Waziri Mkuu, Kassim Majalaiwa akizungumza na Madaktari, Wauguzi na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa Aprili 11, 2016. Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa Lindi, Mzee Mtopa.
Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majalaiwa akizungumza baada ya kukabidhi msaada wa shuka kwa wazazi wanaosubiri kujifungua na waliojifungua kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa Aprili 11, 2016. Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa Lindi, Mzee Mtopa.
Wanawake wa Ruangwa wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakti alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Chama cha Walimu mjini Ruangwa Aprili 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na wanwake wa Ruangwa baada ya kuzungumza nao kwenye ukumbi wa Chama cha Walimu mjini Ruangwa Aprili 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akitembelea soko kuu la mji wa Ruangwa kukagua hali ya chakula na bei zake Aprili 11, 2016. Alikuwa katika ziara ya jimbo lake la uchaguzi la Ruangwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na mabingwa wa soka wa mkoa wa Lindi , timu ya Namungo FC ya Ruangwa baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa huo na kuzungumza nao kwenye uwanja wa michezo wa Ruangwa akiwa katika ziara jimboni kwake , Aprili 11, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………………….
MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua.
Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.
Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati alipotembelea wodi ya akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio wamebeba dhamana ya afya za wananchi.
“Nimefurahi kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia, hongereni sana” amesema.
Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa katika wodi hiyo amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa anakaribia kutoka.
“Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa.
Mbali na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii kwa urahisi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu ikiwemo michezo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa mazoea kwa sababu umepitwa na wakati.
Pia amesema amefurahishwa na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
Comments