Ninamwongelea "kijana" mmoja wa enzi hizo, mzaliwa wa Mwakaleli maeneo ya Isange, jimbo la Busokelo, wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. Msomi aliyebahatika kusoma wakati wa utawala wa wakoloni nchini Tanganyika.
"Kijana" aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa TANU uliojulikana kama Tanganyika Youth League (TYL).
"Kijana" ambaye mwaka 1960 alikuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe (mkoani Mbeya). Wakati huo Jimbo la Rungwe lilikuwa ni jimbo kubwa sana likiwa na maeneo mengine ya majimbo ya sasa ya Kyela na Ileje na Busokelo.
Huu Ubunge aliupata akiwa bado kijana mdogodogo tu. Baadaye Jimbo la Busokelo lilipoanzishwa mwaka 1965 akachaguliwa kuwa Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Busokelo.
Simulizi zinasema huyu "kijana" kuna siku alitaka kumtandika makofi Waziri mmoja pale bungeni baada ya kujibu kwa "porojo" swali lake aliloliuliza bungeni lililohusiana na jimboni kwake Rungwe. Inasemekana Waziri husika alikuwa anatoa majibu yaliyokuwa yanaongea uongo unautofautiana na uhalisia wa kile kilichopo jimboni kwake Rungwe. Inasemekana Mheshimiwa wetu wa Kinyakyusa Elly Anangisye "akalele fijo", akapandwa na hasira za kutaka kushusha kipigo kwa Waziri huyo humohumo ukumbini.
Kumbukumbu zinasema "kijana" huyo mwaka 1967 alikuwa ni miongoni mwa wanachama nane (8) wa Chama cha TANU waliofukuzwa uanachama kwa ajili ya misimamo yake kwenye kusimamia kile alichokuwa akikiamini. Wengine walikuwemo kwenye sekeseke hilo la kufukuzwa ni pamoja na Oscar Kambona, Mwakitwange, Tuntemeke Sanga aliyekuwa mbunge wa Makete, Bwana Chogga aliyekuwa Mbunge wa Iringa. Moja ya sababu ya kufukuzwa kwao uanachama wa TANU, ni pamoja na kupinga uanzishwaji wa mfumo wa Chama kushika hatamu.
Kumbukumbu zinaendelea kusema huyu "kijana" alikuwa ni mmoja wa watu ambao misimamo yake mingi ilimfanya aonekane kuwa "mwiba" kwa serikali na hasa serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Mwalimu Nyerere. Alikuwa na misimamo isiyoyumba katika kutetea na kusimamia yale aliyokuwa anayaamini. Hakuwa mnafiki, na aliupinga unafiki kwa nguvu zake zote.
Kumbukumbu zinasema huyu "kijana" alikuwa anapigania sana Mwakaleli kuwa moja ya maeneo ya vijiji vya hapa Tanzania kupata umeme wa gridi ya Taifa mapema. Juhudi zake zikaja kuzaa matunda baadaye, na hatimaye maeneo ya Mwakaleli yakaja kuwa na umeme wa gridi ya Taifa mapemamapema. Hii ilichangiwa sana na harakati za awali sana za kijana huyo.
Mwakaleli mpaka siku za sasa inayo miti mingi ya mbao. Simulizi zinasema huyu "kijana" ni mmoja wa watu waliohamasisha sana upandaji wa miti ya mbao maeneo ya Mwakaleli na ndiye aliyehamasisha uanzishwaji wa kiwanda cha kupasua mbao kwenye kijiji cha Isange, baadaye likajengwa jengo kubwa la kiwanda. Jengo hilo baadaye lilikuja kubadilishwa matumizi na kuwa shule ya Sekondari ya Isange ambayo ipo mpaka sasa.
Huyu "kijana" ni ELLY ANANGISYE.
Je, unahitaji kujua mengi kuhusu Mwana wa Unyakyusa huyu na habari nyingine nyinginyingi za Wanyakyusa wengine Mashuhuri? Kama jibu ni "ndiyo" basi jiandae kusoma (kwa undani) kitabu changu ambacho ninakiandika cha "WANYAKYUSA MASHUHURI". Humo utapata kujua mengi kuhusu Wanyakyusa mbalimbali.
Lusako Mwang'onda
Katumba, Tukuyu.
6 Machi, 2026.

Comments