Serikali imeahidi kuhakikisha washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Jukwaa Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) wanayafanyia kazi kwa vitendo kwa kuwawezesha katika mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zitakazochangia ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Morogoro na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Beatrice Njawa, wakati akifungua mafunzo hayo kwa wananchi leo Jumatatu Julai 13, 2026, kwenye Ukumbi wa Bwalo la JKT Umwema.
Bi.Njawa ambaye katika semina hiyo alimwakilisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Adam Malima amesema Serikali inataka kuona mafunzo hayo yanazaa matokeo ya moja kwa moja kwa washiriki kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo, kusindika mazao ya kilimo na kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kushindana sokoni.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayoratibiwa na Jukwaa huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) na kutolewa na wakufunzi wa taasisi ya MAMO ENTREPRNEURSHIP yanalenga kuwajengea wananchi mbalimbali uwezo wa kubuni miradi ya ujasiriamali itakayowaongezea kipato na kuchangia ajira kwa vijana.
Mbali na hayo Njawa amelipongeza JUWATA kwa kuona mbali na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda. “Habari peke yake haitoshi. Amesema kuwa Mwandishi wa habari anaweza kuwa mtengenezaji wa bidhaa na mtumishi wa umma anaweza kuwa mjasiriamali huo ndio mwelekeo wa Taifa,” amesema Bi.Njawa.
Katika hatua nyingine Bi.Njawa ameeleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kupitia Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itafanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha washiriki wanatekeleza waliyojifunza na kuahidi kuwa vikundi vitakavyofanya vizuri vitapewa kipaumbele na mwakani 2027 watapelekwa katika maonesho ya Sabasaba.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa JUWATA wa kuwajengea wanachama wake uwezo wa kujitegemea kiuchumi sambamba na kutekeleza majukumu yao ya kuhabarisha umma.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Beatrice Njawa, wakati akifungua mafunzo hayo kwa wananchi leo Jumatatu Julai 13, 2026, kwenye Ukumbi wa Bwalo la JKT Umwema.Kushoto ni Mwenyekiti wa JUWATA, Richard Mwaikenda na kulia ni Katibu Mkuu wa jukwaa hilo, Ahmad Mohamed.
Mwenyekiti wa JUWATA, Richard Mwaikenda akitoa salamu za jukwaa hilo kabla ya kumkaribisha Mwakilishi wa Mgeni Rasmi Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Beatrice Njawa.
Katibu Mkuu wa jukwaa hilo, Ahmad Mohamed akitoa utambulisho kwa viongozi mbalimbali.
Mwaikenda na Mohamed wakimsindikiza Bi Njawa baada ya kufungua mafunzo hayo.
Wakufunzi kutoka Mamo Enterpreneurship wakifundisha jinsi ya kutengeza bidhaa mbalimbali wakati wa mafunzo hayo.













Comments