SIMBA, YANGA NI TAASISI ZENYE NGUVU KULIKO CCM, UKAWA


Simba na Yanga ndiyo taasisi zinazoigawa Tanzania mara mbili. Kama haupo Simba, basi wewe ni Yanga, hakuna zaidi ya hapo. U’Simba na U’Yanga umetengeneza upacha kwenye damu ya Watanzania.
Ipo idadi kubwa ya Watanzania ambao si mashabiki wa mpira lakini nao wana upande, ama wapo Simba au Yanga. Klabu za Simba na Yanga kwa tafsiri pana zimekuwa utamaduni wa Mtanzania.
Lipo kundi fulani husema halishabikii Simba wala Yanga lakini zinapocheza hufurahi au kuumia kimyakimya kwa aina ya matokeo ambayo timu iliyo ndani ya mapenzi yao hupata. Naomba niseme kwa msisitizo; Simba na Yanga ni taasisi pacha na maisha ya Watanzania.
Klabu hizo mbili ni taasisi zenye nguvu kuliko nyingine yoyote nchini. Upacha wa Simba na Yanga kwa maisha ya Watanzania haupatikani kokote duniani. Ni rahisi shabiki wa Barcelona kuwa mnazi wa Real Madrid au kinyume chake lakini siyo Shabiki wa Simba kuipenda Yanga au kinyume chake.
Inawezekana mkereketwa wa Inter Milan kuishabikia AC Milan au kinyume chake lakini hali hiyo huwezi kuipata Simba na Yanga. Mechi ya Simba dhidi ya Yanga huwa na msisimko wenye nguvu unaoigawa Tanzania pande mbili. Hali hiyo mguso wake haufanani na mahali popote duniani.
Mguso ambao naujengea hoja ni ule upacha wa Watanzania kwa timu zao mbili, Simba na Yanga. Nafahamu zitaibuka hoja kuhusu mchuano mkali wa wapinzani wa jadi nchini Argentina kati ya Boca Juniors dhidi ya River Plate (Superclasico).
Takwimu za zinaonesha kuwa Boca Juniors na River Plate, zinabeba asilimia 70 ya mashabiki wote wa soka Argentina. Boca ikiwa na asilimia 40, River ikiwa na asilimia 33. Ukija Tanzania utakuta kuwa asilimia 100 ya mashabiki wa soka nchini wapo Simba na Yanga.
Nenda Uturuki wakute Fenerbahce dhidi ya Galatasaray (Intercontinental Derby), fika Scotland uwaone Celtic na Rangers (The Old Firm), ukikanyaga Serbia utawashuhudia Red Star Belgrade na Partizan Belgrade (The Eternal Derby), shusha maguu Uholanzi ukutane na Ajax dhidi ya Feyenoord (De Klassieker), bado vionjo vya Simba na Yanga vipo kipekee sana.
Hazinishtui Liverpool na Manchester United (North-West Derby) England wala Roma na Lazio (Derby della Capitale) Italia. Natambua ukali wa mahasimu wa Ugiriki, Olympiakos dhidi ya Panathinaikos (Derby of the Eternal Adversaries), Brazil kati ya Palmeiras dhidi ya Corinthians (Paulista Derby), ongezea El Clasico (Barcelona na Madrid) pamoja na Derby della Madonnina (Inter na AC Milana), bado nazipa thamani Simba na Yanga.
Simba na Yanga ni zaidi ya soka
Tanzania, Simba na Yanga ni itikadi zenye nguvu mno. Kasi ya waumini wa Kiislam kubadili dini na kuhamia Ukristo au Wakristo kusilimu kuwa Waislam ni kubwa kuliko mashabiki wa Simba na Yanga kuhama upande mmoja kwenda mwingine.
Mashabiki wa Simba hawana wachoipendea Simba zaidi ya Simba yenyewe. Mafanikio ya klabu hiyo ndiyo furaha kwao. Timu inapoporomoka kwenye mabonde, wanakuwa wanyonge na wenye hasira.
Wanazi wa Yanga hawakushawishiwa kitu kuipenda Yanga zaidi ya Yanga yenyewe. Timu inapofanya vizuri mashabiki wake wanaamka na kutamba, inapopitia nyakati ngumu wanakuwa dhaifu hata mdomoni.
Kati ya Simba na Yanga, timu moja inapokuwa kwenye wakati mgumu, unashuhudia mtikisiko wa mapato kwa jumla. Viwanjani mahudhurio yanakuwa hafifu. Hamu ya mashabiki kufuatilia vyombo vya habari hususan michezo inapungua.
Mapato ni mengi katika mechi za soka pale Simba na Yanga zinapokuwa kwenye kiwango bora zote kwa pamoja. Vyombo vya habari hufuatiliwa mno. Magazeti ya michezo hugeuka lulu hata yale ambayo hufanya kazi zake chini ya kiwango. Ndiyo maana mahasimu wa Soweto Derby, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates siwapi daraja sawa na Simba na Yanga.
Utaona kuwa Simba na Yanga ndiyo soka la Tanzania. Bila zenyewe huuoni mpira ukivutia. Yanga ilipogawanyika na Pan Africa ilidhaniwa kungeibuka ushindani mkubwa kuliko wa Simba na Yanga lakini haikuwa. Hata kifo cha Pan Africa ni menejimenti yake yote kubaki mashabiki wa Yanga.
