vyanzo vilivyozoeleka ambavyo ni pamoja na kodi katika mishahara ya wafanyakazi huku baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wakikwepa kodi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*