Naomba niwazungumzie watu wanne katika makala haya. Sababu ya kufanya hivyo ni kutoa mchango wa kifikra kuhusu joto la sasa kutokana na ajenda zinazogonganisha vichwa vya watu nchini kwetu.
Nawazungumzia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mfanyabishara na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, vilevile kada wa Chadema, Ben Saanane.
Kila mmoja nina sababu naye za kumjadili. Wapo ambao wamesababishiwa na wenzao lakini wengine ni wahusika wa moja kwa moja. Muhimu ni kufikisha kile ambacho nimeona nifikishe kwa wenzangu. Ni jambo la afya kuendelea kushirikishana masuala ya nchi yetu.
Kabla sijaendelea, jana kwenye akaunti yangu ya Twitter niliandika ujumbe wenye tahadhari, nikaeleza kuwa hivi wanaomshambulia Makonda kuwa ameghushi cheti, siku akithibitisha bila kuacha shaka kuwa elimu yake ni halali kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu, wataweka wapi sura zao? Nakumbusha kuweka akiba ya maneno.
Nikauliza pia endapo Makonda itathibitika kweli cheti ameghushi kisha akang’oka ukuu wa mkoa wa Dar es Salaam, na kwa vile vishindo vyake vya mamlaka, je, atakuwa mgeni wa nani? Hapa nakumbusha unyenyekevu.
MAKONDA
Tuhuma kwamba alitumia cheti cha kughushi cha kidato cha nne ili kujiunga na masomo ya elimu ya juu, zimekuwa kubwa sana. Kila mmoja sasa anazungumza. Wengine inafikia hatua wanamkashifu na kumdhalilisha. Hatupaswi kufika huko.
Nawaomba vijana wa Tanzania yetu, wajitengeneze kuwa wenye nidhamu. Wajenge hoja bila kutukana. Kutukana sana haina maana ndiyo ujumbe wako unafika barabara. Kutukana ni dalili ya kupoteza hadhi ya kiutu.
Unadhani Makonda amekosea? Kama ndivyo basi tumia uhuru wako wa kutoa maoni kwa kumfikishia ujumbe au kuusema ujumbe bila matumizi ya lugha za kuudhi na kashfa.
Makonda ni kiongozi, kwa hiyo wakati unamfikishia ujumbe unahitaji kuwa na heshima pamoja na angalizo kwa nafasi yake. Sentensi hizi mbili “muongo mkubwa wewe” na “ndugu hapo hujasema kweli”, zina maana sawa, isipokuwa moja imetoka kwa lugha mbaya, nyingine kwa lugha ya kuelewesha na kusahihisha bila kuudhi.
Sasa tujadili mada; je, Makonda anajadiliwa kwa kupata sifuri mtihani wa kidato cha nne? Kama mjadala upo hivyo kuanzia sasa nitamtangaza Makonda kuwa shujaa wangu.
Maana kama alipata sifuri kidato cha nne na sasa ana shahada ya chuo kikuu, maana yake ni mpambanaji hasa. Maisha yana rangi nyingi sana, wakati mwingine kufeli mtihani darasani siyo kiwakilishi cha ubovu wa akili ya mtu.
Kama hoja ni Makonda kupata sifuri, maana yake unanipa picha tofauti kuwa Makonda baada ya kufeli alituliza kichwa na kujiuliza kisha akaona makosa yake, kwa hiyo alibadili uelekeo na sasa ni msomi wa chuo kikuu.
Mtu huyo siyo wa kumdhihaki. Huyo ni mtu bora kabisa kwenye nchi yetu. Kumbe sasa Makonda kama kweli alifeli kidato cha nne kisha akatumia njia halali kufika chuo kikuu, maana yake anatosha hata kuwa hamasa ya vijana wengine wenye kufeli kidato cha nne na kukata tamaa ya maisha.