Klabu nyingi hazichanui inavyotakiwa hapa Tanzania kwa sababu wachezaji na viongozi wake ni mashabiki wa Simba na Yanga. Zipo timu zilizotikisa soka la Tanzania kisha zikafifia kwa sababu ya itikadi za Simba na Yanga.
Simba na Yanga ni zaidi ya siasa
Mmoja wa waasisi wa taifa hili, Kingunge Ngombale Mwiru, mwaka jana katika Uchaguzi Mkuu 2015, alisimama jukwaa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupiga kampeni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kishindwe kwenye uchaguzi.
Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye hivi sasa ni wanachama wa mstari wa mbele wa Chadema, vilevile ni vinara wa muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), isisahaulike kuwa Lowassa ndiye alikuwa mgombea Urais wa Chadema na Ukawa mwaka jana.
Mwasisi wa CCM, aliyekuwa mmoja wa walioviunganisha vyama vya Tanganyika African National Union (Tanu) na Afro Shiraz Party (ASP) upande wa Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, leo hii siyo mwana CCM.
Hivyo basi, CCM na Ukawa unaweza kuhama kirahisi. Ukiona mambo hayaendi sawa au viongozi wa juu huelewani nao, unahamia upande mwingine au hata kuanzisha chama kipya cha siasa.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, aliyeiongoza klabu hiyo kwa mafanikio makubwa, Hassan Dalali ‘Field Marshal’ alipokataliwa kugombea uongozi Simba kwa sababu ya elimu hakuhamia Yanga. Alibaki kuwa mwanachama na shabiki wa klabu hiyo.
Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (Fat), Michael Wambura, ambaye aliwahi pia kuwa mwenyekiti wa Simba, pamoja na kukataliwa mara nyingi kugombea uongozi wa klabu hiyo, ikiwemo hata kusimamishwa uanachama, bado hajawahi kuhama. Wambura amebaki kuwa shabiki wa Simba, anayeamini katika Simba yake.
Lloyd Nchunga na usumbufu alioupata kutoka kwa wazee wa Yanga na madai ya kuhujumiwa mpaka Yanga ikafungwa mabao 5-0 na Simba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwaka 2012, hasira zake hazikumfanya atimkie Simba.
Huo ndiyo hasa uimara wa Simba na Yanga kama taasisi. Ukimfukuza mwana Simba au Yanga uanachama, ataumia tu huku akisubiri uongozi unaofuata umfungulie, na wakati wote atabaki kuwa shabiki wa timu yake. Ukimfukuza uanachama mwana CCM au Chadema, kesho asubuhi anahamia upande wa pili.
Simba na Yanga zikiamua, zinaweza kuamua nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haifai kuchanganya soka na siasa za nchi lakini nguvu ya timu hizo ikitumika sawasawa wagombea uongozi wa nchi wangekuwa wanyenyekevu sana kwa Simba na Yanga.
Ni Simba na Yanga zenye uwezo wa kuwafanya watu wenye itikadi za kisiasa, wanaoshambuliana majukwaani, wakumbatiane uwanjani kwa timu yao kushinda mchezo, huku wakitaniana bila chuki kwa wale wanaoshabikia timu tofauti.
Ndani ya Simba kuna wanachama wa vyama vyote vya siasa, vivyo hivyo kwa Yanga. Ndani ya Yanga kuna watu wa dini zote na madhehebu yote, kama ilivyo kwa Simba. Kwa maana hiyo Simba na Yanga ni nyenzo muhimu ambayo inaweza kutumika vizuri kuwaunganisha Watanzania wakati wote, na inaweza kutumika kwa urahisi kutibu majeraha ya mgawanyiko pale yanapotokea.
Uzuri ni kuwa Simba na Yanga ni upinzani usio na chuki. Mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kuingia uwanjani pamoja kisha kugawana majukwaa ya kukaa kwa kufuata mapenzi yao kisha wakaondoka pamoja njia nzima wakiwa wanabishana bila kugombana. Huu ndiyo umaalum wa Simba na Yanga duniani.
Makosa ya waamuzi ndiyo husababisha mitafaruku ya hapa na pale lakini mashabiki wa Simba na Yanga wenyewe huwa hawagombani. Wanabishana na kutaniana. Hawagawanywi njia za kupita kama mahasimu wa timu nyingine duniani.
Ndimi Luqman Maloto
Karibu kijiweni kwetu: www.luqmanmaloto.com
LikeShow more reactions
Comment
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA DARASA LA SABA 2013 YATOKA, YAPO HAPA ... YAONE HAPA KWA NJIA RAHISI KABISA

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

HIZI NDIO DALILI ZA VVU KWA WATOTO WADOGO

ANGALIA PICHA WADADA HAWA WALIVYOPIGWA

DK MAGUFULI AZISAMBARATISHA NGOME ZA MBOWE, NDESAMBURO NA NASSARI

JIONEE WAREMBO KUMI WA NGUVU AFRIKA MASHARIKI

WAKIANGALIA MATOKEO YA DARASA LA SABA, MBOZI