............................
NA DOTO MWAIBALE
NAIBU Katibu Kitengo cha Elimu ya Sheria kwa Umma Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), Zainabu Chanzi
amesema kuna umuhimu wa kuandaa mifumo ya kisheria ya muda mrefu bila ya
kubadilishwa mara kwa mara jambo litakalo wasaidia wawekezaji kufanya shughuli
zao bila ya kuwa na hofu.
Hayo
ameyasema wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya
Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam Sabasaba Julai 9,2026.
‘’ Tunahitaji kuwa na mifumo ya kisheria ambayo itakaa muda mrefu bila ya kufanyiwa mabadiliko mara kwa mara, wawekezaji wanahitaji kujiridhisha kisheria na ili kuendelea na biashara ukifanyika utafiti utaangalia maslahi ya wadau wote,’’ alisema Chanzi.
Alisema
Julai 1, 2026 tume hiyo imeanza utekelezaji wa dira ya Taifa ya Maendeleo ya
20-50 na upo muda wa kutosha kuitekeleza hivyo sheria zetu lazima ziakisi
matarajio makubwa ambayo dira hiyo imebeba.
Amesema Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akiizindua dira hiyo aliipa tume yetu jukumu kubwa la kuhakikisha
sheria zote zinaakisi matarajio yote ambayo yapo kwenye dira.
Chanzi
amesema sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa dira kama ambavyo
tunasema tunahitaji uchumi jumuishi na shindani hivyo sheria itoe fursa na ziwezeshe
katika maeneo mbalimbali.
Amesema
ndani ya dira kuna sekta za kimageuzi na
sekta hizo huwezi kuona umuhimu na manufaa yake kama hazita saidiwa saidiwa zikafanya
vizuri.
‘’ Katika kutekeleza maelekezo ya mhe. rais tume kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Tume ya Taifa ya Mipango tumeandaa jinsi ya kuendana na maboresho hayo,’’ alisema Chanzi.
Amesema
wameweza kufanya umbembuzi wa mifumo ya kisheria ambayo wataendanayo ili
kuwezesha dira iweze kufanya kazi.
Chanzi amesema
wameainisha mifumo 28 na watakayoanza nayo ni mifumo miwili, mfumo wa nishati.
‘’ Kama tunavyojua nishati ni kichocheo katika dira imewekwa wazi kabisa kwani tunataka kuwa na nchi yenye viwanda na sekta ya kimageuzi hivyo ili tuwe na viwanda ni lazima tuwe na nishati ya kutosha hivyo tutaangalia mfumo mzima wa sekta ya nishati,’’ alisema.
Aidha, alisema
kuwa wanakwenda kuangalia mfumo wa kisheria unaosimamia biashara, viwanda na
uwekezaji kwa sababu wanaamini sekta nyingine zote za kimageuzi kwa mfano ya
kilimo, uchumi wa buluu, utalii, viwanda vyote hivyo vinawezesha ufanyikaji wa
biashara.
Chanzi
aliongeza kuwa watakapoenda kuangalia mfumo mzima wa ufanyaji wa biashara na
sheria kwa kiwango gani imekuwa ni kikwazo na kuzipitia katika maeneo makubwa
matatu zitaweza kuinua sekta hizo na hakutakuwa na kipingamizi hasa kwenye
mazao ya biashara.
Amesema
Sekta nyingine ni Utalii ambayo ni biashara na wanategemea kuwekeza kwa kuweka
fedha za kutosha na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii na kuwafanya
wafanyabiashara wakubwa kuja kuwekeza kwa kufungua mahoteli makubwa na ili
mambo haya yaweze kufanyika ni kuwepo kwa sheria nzuri za kuvutia.
Amesema
tafiti hizo zitaweza kusaidia utekelezaji wa dira hiyo na kuwa sekta nyingi
zinahitaji sheria ambazo ni dhabiti na mifumo ya usimamizi ambayo ni rafiki na ya
kuwavutia wawekezaji, watekelezaji na
wananchi kwa ujumla.
Chanzi
alisema baada ya mifumo hiyo kupitiwa na sheria zikaandikwa Tume hiyo itarudi
tena kutoa elimu kwa sababu wanaamini kwamba wakiwa na sheria nzuri kwenye
vitabu na wananchi na wadau kwa ujumla hawazitambui, hawaelewi wajibu wao, haki
zao watakuwa hawajafikia lile lengo hivyo watatoa elimu ya mabadiliko ya sheria
yatakapotokea ili wazijue fursa na ndiyo maana wanasema uchumi jumuishi.
Alisema tume
hiyo inaendelea na tafiti nyingine kwa mfano Akili Mnemba (AI) kwani
tukiangalia kwenye dira tunataka uchumi
wa kidijitali na ndiyo uelekeo wa dunia nzima na Tanzania siyo kisiwa hivyo ni
lazima kupitia sheria hizo kwa lengo la kuhakikisha AI zinaweza kutumika bila kuleta
madhara.
Comments