Kumbe Makonda ni kioo cha vijana wengine wanaochukua njia mbaya za kimaisha baada ya kufeli kidato cha nne. Kwamba Makonda ni mfano wa kuigwa kwao kwa sababu alipata sifuri (kama ndiyo hivyo) kisha akajituliza na kufuata njia bora na sasa ni msomi wa chuo kikuu.
Je, mjadala ni kughushi cheti? Kama ndiyo, basi huu ndiyo uwe mjadala halafu suala la kupata sifuri liachwe, maana halina maana yoyote.
Wapo wengi kutokana na changamoto za kimaisha walijikuta wanapata sifuri kidato cha nne lakini walitulia na kujiendeleza na wamekuwa watu bora kabisa. Wapo pia walipata daraja la kwanza na wakafika mpaka vyuoni na kutunukiwa shahada zao lakini chakula kinachotoka kwenye ubongo wao hakivutii.
Tumekubaliana mjadala siyo sifuri, badala yake ni kufanya udanganyifu wa cheti. Ikiwa ni kweli Makonda alighushi cheti cha kidato cha nne, anapaswa yeye mwenyewe kuona aibu na kumsaidia Rais John Magufuli kwa kujiweka pembeni.
Udanganyifu wa cheti siyo jambo zuri. Hili lisiposhughulikiwa ipasavyo, taifa litakuwa na mfano mbaya sana. Vijana wengine wenye kufeli kidato cha nne, wataona hakuna umuhimu wa kurudia mitihani watengeneze matokeo yao, bali watajua njia bora ni kununua. Mfano wao utakuwa Makonda alinunua na alifanikiwa.
Makonda anatakiwa apokee kama kiongozi kisha achukue hatua mahsusi, ama kuuthibitishia umma kuwa yote yanayosemwa siyo sahihi au kujiuzulu ili kuruhusu vyombo vya sheria vifanye kazi yake.
Jambo lolote atakalolifanya kati ya hayo mawili, atakuwa amemsaidia Rais Magufuli, vilevile kuliponya taifa. Kwamba Rais Magufuli hatakuwa na kazi ya kumfukuza kazi tena. Kwamba taifa litakuwa limejifunza kuwa udanganyifu wa cheti cha shule ni dhambi kubwa isiyobagua kiongozi wala raia wa kawaida.
Kama Makonda kweli anaitwa Daud Albert Bashite na kwamba jina la Paul Christian alilinunua kwa mtu pamoja na cheti chake cha kidato cha nne, ni suala la kugundua kuwa siri imebumbulika.
Ni heshima kwake kujiuzulu kuliko kufukuzwa kazi. Afanye kama alivyofanya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, hayati Ditopile Mzuzuri, alipopatwa na kesi ya kumpiga risasi dereva wa daladala, marehemu Hassan Mbonde, yeye mwenyewe alimwandikia barua Rais ya kujiuzulu.
Katika barua yake, Mzuzuri alisema kuwa anajiuzulu ili kutoa uhuru kwa vyombo vya dola kushughulikia kesi yake. Yaani alijiuzulu ili kuviondolea hofu vyombo vya dola kuwa vinashughulika na kiongozi, bali mtu wa kawaida.
Kwa vile hili suala la Makonda nalo, ikiwa lipo kama linavyozungumzwa basi na lenyewe linahusu makosa ya kisheria. Akijiuzulu atazisaidia mamlaka kumfungulia mashitaka kama mtu wa kawaida na siyo kiongozi.
HAKUNA DHAMBI YA PEPONI
Zipo sauti nyingi zinapazwa kuwa kelele za cheti zinasababishwa na vita ya wauza dawa za kulevya. Sikubaliani na hoja hiyo, ingawa naweza kukubali kwamba watu wasiompenda Makonda kwa sasa wamepata fimbo ya kumcharaza hasimu wao.
Usiseme vita ya wauza dawa za kulevya ni ngumu ili kuhalalisha cheti bandia cha Makonda kama kweli anacho. Mtetee Makonda kwa kujibu hoja zote zinazotolewa. Kwamba safari nzima ya kielimu ya Makonda ni halali na haina doa. Huo ndiyo utetezi unaopaswa kutolewa kwa wakati huu.
