Na Mwandishi Wetu
SIYO siri, Julai 7, mwaka huu (Siku ya Sabasaba), anga lote la Jiji la Dar es Salaam litasimama kwa muda wa saa 16. Burudani mfululizo pamoja na matukio ambayo hayajawahi kushuhudiwa, mengine ni adimu sana, yatachukua nafasi pana siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa.
Diamond.
Ni saa 16 za maajabu! Tafakari Mbunge wa Kigoma Mjini (Chadema), Zitto Kabwe, ataonesha uwezo wake wa kucheza masumbwi na kuchapana na staa wa filamu Tanzania, Vincent Kigosi ‘Ray’. Je, ni vigumu kuamini?
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, atakuwa na kibarua chake katika mchezo wa ndondi, atakapopanda ulingoni kuzipiga na malkia wa Bongo Movie, Jacqueline Wolper. Uheshimiwa na usupastaa kando, zitapigwa ngumi tu kwa raundi nne.
Prezzo.
Vilevile, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Mara, Ester Bulaya, siku hiyo atakuwa na kazi moja tu ya kukong’otana na mrembo nyota wa sanaa za maigizo nchini, Aunt Ezekiel. Ni burudani ambazo awali hazikuwahi kufikiriwa kwamba zingewezekana lakini ndani ya Usiku wa Matumaini, imewezekana.
Kila mmoja anatamba kivyake kumchapa mpinzani wake lakini mwisho wa ubishi ni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwenye Usiku wa Matumaini, Dar es Salaam.
JB.
JB YEYE ANAMTAKA AZZAN
Kuonesha kwamba homa ya Tamasha la Usiku wa Matumaini imepanda juu sana, staa mkubwa wa filamu Tanzania, Jacob Steven ‘JB’, amemtaka Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, wakutane Uwanja wa Taifa, amuoneshe kazi.“Idd Azzan asiogope, namtaka aje tukutane ulingoni. Ila kiukweli ndani ya sekunde 35, itakuwa nimeshampiga na atakuwa ameshalala,” alisema JB na kuongeza:
“Nakuomba Azzan, njoo nikuoneshe mchezo. Inawezekana uzito wa ngumi zangu hujaujua, kwa hiyo lengo langu ni kukuchapa makonde mazito halafu baada ya hapo, nitaanza kufukuzia mapambano ya kimataifa, maana naona hapa nchini sitakuwa na mpinzani.”
Ester Bulaya.
Upande mwingine, JB alisema kuwa anaamini kuwa pambano la Zitto na Ray litakuwa na upinzani mkali kwa sababu wote wana mazoezi ya kutosha.
“Naamini mdogo wangu Ray yupo vizuri ila upinzani utakuwa mkali sana dhidi ya Zitto. Vilevile nawatakia kila la heri Jacqueline Wolper ambaye bila shaka atamchakaza mheshimiwa Halima Mdee na Aunt Ezekiel sina shaka naye kwamba atampiga mheshimiwa Ester Bulaya,” alisema JB.
Wabunge: Simba vs Yanga.
MAAJABU YAAENDELEA
Mechi kali yenye ushindani mkubwa, itakuwa ni Simba na Yanga. Waheshimiwa wabunge wanaoshabikia timu hizo mbili, watachuana wao kwa wao kumtafuta Bingwa wa Kombe la Matumaini mwaka 2013.Mechi kama hiyo, ilipigwa mwaka jana, Uwaja wa Taifa, Dar es Salaam kwenye Tamasha la Usiku wa Matumaini na Simba iliibuka mshindi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
Mambo yatanoga kwa mara nyingine mwaka huu, kuonesha kuwa Yanga wanataka kurejesha heshima yao, wameogeza wachezaji wanaocheza kikosi A.
Mashali.
Mmoja wa viongozi wa timu ya wabunge wanaoshabikia Yanga, Abbas Mtemvu, amesema kuwa wameamua kuongeza wachezaji wanne kutoka kwenye kikosi A cha Yanga ili kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Tumewaogeza Mrisho Ngassa, Ally Mustapha ‘Barthez’, Kelvin Yondan na Athuman Idd ‘Chuji’. Watacheza kuhakikisha Yanga inashinda. Hatuna utani katika mechi, sisi tunakweda kulinda heshima,” alisema Mtemvu.Upande mwigine, nahodha wa timu ya wabunge wa Simba, Amos Makalla, amesema kuwa ameshajua hila ya Yanga, kwa hiyo nao wanajipanga kuongeza wachezaji wengine kutoka Simba A ili kuhakikisha Yanga hawatoki siku hiyo taifa.
