Na Ali Issa na Zahira Bilali-Maelezo Zanzibar 24/01/2013
Jumla
ya Wanafunzi 11,195 wamechaguliwa kujiungia Kidatu cha Tatu kwa mwaka
wa masomo 2013 katika Skuli mbalimbali za Unguja na Pemba ambapo kati
yao wasichana ni 6,768 na wavulana ni 4,427.
Aidha Wanafunzi 17,511 wamefaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu ambapo kati yao Wasichana ni 9,652 na Wavulana 7,859 .
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma Shamhuna amebainisha
hayo leo wakati alipokuwa akitoa tathimini ya matokeo ya mitihani hiyo
huko ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Amesema
kuwa Wanafunzi waliofanya mtihani wa kuingilia Kidato cha Tatu walikuwa
19,679 ambapo kati yao Wasichana walikuwa 11,045 na wavulana 8644 sawa
na asilimia 93.6 %.
Aidha ameongeza kuwa ufaulu wa kidato cha Tatu umeongezeka kwa asilimia 0.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kwa
upande wa Mtihani wa Darasa la Saba Waziri Shamhuna amesema jumla ya
Wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 23,039 kati yao wasichana
walikuwa 12,236 na wavulana 10,803.
Akielezea
Skuli zilizoshika nafasi ya juu kwa matokeo ya Darasa la Saba Waziri
Shamhuna amesema ni pamoja na Kizimbani iliyopo Wilaya ya Wete Pemba na
Skuli za Wazazi na Mkunazini zote za Wilaya ya Mjini Unguja.
Aidha amezitaja Skuli zilizofanya vibaya matokeo ya Darasa la Saba kuwa ni Kojani, Ukunjwi na Makoongwe zote za Kisiwani Pemba.
Kwa
upande wa Matokeo ya Kidato cha Pili skuli zilizofanya vyema kuliko
nyingine ni Mtoni iliyopo Wilaya ya Magharibi Unguja na Skuli za Msuka
na Kiuyu zote za Wilaya ya Micheweni Pemba.
Akielezea
Skuli zilizofanya vibaya mtihani wa Kidato cha Pili Waziri Shamhuna
amesema ni Skuli za Mwenge iliyopo Wilaya ya Magharibi na Skuli za Mfuru
matonga na Kinyasini zote za Kaskazini A Unguja.
Waziri
Shamhuna amezitaja pia Skuli ambazo zitalazimika kufungwa kutokana na
kupasisha idadi ndogo ya Wanafunzi ambazo ni Bwefum, Umbuji, Uzi,
Ubago,Pongwe Pwani, Michanvi,Mtende,Kisiwa Panza,Makongwe na Ndagoni.
Ameongeza
kuwa jumla ya Kesi za udanganyifu 12 ziliripotiwa kwa wanafunzi wa
Kidato cha pili ambapo Wizara imeamua kwafutia matokeo wanafunzi
waliohusika na Udanganyifu huo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 24/01/2013
Comments