Ubao ulivyokuwa unasomeka baada ya Yanga kupigwa na Simba mabao 5 kwa nunge katika Ligi Kuu ya Vodacom, kwenye Uwanja wa Tgaifa, Dar es Salaam leo.
Waziri Mteule wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mkangala (kushoto), akimkabidhi kombe la ubingwa wa Tanzania Bara baada ya mechi na Yanga kumalizika leo kwenye Uwanja wa Tgaifa, Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA KAMANDA MWAIKENDA)
Simba wakishangilia ubingwa kiaina
Wapenzi wa Simba wakishangilia ushindi wa mabao matano dhidi ya Yanga pamoja na ubingwa
Ni furaha kwa Simba kila mahala
Wachezaji wa Simba wakishagilia ubingwa baada ya kukabidhiwa kombe na Waziri Mteule wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenela Mkangala |
Wachezaji wakifurahia kombe |
Kocha wa Simba Milovan Circovic akiwa amebebwa na wachezaji |
Wachezaji na viongozi wa Simba wakicheza mduara baada ya kuifunga Yanga mabao matano na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara |
Ni furaha kwa Simba kila mahala
WEKUNDU
wa Msimbazi, Simba SC jioni hii wamekabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe nzito, kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
Hiki ni kipigo cha pili kihistoria Simba wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
Ilikuwa
ni hoi hoi, nderemo na vifijo kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala
na shangwe za Simba.
Hadi
mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na
mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya
kwanza tu ya mchezo huo.
Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
Katika
kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga,
Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye aliishia kumkwatua mara kwa
mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha kupumzikia akiwa ana
kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
Pamoja
na kufungwa bao hilo, Yanga waliendelea kucheza kwa utulivu,
wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa, ingawa kikwazo
kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
Nafasi
pekee nzuri katika kipindi hicho na ambayo Yanga wataijutia waliipata
dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka
vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye na kipa, hesabu zake
ziliendana na Kaseja.
Kiiza aliupelekea mpira upande wa kushoto wa kipa huyo bora Tanzania, ambaye naye akachupa upande huo huo na kuokoa.
Kipindi
cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na
kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati Simba walimpumzisha Mwinyi
Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
Bao
la pili la Simba lilitokana na penalti, baada ya Nsajigwa Shadrack
kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu akaenda kufunga kwa
penalti.
Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 52, baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina.
Dakika ya 66 Uhuru Suleiman aliangushwa na Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti.
Patrick Mafisango alifunga bao la tano kwa penalti pia dakika ya 73.
Simba
SC: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe,
Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi
Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi
‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Yanga:
Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua,
Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’,
Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth Asamoah, Rashid
Gumbo na Hamisi Kiiza.
Comments