Mwigamba: Najiweka pembeni Chadema

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba
Mwenyekiti  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amesema ameamua kujiweka pembeni kuepusha malumbano kati yake na chama kufuatia uamuzi usio halali wa kusimamishwa uongozi uliofanywa na kikao cha Baraza la Uongozi la Kanda.

Alisema atakuwa pembeni mpaka hapo Kamati Kuu itakapojadili na kutoa uamuzi dhidi yake.

Akizungumza na  waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwigamba aliwasihi wanachama, viongozi, na wananchi wote nchi nzima kutambua kwamba yeye ni mwanachama na Mtanzania safi anayeipenda nchi yake na chama chake na anayeamini kwamha hakuna chama kingine kilichobeba matumaini ya Watanzania katika kuleta mabadiliko na kuluikwamua taifa kutoka lindi la umaskini.

“Naendelea kuwasisitiza wakiamini chama hiki…ninachotaka mimi ni kukiandaa chama hiki ili kitakapoingia madarakani kiwe ni chama makini kitakacholeta mabadiliko tunayoyatarajia na si kuwa kibovu kuliko hata kilichoko madarakani kwa sasa,” alisema na kuongeza:

“Ikitokea hivyo, nitakuwa wa kwanza kuumia sana pamoja na idadi kubwa ya watu waliokiamini na kukitumaini sana.”

Alisema anatambua kikao kinachoitwa Baraza la  Uongozi la Kanda kuwa ni kikao cha mashauriano na si cha maamuzi na kimsingi si cha kikatiba.

“Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, Ibara ya 6, mamlaka yangu ya nidhamu ni Kamati Kuu. Na kuna utaratibu wa kikatiba wa kumchukulia kiongozi na hata mwanachama wa kawaida hatua za kinidhamu.

“Lakini kwa kuwa kile kikao ambacho hakikuwa na uhalali wa kunichukuliwa hatua yoyote ya kinidhamu, kilihudhuriwa na mwenyekiti wa taifa, na ili kuepusha malumbano, nimeamua kujiweka pembeni mpaka hapo Kamati Kuu itakapojadili na kutoa uamuzi dhidi yangu,” alisema.

ALIYOANDIKA KWENYE MTANDAO
Akizungumzia kuhusu alichoandika kwenye mtandao wa Jamii Forums, ambayo ndiyo yanadaiwa kuleta sakata la yeye kusimamishwa uenyekiti, Mwigamba alisema:
“Kwanza kabisa nasema bila kumung’unya maneno kwamba nilimaanisha nilichokiandika na nilikuwa sibahatishi.

“Ni vema sote tukaelewa kwamba katiba ya Chadema inakataza viongozi kutoa hadharani na kuzungumza mambo ya chama badala yake watumie vikao.
Ndio maana inapotokea kiongozi ana maoni yanayohusiana na mambo ya ndani anayotaka wanachama wenzake wayapate na bila kuyahusisha na cheo chake, huchagua njia yo yote ambayo ataona inafaa ikiwa ni pamoja na kuficha jina lake.

“Napenda niwahakikishie kwamba kuna viongozi wengi sana ndani ya Chadema ambao wanazo ID zisizojulikana kwenye mitandao na huzitumia kuzungumza na wanachama mambo mengi ambayo hawataki yahusishwe na vyeo vyao bali yabaki kama maoni ya mwanachama binafsi. Na ndicho nilichokifanya.”

Alisema kama angetoa kwenye vyombo vya habari na kujitambulisha kama Samson Mwigamba, Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha na kuanza kuzungumza yale aliyozungumza, walikuwa na haki ya kunishtaki kwenye mamlaka yake ya nidhamu.

 “Nikiwa pale makao makuu ndipo nilianza kujua madhaifu makubwa ya kiuongozi kwenye chama changu. Hata kuondoka kwangu makao makuu niliondolewa kwa mizengwe.

Kiongozi mkubwa kabisa alinifukuza kazi kwa agizo la simu ambapo alimpigia simu Mkurugenzi wa Fedha tena akiwa nje ya Dar es Salaam na kumwagiza kwamba, ‘nikirudi nisimkute Mwigamba ofisini,” alisema.

Hata hivyo, alisema pamoja na yote hayo yaliyojiri, hajawahi kujitokeza mahali popote iwe kwenye vyombo vya habari ama kwenye mitandao, kuzungumzia matatizo makubwa ya viongozi na uongozi ndani ya chama ambayo wanachama wa kawaida wanaokiamini chama na viongozi wake wangesikia wangeweza kukata tamaa.

“Nilifanya hivyo kwa mapenzi mema na kwa maslahi ya chama changu,” alisema.

Akizungumzia sakata la kuchokonoa mtandao wake, alisema hakuna mtu ye yote  awe ni mtaalamu wa IT ama vyovyote vile bila kujali uanachama wake ama uongozi wake, mwenye haki ya kwenda kwenye mtandao na kuanza kuchokonoa mpaka apate IP address atafute kujua hicho kilichoandikwa kimetoka kwenye kompyuta gani na nani katuma.

Hata hivyo, alisema kuwa alichokiandika ni kuwaeleza wananchama kwamba uongozi wa sasa umekaa madarakani kwa muda mwafaka hivyo uwaachie wengine wakiongoze chama.
CHANZO: NIPASHE

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI

π—₯π—”π—§π—œπ—•π—” 𝗬𝗔 π—¬π—”π—‘π—šπ—” 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—™π—¨π—‘π—šπ—” 𝗠π—ͺπ—”π—žπ—” 2024 πŸ”°

MONGELLA AWATEMBELEA HOSPITALI WALIOMWAGIWA TINDIKALI

GERSON MSIGWA AREJESHWA KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

AUCHO, BACCA, BOKA WAJUMUISHWA KWENDA ALGERIA LEO