“Mpaka sasa tumeshawaongeza Shomari Kapombe na Amri Kiemba, tunatarajia kuongeza wengine baada ya kocha wetu kutoa mwongozo. Siku hiyo watake wasitake, tutawapiga tu Yanga, hawana ujanja. Mwaka huu tunawatengeneza ndani ya dakika 90,” alisema Makalla.
MAKONGO VS JITEGEMEE
Katika tamasha hilo, kivutio kingine ni mechi ya soka kati ya timu za kombaini ya Makongo Sekondari na Jitegemee.Inaeleweka kuwa Jitegemee na Makongo ni shule zenye upinzani wa jadi kimichezo, kwa hiyo siku hiyo bingwa atajulikana na kukabidhiwa kikombe.
BONGO MOVIE VS BONGO FLEVA
Hii ni mechi inayokutanisha mastaa watupu. Wale wa filamu, Bongo Movie FC, wataoneshana umwamba kwa dakika 90 na wakali wa muziki, Bongo Fleva FC. Mwaka jana katika Tamasha la Usiku wa Matumaini, mechi hii ilifanyika na Bongo Movie walishinda bao 1-0, kwa hiyo mwaka huu Bongo Fleva wanataka kurejesha heshima yao.
Bongo Fleva vs Bongo Movie.
Nahodha wa Bongo Fleva FC, Hamis Ramadhan ‘H. Baba’, amesema kuwa wao kama timu, wanajua mbinu ambazo Bongo Movie walizitumia kushinda mwaka jana, kwa hiyo mwaka huu wasitegemee mazingira yaleyale.
“Tutawafunga kwa urahisi sana mwaka huu. Hatutaki kurejea makosa ya mwaka jana. Hili naomba hao Bongo Movie walijue. Mimi binafsi lazima niwafunge, nina usongo nao sana wale jamaa,” alisema H. Baba.Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie, Vincent Kigosi ‘Ray’, alisema kwamba hana shaka na timu yake, kwani watashinda kama ilivyokuwa mwaka jana.
“Lile kombe ni letu, Bongo Fleva wataendelea kuwa wateja wetu tu. Tunaendelea kufanya mazoezi makali, tupo vizuri sana. Bongo Fleva wasubiri kichapo kingine. Tunatarajia mwaka huu tutawafunga zaidi ya mabao mawili,” alisema Ray.
Kiongozi wa Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf.
MUZIKI
Siku haitakamilika bila burudani ya muziki, Nasibu Abdul ‘Diamond’ wa Tanzania na Rapa Jackson Makini ‘Prezzo’, watabadilishana mic, kuoneshana ni nani mkali zaidi ukanda wa Afrika Mashariki.Bendi hasimu na kongwe zaidi, Msondo na Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, watapishana kwenye jukwaa moja kisha mashabiki wataamua nani mkali kuliko wengine.
Mfalme wa Taarab, Mzee Yusuf akiwa na kundi zima la Jahazi Modern Taarab, watafanya muziki mzuri siku hiyo na kukamilisha shangwe za wapenda mambo ya Pwani hususan muziki wa mwambao.
Mwanza Suspastaa, Hamis Ramadha ‘H. Baba’, atakuwa na timu yake ya shoo, yote ni kuhakikisha kwamba anafanya muziki utakaoacha historia kubwa siku hiyo.
Kundi la TMK Wanaume Family linaloongozwa na mastaa, Amani James Temba ‘Mheshimiwa Temba’ na Saidi Juma ‘Chegge’, litakuwepo na lile la TMK Wanaume Halisi ambalo kinara wake ni Juma Kassim Kiroboto ‘Sir Nature’.
Flora Mbasha.
INJILI
Muziki wa Injili, utakutanisha mchuano wa nguvu kwa wanamuziki wa Tanzania kuchuana na wale wa Kenya. Kenya itaongozwa na Anastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa, Sara K na 24 Elders ambao wameahidi kutoa ushindani mkubwa kwa Watanzania.Kwa upande wa Tanzania, watakuwepo waimbaji mahiri kama Upendo Nkone, Flora Mbasha, Martha Mwaipaja, Edson Masabwite, Ambwene Mwasongwe, Glorious Worship Team, Enock Jackson, Kundi la The Voice, Jesca na Kundi la The Voice.
Viingilio vya tamasha hilo ambalo litasheheni matukio kibao ya kus
isimua kwa lengo la kuchangia Mfuko wa Mamlaka ya Elimu nchini (TEA), vitakuwa ni shilingi 20,000 kwa V.I.P, 10,000 viti vya bluu na 5,000 viti vya kawaida.(kwa hisani ya FullshangweBlog)
Comments