MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kigoma kujipanga kuchangamkia fursa zitakazotokana na ujio wa Treni ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake umeanza.
" Amesema hapa Mgombea ubunge wa Kasulu Mjini, Prof. Joyce Ndalichako kuhusu SGR, hata mimi nasema huu ni mradi mkubwa ambao kwa Kigoma utakuwa na vituo vingi hivyo jipangeni kuchangamkia fursa za kibiashara,"amesema Dkt. Samia huku akishangiliwa na umati mkubwa uliojitokeza kwenye mkutano huo.
Ameyasema hayo alipokuwa akijinadi yeye na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho katika mikutano ya kampeni Uvinza, Kasulu na Buhigwe.
Amesema kuwa kwenye vituo hivyo yatajengwa maghala ya kuhifadhia bidhaa jambo litakalochangia kuufungua Mkoa huo kibiashara kwa kusafirisha mazao kwenda kuuza hatika katika nchi jirani.
Dkt. Samia amesema kuwa SGR itawavutia pia Wawekezaji kujenga viwanda katika Mkoa huo, hivyo kuongeza wigo wa biashara na ajira kwa vijana.
Aidha, Dkt. Samia amesema akichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na kupata ridhaa ya kuongoza nchi atahakikisha anakamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ya maji, afya, elimu, nishati na mingineyo.
Comments