Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kwamba hakutokuwa na maadhimisho ya sherehe za Uhuru December 09,2025 na badala yake fedha ambazo zilipaswa kutumika katika sherehe hizo zitapelekwa kutumika kurekebisha miundombinu iliyoharibika kutokana maandamano October 29, 2025.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hayo wakati akiongea na Wakazi wa Mbezi Luis Jijini Dar es salaam leo November 24,2025.
“Ninaungana na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa wote walioathirika na vurugu zilizotokea oktoba 29, 2025, tumuunge mkono Rais na Wajumbe wa Tume iliyoundwa kwa ajili kuchunguza kwenye undani tukio la vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 ili tujue namna lilivyofanyika na hatua stahiki zitakazochukuliwa
“Nimepitia na kukagua uharibifu wa mali na miundombinu ya umma, huwezi kuamini kama tukio hili limetokea Tanzania, Watanzania tunapaswa kujua miundombinu hii ni mali ya umma, tunazijenga kwa fedha zetu sisi Watanzania, si pesa za Serikali”
“Wanaoshabikia uharibifu wa miundombinu ya Umma hawapo hapa nchini, wanawaambia mkachome mali za umma, mkifanya hivi mtaishije? huko wanakoishi haya wanayowaambia mfanye huko kwao hauwezi kuyafanya.
“Wanajipa haki kwamba wao wanaipenda Tanzania, mpenda Tanzania hawezi kukwambia uichome Tanzania, msiwasikilize, mkiichoma zaidi Tanzania wao ndio wanalipwa zaidi”

Comments