MWANDOSYA ALITIKISA BUNGE

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya (kushoto), jana alikuwa kivutio kikubwa bungeni na kuwafanya wabunge wamshangilie kwa muda mrefu wakati akitambulishwa.

Mwandosya ambaye alikuwa Waziri wa Maji kabla ya mabadiliko yaliyofanyika miezi mitatu iliyopita alishindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa mwaka mmoja, kwa sababu ya matatizo ya kiafya.

Waziri Mwandosya aliingia bungeni jana asubuhi muda mfupi baada ya kumalizika kwa maswali na majibu, hivyo kuwafanya wabunge kulipuka kwa makofi na vigelegele.

Shangwe hizo zilimduwaza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa ameitwa na Mwenyekiti wa Bunge kuwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake.

Mwenyekiti, Jenista Mhagama, alimuona Waziri Mwandosya akiketi na hivyo kumwomba Dk. Mwakyembe, angoje kidogo ili aliarifu Bunge juu ya uwepo wa kiongozi huyo.

“Waheshimiwa wabunge natambua uwepo wa Waziri Mwandosya, kwa kweli Mwenyezi Mungu ni mkubwa, mwingi wa rehema sana na ana mipango yake, hivyo tunakukaribisha uendelee na majukumu yako,” alisema Mhagama.

Baada ya utambulisho huo, Kaimu Waziri Mkuu, Samuel Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alitoa hoja na kuungwa mkono, akitaka Mwandosya apewe muda wa dakika tano aseme neno kidogo.

Katika hotuba yake fupi, Waziri Mwandosya alianza kwa kumshukuru Mungu akisema hakutegemea kama afya yake ingeimarika kwa kiwango alichonacho hivi sasa, lakini imetokea na kwamba ameuona mkono wa Mungu katika uponaji wake.

“Ni zaidi ya mwaka tangu nimekwenda kwenye matibabu na sijazungumza katika Bunge lako tukufu na moja ya mambo niliyokuwa nikimwomba Mungu, anirudishie walau dakika tano kuja kuongea na wabunge wenzangu na Mungu ameridhia ombi langu,” alisema.

Aliwashukuru Watanzania wote kwa kumwombea akisema ukiugua hakuna chama, kwani alipokea salamu za kumtakia nafuu kutoka kwa vyama vyote vya siasa.

“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete, alinisisitiza sana kuwa afya ni jambo la mhimu sana, kwa hiyo akaniambia ondoka nenda ukatibiwe wala usije ukafikiria wapi hakuna maji…kumbe ilikuwa kweli, maana si tena waziri wa maji…hivyo ningeendelea ningekuwa nawaza mheshimiwa Zitto ataniuliza maji Kigoma,” alisema.

Pia aliwashukuru Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein na makamu wote wawili wa serikali hiyo lakini akasema zaidi ni kwa Maalim Seif Sharrif Hamad na viongozi wengine wote ambao ni sehemu ya kupona kwake.

“Nawashukuru sana waheshimiwa wabunge na zaidi mmekuwa sehemu ya kupona kwangu…wote bila kujali vyama vyetu…nimeamini kuwa vyama ni nguo tu, kwani wakati mwingine nimepokea salamu zaidi kutoka upinzani,” alisema.

Waziri Mwandosya ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatizwa kwa makofi ya wabunge, aliongeza kuwa moja na la msingi ambalo amejifunza ni kwamba sasa amejua kwamba Wizara ya Afya ni mhimu sana.

“Afya ni mhimu sana, hasa baada ya kuugua…sijui kilimo ndiyo namba moja au elimu, lakini ukiugua kilimo wala elimu huwezi, hata hapa bungeni huwezi kuomba mwongozo wa Spika, kwa hiyo afya kwanza,” alisema.

Aliwashauri wabunge kuendelea kupima afya zao, akisema kuwa kwa miaka 45 alikuwa hajawahi kulazwa hospitalini, lakini amekiona kitanda huko Hadrabad nchini India alipokwenda kutibiwa, maana awali alijiona ni mtu mwenye afya na mazoezi sana.

“ Sasa naomba pia tuangalie afya zetu hata baada ya kustaafu, maana tunajisikia tuko wazima tunapozungumza sana, lakini baada ya kumaliza je, tumeingia mkondo gani wa afya? Katika taratibu za afya nchini ni jambo la muhimu,” alihitimisha Waziri Mwandosya.

Baada ya kuhitimisha, Mhagama alimpa nafasi Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Kabwe Zitto, ambaye alimkaribisha waziri huyo na kumtakia kazi njema.

Naye Waziri Mwakyembe alipoitwa kusoma hotuba yake, alitumia muda mfupi kumtakia waziri mwenzake kazi njema, akisema kwamba amefarijika kumwona kaka yake huyo bungeni tena na kuwa mwache Mungu aitwe Mungu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.