SIMBA SC YAWAONYA YANGA KWA KUANZA UJENZI WA UWANJA BUNJU, ZANA ZATUA RASMI!

Hivi ndivyo mambo
yalivyo huko Bunju. Picha hii ni kwa hisani ya Blog ya Bin
Zubeiry.
Na Baraka Mpenja, Dar es
salaam
WAKATI mchakato wa
uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu ukizidi
kushika kasi hasa baada ya mgombea aliyeenguliwa kuwania Urais Michael Richard
Wambura kurejeshwa, taarifa njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kwamba mkakati
wa ujenzi wa uwanja umechukua sura mpya leo hii.
Mtandao huu unafanya
jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba ili kujua zoezi hilo linaendeleaje huko
Bunju.
Hata hivyo, Msemaji wa
Simba sc, Asha Muhaji ameuambia mtandao huu kuwa hajapewa taarifa rasmi na
uongozi kuhusu zoezi hilo.
Muhaji amesema
linapotokea jambo katika klabu hiyo anapewa taarifa, hivyo ameahidi kufikia
baadaye atakuwa na taarifa zaidi.
“Mimi bado sijapewa
taarifa kamili, labda tuwasiliane baadaye ili tujue”. Amesema
Muhaji.
Uongozi wa Simba
amepeleka magari yanayomwaga vifaa na kusafisha eneo la uwanja wao uliopo Bunju
jijini Dar es salaam.
Awali suala hili
lilichukuliwa kwa utani na kuwabatiza viongozi na wanachama wa Simba jina la
utani la`wazee wa kilimo kwanza` , lakini mambo yamebadilika baada ya viongozi
kuonekana wamekusudia kujenga uwanja wa kisasa wa klabu
hiyo.
Jina hilo lilitokana na
katibu mkuu wa Simba kutangaza kuwa wanachama wachukue majembe, makwanja,nyengo
ili wakafyeke na kusafisha eneo la uwanja wa Bunju.
Leo hii mambo
yamebadilia na magari yameanza kazi ya kusafisha eneo na kumwaga vifaa kwa ajili
ya kuanza ujenzi.
Suala la uwanja limekuwa
wimbo wa taifa kwa klabu za Simba na Yanga tangu zianzishwe miaka mingi
iliyopita.

Picha hii ni kwa hisani
ya Blog ya Michezo ya Bin Zubeiry. Unaweza kuitembelea kwa picha
zaidi.
Lakini sasa klabu zote
zinaonekana kuwa katika mipango ya ujenzi wa viwanja
vyao.
Yanga chini ya
mwenyekiti aliyeongezewa muda wa mwaka mmoja Yusuf Manji wapo katika mkakati
mzito wa kujenga uwanja wa kisasa maeneo ya jangwani.
Lakini kwa upande wa
Simba, mwenyekiti wake Ismail Aden Rage alileta siasa katika suala la uwanja,
ila sasa inaonekana kuna watu wameamua kulivalia njuga.
Japokuwa kuna watu
wanahoji kwanini suala hili limekuja wakati huu wa uchaguzi?, mpango huo unataka
kutumika kama kampeni kwa wagombea Fulani?
Lakini bado majibu
hayajapatikana kwasababu haijatangazwa kuwa ni mtu fulani anasimamia suala
hilo.
Kujenga uwanja ni muhimu
sana kwa klabu kama Simba, lakini wasiwasi kwa baadhi ya watu unakuja kulingana
na wakati ilionao Simba.
Klabu inaelekea kwenye
uchaguzi wiki mbili zijazo na siku kadhaa, hivyo watu wanaanza kuhusianisha na
kampeni.
Lakini hata kama ni
kampeni, bado ukweli uko pale pale kuwa kiongozi yeyote atakayeingia madarakani
ajitahidi kujenga uwanja.
Endapo Kuna watu
wameamua kuwahadaa wana Simba kwa ujenzi huo, basi ni tatizo na inaweza kuleta
mashaka kama mpango wenyewe utakamilika.
Tusubiri kampeni, kama
kuna mtu ametumia ujenzi huo itajulikana, lakini kwasasa
tuliache.
Comments