Wananchi wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika TikTok LIVE ya dharura iliyoendeshwa leo, Oktoba 4, 2026, na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, *Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,* iliyolenga kujadili changamoto za wanaume kwenye ndoa.
Katika kipindi hicho, wananchi wakiwemo wanaume walipata fursa ya kueleza kwa uwazi uzoefu na changamoto ambazo wanaume wanazokutana nazo katika maisha ya ndoa, huku wakitaja sababu mbalimbali wanazoona zinachangia migogoro ya ndoa na familia kwa ujumla. Aidha, wanaume walifunguka kuhusu yale ambayo wamekuwa wakiyabeba kimya bila kupata nafasi ya kuyazungumza, jambo lililoonesha namna mjadala huo ulivyowagusa wananchi na hasa wanaume.
Kwa muda wa saa 4 na dakika 26, TikTok LIVE hiyo ilifikisha jumla ya watazamaji 108,900, maoni 10,300, likes 270,500 na wafuasi wapya 2,200. Aidha, LIVE hiyo ilipokea zawadi kutoka kwa watoa zawadi 71 zilizofikia diamonds 1,000, takwimu zinazoonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika mjadala kuhusu masuala ya ndoa na familia.
Mjadala huo uliibua hoja mbalimbali kuhusu mawasiliano katika ndoa, kuheshimiana, uaminifu, uwajibikaji, malezi ya watoto, changamoto za kiuchumi na namna wanandoa wanavyoweza kukabiliana na migogoro. Wanaume waliopata nafasi ya kuzungumza walieleza changamoto mbalimbali wanazopitia, huku wengine wakitoa maoni na mapendekezo kuhusu namna jamii inavyoweza kusaidia wanandoa kukabiliana na changamoto hizo.
TikTok LIVE hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa dini imekuwa pia jukwaa la wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kusikilizana, kubadilishana uzoefu na kutafuta kwa pamoja njia za kujenga familia zenye amani na ustawi. Mjadala huo umeendelea kuonesha umuhimu wa wanandoa kuzungumza kwa uwazi kuhusu changamoto zao, kusikilizana na kutafuta ushauri na suluhisho sahihi kwa ajili ya kujenga ndoa na familia imara.

Comments