Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, leo ametembelea Soko la Machinga jijini Dodoma kukagua mwenendo wa shughuli za biashara, kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kujionea hatua zinazochukuliwa kuzitatua.
Katika ziara hiyo, Msigwa alipata fursa ya kupata mlo wa supu kutoka kwa mama lishe (Mama Ntilie), akionesha ukaribu na wafanyabiashara na wananchi wanaotumia huduma mbalimbali ndani ya soko hilo.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya soko, Meneja wa Soko la Machinga, Nicholous Mitembo, alisema soko hilo limezidiwa na idadi ya wafanyabiashara kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya nafasi za biashara.
Alieleza kuwa soko hilo lilijengwa kwa uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 2,700, lakini kwa sasa lina wafanyabiashara takribani 4,800, hali inayosababisha msongamano na changamoto za utoaji wa huduma.
Mitembo alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, kuna mpango wa kujenga masoko mapya mawili katika maeneo ya Kisasa na Kizota, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano na kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wa jiji la Dodoma.
Ziara ya Msigwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia kwa karibu hali ya masoko nchini na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafanyabiashara zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Comments