SIRI NZITO YA KUTIMULIWA MAWAZIRI YAFICHUKA..MADUDU WALIO KUWA WAKIFANYA NI AIBU TUPU

SIRI mbalimbali zimeanza kufichuka kuhusiana na ‘madudu’ yaliyokuwa yakifanyika, katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, iliyowang’oa madarakani mawaziri wanne. 

Siri hizo zimeanza kuvuja baada ya kubainika kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliandikiwa barua mara mbili na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi juu ya ‘madudu’ hayo, lakini hakuweza kuchukua hatua.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA Jumamosi limezipata zilisema kutokana na Pinda kushindwa kuchukua hatua, kulisababisha Dk. Nchimbi kugoma kujiuzulu pale alipotakiwa kufanya hivyo.
Chanzo chetu cha habari kilisema kuwa Nchimbi aligoma katika kikao kilichoitishwa na Pinda, wakati akizungumza na mawaziri wanne waliotajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, akiwashawishi waachie ngazi.
Chanzo chetu kilieleza kuwa katika kikao hicho, Dk. Nchimbi alimkumbusha Pinda namna alivyokuwa akimpatia taarifa juu ya malalamiko ya wananchi, lakini alijibiwa kuwa hiyo ni kazi maalumu ya Serikali.
Mbali na Dk. Nchimbi, mawaziri wengine walioitwa na Pinda ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo.
“Katika kikao kile, Dk. Nchimbi alimkumbusha waziri mkuu juu ya barua mbili alizomwandikia, akimlalamikia jinsi operesheni ilivyoendeshwa. Katika barua hizo, alimweleza mbona watuhumiwa wanaokamatwa hawapelekwi katika mahabusu za polisi na badala yake wanafungwa katika nguzo za umeme?
“Hakuishia hapo, Nchimbi akamweleza tena waziri mkuu kwamba, wakuu wa mikoa na wilaya nao wanalalamika kwamba mikoa yao imevamiwa, watu wanateswa, hiyo Task Force inaingia bila kamati za ulinzi na usalama za mikoa yao kuwa na taarifa?
“Waziri mkuu alimjibu akisema kuwa ile ilikuwa ni Task Force (kikosi kazi) na kwa msingi huo, Dk. Nchimbi aligoma katakata kuwajibika,” kilisema chanzo chetu cha habari.
MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta, Dk. Nchimbi kupitia simu yake ya kiganjani lakini simu hiyo ilikuwa ikiita bila kupokewa na baadaye ilizimwa.
Mawaziri wote waliong’olewa kwa nyakati tofauti wameelezea hatua hiyo na wengi wakionesha wazi ni kama vile wameonewa.
Dk. Nchimbi aliweka wazi kile kilicho moyoni mwake kupitia mtandao wa Facebook, akielezea alivyoguswa na namna atakavyoendelea kuwa na upendo kwa wanadamu wenzake.
Balozi Kagasheki yeye alipata wasaa wa kuzungumza muda mfupi kabla ya Waziri Mkuu kutangaza bungeni uamuzi wa Rais Kikwete, akikubali kuwajibika kutokana na kilichojiri katika ripoti iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, James Lembeli.
Dk. Mathayo naye alipata fursa kama ya Kagasheki kuzungumza bungeni akisema tuhuma zilizomo kwenye taarifa ya Operesheni Tokomeza hazijamgusa.
Nahodha naye alihusisha kilichomtokea kuwa ni sawa na mitihani inayompata mwanadamu duniani na hivyo anapaswa kukabiliana nayo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini, Isaya Mungulu amesema ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iko upande mmoja kwa kutoangalia pande mbili zilizoathirika na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi ofisini kwake jana, Mungulu alisema hata wabunge waliochangia mjadala wa ripoti ya Kamati ya Lembeli, nao waliangalia upande mmoja wa waathirika.
“Katika operesheni ile askari polisi mmoja aliuawa, lakini wabunge hawakuona huo umuhimu wa kuwazungumzia, lakini inategemea na hadidu za rejea walizopewa,” alisema Mungulu.
Hata hivyo, Mungulu alisema Operesheni Tokomeza iko kwa maandishi na haikuagiza askari wakaue wananchi.
Naye, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alizungumza na MTANZANIA Jumamosi alikiri ripoti ya Lembeli kuonyesha upungufu kwa kutoeleza bayana namna majangili walivyoua askari waliokuwa wakipambana na ujangili.
Lugola alisema katika operesheni hiyo, ndugu yake wa kike ambaye ni askari alikufa baada ya kupigwa risasi na majangili na kufa papo hapo.
“Ripoti ingeenda ndani zaidi tuone namna askari walivyokuwa wakikabiliana na mazingira magumu wakati wakipambana na majangili na wengine waliofariki.
“Lakini hii hoja ya watu kuteswa ni ya muda mrefu na haya yaliyotokea imekuwa sawa na moshi tu uliowekwa kwenye mzinga wa nyuki,” alisema Lugola.

Chanzo: Mtanzania

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI

π—₯π—”π—§π—œπ—•π—” 𝗬𝗔 π—¬π—”π—‘π—šπ—” 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—™π—¨π—‘π—šπ—” 𝗠π—ͺπ—”π—žπ—” 2024 πŸ”°

MONGELLA AWATEMBELEA HOSPITALI WALIOMWAGIWA TINDIKALI

GERSON MSIGWA AREJESHWA KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

AUCHO, BACCA, BOKA WAJUMUISHWA KWENDA ALGERIA LEO