WAZIRI ULEGA AKAGUA MIRADI MALINYI, DKT. MDAKU AIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb), amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya kimkakati ya ujenzi katika Wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya wananchi.
Katika ziara hiyo, Waziri Ulega alikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Fuluwa, Daraja la Namahanga pamoja na barabara ya Ifakara–Lupiro–Mtimbira yenye urefu wa kilomita 112, miradi inayotarajiwa kuimarisha mawasiliano, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza fursa za kiuchumi katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja ili kuunganisha wananchi na fursa za maendeleo.
Amesisitiza kuwa miradi inayotekelezwa Malinyi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha usafiri, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo ya uzalishaji.
Akitumia fursa ya ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Mhe. Dkt. Mecktridis Mdaku, aliiomba Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi kuharakisha ujenzi wa barabara za lami ndani ya jimbo hilo, akisema kukamilika kwa madaraja pekee hakutatosha kufungua uchumi wa Malinyi bila kuwa na mtandao bora wa barabara.
"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea Malinyi. Sasa tunaomba Serikali ikamilishe azma hii kwa kuharakisha ujenzi wa barabara za lami, kwani ndizo zitakazorahisisha usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi," alisema Dkt. Mdaku.
Dkt. Mdaku pia aliiomba Serikali kuipa kipaumbele barabara ya Malinyi – Songea, akieleza kuwa ni njia muhimu ya kuunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma.
Ziara hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wabunge wa Mkoa wa Morogoro, viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na wakurugenzi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS.
Kukamilika kwa miradi hiyo pamoja na utekelezaji wa maombi ya ujenzi wa barabara za lami kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo katika Wilaya ya Malinyi kwa kuboresha usafiri na usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuongeza biashara na uwekezaji, na kuimarisha uchumi wa wananchi.
.jpg.jpeg)
.jpg.jpeg)
.jpg.jpeg)
.jpg.jpeg)
.jpg.jpeg)
.jpg.jpeg)
Comments