HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAGEUKA KITOVU CHA TIBA AFRIKA MASHARIKI, MAELFU YA WAGONJWA KUTOKA NJE WAMIMINIKA DODOMA- MSIGWA
Na Richard Mwaikenda, Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kujijengea sifa kimataifa baada ya maelfu ya wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati kumiminika nchini kupata huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imewekeza jumla ya shilingi bilioni 283 kuanzia mwaka 2015 hadi 2026 kwa lengo la kuifanya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa kituo cha kisasa cha tiba kinachokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 22, 2026 kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Msigwa alisema uwekezaji huo umeiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma ambazo awali zilipatikana katika mataifa machache duniani.
Kutokana na mafanikio hayo, wagonjwa 2,897 kutoka Burundi na 526 kutoka Comoro wamepata huduma katika hospitali hiyo, huku wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati wakiendelea kuwasili kwa matibabu.
Alisema hali hiyo inaonyesha Tanzania imeanza kujijengea nafasi kama kitovu cha utalii wa matibabu (medical tourism), huku ikipunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu na hivyo kuokoa fedha nyingi za Serikali na wananchi.
Msigwa alisema fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa majengo ya kisasa ya huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu, kuboresha mifumo ya TEHAMA pamoja na kuongeza wataalamu wa afya.
Kutokana na uwekezaji huo, idadi ya watumishi imeongezeka kutoka watumishi 20 mwaka 2015 hadi watumishi 1,076 mwaka 2026, wakiwemo zaidi ya madaktari bingwa na bingwa bobezi 100.
Hospitali hiyo sasa inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo (Cardiac Catheterization), upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, upasuaji kwa njia ya matundu madogo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, radiolojia ya kisasa pamoja na huduma za uchujaji damu (dialysis).
Kwa mafanikio hayo, Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuimarisha hadhi ya Tanzania kama kitovu kipya cha huduma za afya za kibingwa barani Afrika, huku ikivutia wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kutafuta tiba ambazo hapo awali walilazimika kuzifuata nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Comments