Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatinga Mkoa wa Geita baada ya jana Oktoba 2,2025 kufanya Kampeni zake katika mkutano mikubwa kwenye Uwanja Kambarage Shinyanga Mjini na kuhitimisha kwenye Uwanja wa Magufuli wilayani Kahama.
Anaingia Mkoa huo leo Oktoba 12, 2025 kwa kuanza kampeni Mbogwe na baadaye mchana katika Jimbo la Bukombe linalogombewa na Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na hatimaye Runzewe.
Mkoa wa Geita umepokea zaidi ya shilingi Trilioni 1.4 kutoka katika Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Juni 2025 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, maji, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, utalii, viwanda, biashara, uwezeshaji wananchi kiuchumi na miradi ya kimkakati.
Ndani ya kipindi cha miaka minne viwanda vimeongezeka kutoka 824 mwaka 2021 hadi viwanda 1,542 mwaka 2025. Kadhalika utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara umeongezeka kutoka leseni 1,346 mwaka 2021 hadi leseni 2,815 mwaka 2025.
Idadi ya vizimba vya kufugia samaki Mkoani Geita imeongezeka kutoka vizimba vinne mwaka 2021 hadi vizimba 27 mwaka 2025 na mitaji iliyotolewa na Serikali kwa wafugaji wa samaki imeongezeka kutoka shilingi Milioni 14 hadi zaidi ya shilingi Milioni 792 kwa mwaka 2025
Kwa upande wa Sekta ya Elimu, hadi mwaka 2021 Mkoa ulikuwa na madarasa 7206 lakini hadi Juni 2025 Mkoa una madarasa Zaidi ya 10500 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35 ambalo limesaidia kuwajengea wanafunzi kupata madarasa mengi ya kusomea na kujifunzia na kuondokana na msongamano wa wanafunzi darasani.
Baada ya kufanya uzinduzi wa kampeni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe ijini Dar es Salaam Agosti 28, 2025, leo Oktoba 12, 2025 Dkt. Samia ameingia mkoa huo ukiwa ni Mkoa wa 25 baada ya kufanikisha kwa kiwango kikubwa kampeni katika mikoa mingine 24.
Tanzania Bara ni; Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, Manyara, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga
Tanzania Visiwani; Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkoa wa Kusini Pemba.
Bado mikoa ya; Dar es Salaam, Rukwa, Katavi, Kagera, Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini Pemba
Akiwa katika mikutano hiyo, Dkt. Samia hujinadi kwa kuelezea mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mikoa hiyo, pia hutoa ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa miaka mingine mitano endapo atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.
Aidha, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza kudumisha Muungano na kuendelea kulinda amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Pia amewatoa wananchi wasiwasi kwamba hakutokuwa na vurugu kwani vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko imara, hivyo siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi tena bila hofu kwenda kupiga kura na kurejea salama majumbani.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, hutumia fursa hiyo kujinadi yeye, wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho.
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203
Comments