Hao wauza dawa za kulevya ni akina nani mpaka wawe huru kumshambulia Makonda? Huu ni utoto ambao kwa watu wenye fikra timamu wanajisikia vibaya kuusikia ukisemwa kumtetea Makonda.
Kama kweli Makonda alighushi cheti, basi dhambi yake isifunikwe kwa kisingizio cha wauza dawa za kulevya. Uhalifu mmoja siyo pepo ya uhalifu mwingine.
Uhalifu wa kughushi cheti siyo pepo dhidi ya uhalifu wa biashara haramu ya dawa za kulevya. Wote ni uhalifu. Kwa hiyo dhambi ya kughushi cheti ya Makonda (kama kweli ameitenda), haipaswi kufichwa kwenye kivuli cha mapambano ya dawa za kulevya.
Kwanza muuza unga gani huyo anayepambana na Makonda? Maana wote aliowataja wapo mitaani, hakuna hata mmoja ambaye alithibitika.
Hivyo basi, kusema Makonda anashambuliwa na wauza unga ni kuwaonea wale waliotajwa kisha wakabainika kuwa hawahusiki. Watu wasihukumiwe kwa makosa ambayo hayajathibitishwa na mahakama.
Tena kwa maneno haya ni matusi hata kwa Serikali, kwamba wauza unga walikamatwa, wakaishinda Serikali na sasa wanaendesha vita dhidi ya Makonda. Haya siyo maneno mazuri kuzungumzwa.
Nayasema haya kuweka sawa huu mjadala. Ni vizuri hasa Makonda ajitetee na ashinde hii vita dhidi yake ili kama kijana awe na safari njema ya kiuongozi. Na kama ni kweli dhambi inayotajwa kaitenda, basi vita ya dawa za kulevya isiwe chimbo la kujifichia (scapegoat).
MANJI
Hakuna taarifa rasmi kutoka vyombo vya usalama kuhusu Manji, zaidi ya ile ya uhamiaji kuwa walikuwa wakimsubiri atoke hospitali Muhimbili ili wamlaze mahabusu. Wakati huo Manji alikuwa amelazwa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Manji alilazwa Muhimbili baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam, alipowekwa mahabusu baada ya kutajwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ingawa alifunguliwa kesi ya kutumia na siyo kuuza.
Habari zinasema Manji anaumwa matatizo ya moyo na amelazwa hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Wakati huohuo, zipo habari kuwa akaunti zake zimezuiwa. Nyingine zinasema Manji amekutwa na uraia wa nchi mbili.
Kampuni zake zinashindwa kujiendesha. Gazeti lake la Jambo Leo halijachapwa na kuingia mitaani kwa wiki nzima sasa. Angalau hili linathibitishika kwa urahisi.
Hapa ndipo kwenye utata kuhusu Manji na lazima tujadili kwa sababu Manji akiathirika, wanaothirika ni Watanzania wengi mno ambao maisha yao yapo kwenye ajira kupitia kampuni za Manji.
Shida ni kuwa Serikali haisemi kitu. Je, watu wa Manji wanaisingizia Serikali, kwamba yenyewe haijafunga akaunti hata moja ya Manji? Serikali inatakiwa itoke na kukanusha kusingiziwa huku.
Kama ni kweli akaunti za Manji zimezuiwa, maana yake hiyo ni kesi nzito mno. Na inapaswa kuelezwa kinagaubaga ili Watanzania wengine wajue kuwa nini ambacho kinamsibu Mtanzania mwenzao. Izingatiwe kuwa Manji ni mwekezaji mkubwa nchini.
Maana kama ni ile kesi ya uhamiaji mbona watuhumiwa walishapandishwa kizimbani na dhamana yao kuwekwa wazi?
