MOKIWA AMTAKA RAIS SHEIN KUCHUKUA HATUA HARAKA KUDHIBITI VITENDO VYA UCHOMAJI MAKANISA ZANZIBAR

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa akimweleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud (kulia) maazimio ya viongozi wa dini wa madhehebu ya kikristo juu ya hali ya vurugu, kuchomwa moto na kuvunjwa kwa makanisa visiwani humo. Viongozi hao walipeleka msimamo huo katika Ofisi ya Waziri Abood mjini Unguja, jana. Kushoto ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Ernest Kadiva. Picha na Edwin Mjwahuzi

JOPO la maaskofu limeitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inayoongozwa na Dk Ali Mohamed Shein kuchukua hatua thabiti kudhibiti vitendo vya uchomaji moto makanisa.  Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk Valentino Mokiwa akizungumza kwa niaba ya maaskofu wengine wa madhehebu mbalimbali mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema:

“Tunaiomba Serikali ichukue hatua madhubuti kudhibiti vitendo hivyo, Wakristo wamechoka. Leo tukirejea historia tangu mwaka 2001 kuna makanisa 25 yameshaharibiwa, yaani kuwa Mkristo ni maisha ya hofu.” Askofu Mokiwa alisema kuwa, Wakristo visiwani Zanzibar wanaishi kwa hofu ya kutishiwa maisha kwa kupigwa mawe na wanaonekana kama daraja la pili, lakini Serikali haichukui hatua madhubuti. “Matukio yote hayo yameripotiwa polisi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Tumesikia mkisema (Serikali) eti wanaofanya hivyo ni wahuni. Sisi tunasema hiyo ni lugha ya kututia ganzi.

Wale siyo wahuni ni wahalifu na kuna taratibu za kuwachukulia hatua za kisheria. Serikali inakemea lakini haina 'confidence' (haijiamini),” alisema Askofu Mokiwa. Aliitaka pia Serikali kueleza mikakati inayochukua na kuwataja majina wahalifu waliokamatwa ili waamini kama kweli hatua zimechukuliwa. Alisema Serikali pia inapaswa kuchukua hatua kwa vikundi vya dini vinavyohubiri siasa kinyume na masharti waliopewa. “Siyo dhambi watu kutaka nchi yao au Serikali yao, lakini masuala haya (ya kuchomewa makanisa) hayana uhusiano wowote na Muungano. Basi kuwe na majadiliano na vikundi hivi ili kuleta maridhiano. Akijibu malalamiko hayo, Waziri Aboud alisema atayafikisha yote kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete bila kupunguza hata nukta.

Alikiri Serikali kuzembea katika matukio hayo, lakini akasisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutoeneza lugha za chuki. “Lazima tuwe na mkakati wa pamoja na kuhakikisha tunapambana na wote wanaoeneza chuki.

Uvumilivu wenu mliouonyesha ni mkubwa hivyo tunaomba muendelee. Hao wanaofanya hayo tutahakikisha tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria.” alisema. Akizungumzia uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu visiwani humo, Waziri Aboud alisema tangu kanisa la kwanza lilipoanzishwa visiwani humo mwaka 1870, wamekuwa wakiishi kwa kushirikiana bila kubaguana hadi siku za hivi karibuni.

Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu ukimya wa Rais Shein tangu machafuko hayo yatokee, Waziri Aboud alihamaki akisema ameshatoa matamko mengi kwa nyakati tofauti. “Rais ameshazungumza kwa nyakati tofauti, akiwa hapa na huko Pemba... Ameshazungumza sana, lakini ninyi hamwandiki tu. Hata sasa amenituma nizungumze, sisi ndiyo tunaomwakilisha. Lakini ameshazungumza mno.”

Uamsho yakana Mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho), Sheikh Farid Hadi Ahmed amesema hawahusiki na vitendo vya kuchoma na kuharibu makanisa na kuwalaani watu wanaounganisha kundi hilo na tuhuma hizo. Akizungumza katika Msikiti wa Mbuyuni uliopo eneo la Darajani mjini hapa, Sheikh Ahmed alisema kuwa kundi hilo linafuata taratibu katika harakati zake hivyo halipaswi kulaumiwa kwa vurugu. “Lakini tuna wasiwasi na hawa wanaolipua makanisa na sisi tunawalaani vibaya, hawa tunaamini ndiyo walewale waliokuwa wakisimama na kutukana matusi, tena wana visu, wana nondo, wana pesa...” alisema Sheikh Ahmed.

Sheikh wa msikiti huo, Mussa Juma wataendelea kuandamana kwa amani kudai Zanzibar yao. Sheikh Juma aliyekuwa amekamatwa na polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana aliwapongeza wananchi waliojitokeza katika maandamano. Alidai kuwa kuandamana si kosa kisheria... “Kwani mtu akitembea kwenye nchi yake anatembea kwa kibali? Sisi tumeamua kutembea… Mwenyezi Mungu kajalia tumetembea kwa furaha yote. Timu zinapofanya mazoezi zinachukua vibali? Watu wanakwenda hitimani wanapewa vibali?”  

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.