NAIBU WAZIRI AKOSHWA NA JITIHADA ZA MBUNGE MECKTRIDIS KUWAINUA VIJANA WA MALINYI KIUCHUMI



Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Dkt. Evaline Munisi amempongeza Mbunge wa Malinyi Mhe. Dkt. Mecktridis Mdaku kwa jitihada zake za kuwainua vijana wa Malinyi kiuchumi kwa kuwapatia ujuzi wa elimu. 

Amesema kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana walio wengi bado ni kubwa na inaleta athari katika uchumi na uzalishaji mali nchini, fursa hii ni ya kipekee sana kwa kuwa itasaidia kuwainua na kuwatengenezea uchumi jumuishi. 

"Mhe Mbunge nakupongeza sana kwa jitihada hizi, maana imeisaidia sana Serikali katika utekelezaji wa mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mafunzo ya ufundi ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe," amesema Dkt. Evaline katika mahafali ya 48 ya Chuo cha FDC kilichopo Kata ya Sofi, Wilayani Malinyi.

Amebainisha kuwa Serikali bado inatambua changamoto iliyopo ya ajira, kwa kushirikiana na sekta binafsi, inatekeleza mkakati wa kuwainua vijana kiuchumi ili waweze kuwa na tija katika maisha yao, jamii yao na taifa lao kwa ujumla. 

Katika mahafali hayo, jumla ya vijana 150 kutoka Wilaya ya Malinyi wamehitimu mafunzo hayo ambao ni sehemu ya mkakati wa Mbunge wa kuwawezesha vijana 500 ndani ya kipindi cha miaka mitano. 

Kwa upande wake Mbunge wa Malinyi Dkt Mecktridis amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo haya ni ili kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwaondolea utegemezi kwa familia, bali waweze kuwa tegemeo kwao. 

Amewataka vijana kutobweteka na mafunzo haya, bali wajitahidi kutafuta na kuchangamkia fursa zilizopo ili waweze kunufaika na fursa zinazojitokeza. 

"Nipende kuiomba Serikali iendelee kuangalia kwa karibu changamoto zinazowakabili vijana wetu baada ya kumaliza mafunzo, tunataka tuone matokeo ya elimu hii katika maisha yao," ameeleza Mbunge Mecktridis. 

Ndugu Farida Mgomi mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ametoa shukrani zake kwa Mbunge Dkt kwa fursa aliyowapatia ya mafunzo ambayo itawafungulia fursa ya kunufaika uchumi. 

"Binafsi huu ni mtaji mkubwa kwangu ambao utanisaidia kujiendeleza kiuchumi na kunipa msingi wa kuboresha maisha yangu kwa ujumla," amesema Bi Farida.






 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

𝐌𝐉𝐔𝐄 𝐊𝐀𝐂𝐇𝐄𝐑𝐎 𝐌𝐙𝐄𝐍𝐀

KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA.

YANGA YAMPOTEZA MAMA FATMA KARUME MWANA YANGA KINDAKI NDAKI

MVUA ZA EL NINO ZINASABABISHWA NA NINI?.

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU