4x4

BOCCO ATUA SAUZ KUIONGEZEA NGUVU STARS


STRAIKA mpya wa Simba, John Bocco, ameongezwa katika kikosi cha Taifa Stars kinachotarajiwa kucheza nusu fainali ya Kombe la Cosafa dhidi ya Zambia, leo Jumatano.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, Kocha Mkuu, Salum Shaban Mayanga, amelazimika kumuita Bocco kutoka Tanzania na sasa yupo Afrika Kusini, akichukua nafasi ya Mbaraka Yussuf aliyepata majeraha katika michuano hiyo iliyoanza Juni 25, mwaka huu.
Stars ilikuwa Kundi A pamoja na timu za Malawi, Mauritius na Angola, ikaibuka kinara na kutinga robo fainali ambapo iliwatoa wenyeji Afrika Kusini juzi Jumapili baada ya ushindi wa bao 1-0.
Mayanga alisema amemuongeza Bocco ili pia ajiandae na mchezo dhidi ya Rwanda ambao ni wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan). Mechi hiyo dhidi ya Rwanda itachezwa Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kabla ya kurudiana ndani ya mwezi mmoja.
Kama Stars ikiitoa Rwanda, itakutana na Uganda na mshindi wa jumla wa mechi hizo, atafuzu fainali za Chan zitakazofanyika mwakani nchini Kenya.
Post a Comment