Kilichosababisha akaunti za Manji zizuiwe ni nini? Je, ni ile kesi yake ya matumizi ya dawa za kulevya au ya uhamiaji? Mbona kesi hizo hazina uzito wowote wa kusababisha akaunti za mfanyabiashara mkubwa kama Manji zifungwe?
Nini kimesababisha? Serikali iseme, kufanya vitu kimyakimya si vizuri kwa uendeshaji wa nchi. Manji ni Mtanzania, hata kama angekuwa siyo Mtanzania, vema kama anakuwa na matatizo ya kisheria yasemwe na mchakato uonekane ukitendeka.
Serikali ijiepushe na nyenendo ambazo itaonekana inafanya vita binafsi na raia wake. Hata kauli ya uhamiaji kuwa walitaka kumlaza Manji mahabusu kwa makosa ya wafanyakazi wa Quality Group kutokuwa na vibali, haikuwa njema.
Kwa mtu yeyote anayeifahamu nafasi ya Manji Quality Group lazima ashangazwe na kauli ile. Kwa nini Manji binafsi na siyo mamlaka za ajira?
Gazeti la Jambo Leo linatengeneza ajira za Watanzania wengi sana. Anzia chumba cha habari, idara ya masoko, usambazaji mpaka kwa wauzaji mitaani. Wote hawa wameathirika na gazeti kutoingia sokoni.
Jambo Leo ni gazeti ambalo uwekezaji wake ni mkubwa mno. Jambo Leo usilitazame kama gazeti tu, thamani yake ni kubwa mno kwenye uwekezaji.
Nimelifanyia kazi Jambo Leo na nilikuwa sehemu ya timu iliyolibadili kutoka sera na mwonekano wa zamani mpaka kuwa lilivyokuwa katika upya wake. Sina shaka mchango wangu Jambo Leo unaendelea kuenziwa.
Hivyo basi, natambua uwekezaji uliofanywa na Quality Group kwa Jambo Leo. Uwekezaji huo haupaswi kupuuzwa. Si rahisi kupata watu kwenye tasnia ya habari wakawekeza kama Quality Group walivyofanya.
Ndiyo maana mimi kama mwanahabari naumizwa hali iliyopo sasa, maana ni pigo kwa tasnia ya habari, lakini zaidi ni athari ambazo waandishi wenzetu wa habari wanazipata kwa sasa pamoja na Watanzania wengine wote ambao walikuwa wananufaika na mzunguko wa kibiashara wa gazeti hilo.
Mimi sipo Quality Group, nilishaondoka. Hata hivyo, ukweli ndani ya moyo wangu ni kuwa ilikuwa kampuni bora kufanya nayo kazi. Niliondoka kwa hiari yangu na kwa kufuata taratibu za ajira kutokana na mtazamo wangu wa kimaisha.
Niliwaacha ndugu zetu wengi wakiwa na furaha lakini sasa hawana furaha, maisha ya kazi yamekuwa na wasiwasi mkubwa. Serikali ilione hili. Iseme wazi makosa ya Manji kisha iangalie namna ya kushughulika naye kisheria bila kuathiri maelfu ya watu ambao ajira zao zipo Quality Group.
MBOWE
Namzungumzia kidogo tu; mjadala kuhusu Makonda kughushi cheti umeamsha watu wengine kuhoji elimu ya Mbowe, kwamba eti naye aoneshe cheti chake. Wapo wanaosema Mbowe alipata sifuri kidato cha sita.
Nawakumbusha Watanzania kutumia busara. Tanzania haipaswi kuwa na vijana wapiga domo, wapenda kulaumu na ushabiki pasipo kuwa na ujazo wa kutosha kichwani.
Hivi suala la Makonda linafanana vipi na Mbowe? Makonda anatuhumiwa kughushi cheti, je, Mbowe naye aliwahi kughushi cheti?
Wanaomtuhumu Makonda wametoa taarifa ambazo kwa kiasi kikubwa zinafikirisha. Wanaomtuhumu Makonda wamekuja na maelezo ambayo si ya kusikiliza na kupuuzwa, yanaonekana yana kitu ndani yake.
