Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya uwepo wa mvua na radi kwa kipindi cha Januari 1 hadi 10, 2026, huku vipindi vya mvua vikitarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania.
Kwa mujibu wa TMA, maeneo yanayotajwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi ni mikoa ya ukanda wa ziwa Viktoria abayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara.
Kwa upande wa nyanda za juu Kaskazini-Mashariki mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro itapata vipindi vya mvua machache, hasa katika siku tano za mwanzo za Januari.
Pwani ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani ya Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba vinatarajiwa kupata mvua
Aidha, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo katika kanda ya Magharibi mwa Nchi huku Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida itapata mvua zinazoambatana na radi, hususan katika siku tano za mwanzo za Januari.
Katika Nyanda za juu Kusini-Magharibi mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo wakati mikoa ya Pwani ya Kusini ya Mtwara na Lindi kulingana na taarifa ya TMA itapata vipindi vya mvua machache.
Wakati Kanda ya Kusini mikoa wa Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo, wakulima wote nchini wameshauriwa kuzingatia ratiba za mvua ili kuepuka hasara ya mazao. #EastAfricaTV

Comments