Serikali imetangaza wanafunzi 1,050 waliofanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2026 watakaonufaika na mpango wa Samia Scholarship.
Kati yao, wanafunzi 50 bora zaidi watapelekwa kusoma nje ya nchi katika fani za Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), Data Science na teknolojia nyingine za kisasa, huku wanafunzi 1,000 wakipata ufadhili wa kusoma katika vyuo vikuu vya ndani.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema mpango huo unalenga kukuza vipaji vya wanafunzi wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kuandaa wataalamu watakaosaidia maendeleo ya Taifa.
Amesema uteuzi umezingatia alama halisi za mitihani na wanafunzi waliopatikana wametoka katika tahasusi mbalimbali za sayansi zikiwemo PCM, PCB, PMG na PMC.
Serikali itagharamia masomo ya wanafunzi hao kwa asilimia 100, huku majina ya waliochaguliwa yakipatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Comments