Nawe kama unaamini Mbowe alighushi cheti, njoo na taarifa zako. Siyo kupaparika kuzungumza vitu ambavyo havina ushahidi ili kuchafua majina ya watu.
Mbowe ni Freeman yuleyule tangu alipozaliwa, wanaomtuhumu Makonda wanasema Paul wa sasa ni Daud wa zamani.
Naomba kushauri jambo hili kwamba linapoibuliwa suala nyeti kwa nchi, kama hili la Makonda kutuhumiwa kughushi cheti, inatakiwa liachwe lichukue mkondo wake, kisha na wewe kama unazo tuhuma za Mbowe uje nazo.
Usiseme Mbowe alipata sifuri, huo siyo mjadala kwa wenye akili timamu. Njoo useme Mbowe alighushi cheti halafu ueleze ushahidi.
Mjadala unasema Makonda kaghushi cheti, wewe unakuja mbio “mbona Mbowe alipata sifuri”, je, kama kweli Mbowe alipata matokeo hayo, ndiyo yanahalalisha Makonda kughushi cheti? Vijana kueni, tena ukuaji wa vichwa, siyo vichwa viwe vikubwa, la! Ujazo ndani ya kichwa uwe na afya.
BEN SAANANE
Kelele nyingi kuhusu Makonda na umaarufu wa jina la Daud Bashite uliopo sasa, umenifanya nione kuwa kumbe Watanzania wakiwa na mshikamano na kuhoji jambo linawezekana.
Kelele za mitandaoni kuhusu Makonda kama zingetumika kuhoji mahali alipo Ben, zingefanya mamlaka za nchi zijue kuwa suala la Ben lina athari kubwa kijamii na halipaswi kufanyiwa mzaha au kupuuzwa.
Mwezi wa nne sasa Ben hajulikani alipo. Inatakiwa watu wapaze sauti na Serikali itambue kuwa siyo rahisi Watanzania wapotelewe na ndugu yao kisha wanyamaze kama hakijatokea kitu.
Naamini kuwa Serikali ikiamua kulivalia njuga suala la Ben, majibu yatapatikana na itajulikana ni wapi alipotelea. Ben hapaswi kupotea kama Mtanzania wa enzi za ujima. Ben ni kijana wa kisasa, akifuatiliwa zipo alama alizoacha zitatoa majibu.
Niliwahi kuandika kuwa Tanzania siyo Alaska, Marekani, ambako watu mamia hupotea kila mwaka pasipo kujulikana walipokwenda. Tanzania ni Tanzania, mtu akipotea tunajua kuna chanzo. Hicho chanzo ndiyo tukitafute na tukijue.
Hivyo basi, kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha anaifanya Tanzania yake inakuwa si rahisi kwa matukio ya hovyo, ama kupoteza watu au watu kujipoteza. Watanzania wanatakiwa kuwa na mshikamano wa kuhoji kuhusu Ben na majibu yenye kutosheleza yatolewe.
Zingatia kuwa kama Ben amepotezwa, waliocheza mchezo huo wataendelea kucheza na wengine, ipo siku watakuja kwako au kwa ndugu yako. Ndiyo maana nimesema Watanzania wanatakiwa kuhoji sana ili kama wapo watu hao, wapate ujumbe kuwa Tanzania siyo rahisi.
Hata kama ni Ben mwenyewe alijipoteza, naye apate ujumbe kuwa Tanzania siyo rahisi. Kwamba huwezi kufanya mchezo wa hovyo kwa nchi yao kisha ukafanikiwa kwa urahisi tu. Tuendelee kuhoji Ben. Tumuombe Mungu amlinde Ben. Kama kuna watu wamecheza mchezo mchafu, basi Mungu atusaidie kuwabaini.
Ndimi Luqman MALOTO
Karibu sana www.luqmanmaloto.com
Comments