Wakulima wavuna Sh. trilioni 2.3; Serikali za Mitaa zakusanya Sh. bilioni 61
Na Richard Mwaikenda, Dodoma
MFUMO wa Stakabadhi za Ghala umeandika rekodi mpya baada ya zaidi ya kilo bilioni 1.1 za mazao tisa kuuzwa kupitia minada ya kidijitali katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku wakulima na wauzaji wakilipwa jumla ya Sh. trilioni 2.298.
Mafanikio hayo yamekuja sambamba na ongezeko la asilimia 43.6 la kiasi cha mazao yaliyouzwa kupitia mfumo huo, ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa imani ya wakulima katika mfumo rasmi wa masoko.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, amesema jumla ya kilo 1,122,246,475 za korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai ziliuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika minada ya kidijitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Bangu alisema kiasi hicho ni ongezeko la zaidi ya kilo milioni 340 ikilinganishwa na kilo 781,659,285 zilizokuwa zimeuzwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ndani ya mwaka mmoja tumeshuhudia ongezeko kubwa la mazao yanayouzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Hii inaonesha wakulima wengi zaidi wanaendelea kuuamini mfumo rasmi wenye ushindani, uwazi na fursa bora za masoko,” alisema Bangu.
Mbali na fedha zaidi ya Sh. trilioni 2.2 zilizolipwa kwa wakulima na wazalishaji, thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia mfumo huo ilifikia Sh. trilioni 2.679.
Serikali za Mitaa nazo zilikusanya Sh. bilioni 61.05 kupitia ushuru wa mazao, maarufu kama CESS, fedha zinazotarajiwa kuongeza uwezo wa Halmashauri kuboresha huduma za jamii na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Bangu alisema mafanikio hayo yamechangia kuongeza kipato cha wakulima na kuboresha ustawi wa kaya, huku fedha zilizopatikana zikiwezesha wananchi kugharamia mahitaji muhimu, yakiwemo elimu, afya na makazi, pamoja na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.
Alisema mapato ya CESS yameendelea kuwa nguzo muhimu kwa Halmashauri katika ujenzi na matengenezo ya barabara, shule, vituo vya afya, masoko na miundombinu mingine.
WRRB, ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ina jukumu la kusimamia na kuhamasisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuwawezesha wakulima na wadau wengine kupata masoko yenye ushindani, huduma za uhifadhi wa mazao na fursa za mikopo.
Mafanikio hayo yameelezwa wakati WRRB ikitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha 2025/2026 na kuweka mwelekeo wa shughuli za mwaka wa fedha 2026/2027.
Sehemu ya waandishi wa habari.
Comments