NMB YAMTAMBULISHA MTOA HUDUMA KWA WATEJA KIDIJITALI



 
NA MWANDISHI WETU
 
KATIKA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya NMB imeitambulisha kampeni kubwa ya mapinduzi huduma kiteknolojia iitwayo Sisi ni Huduma ‘Tumekupata,’ utambulisho uliofanyika sambamba na uzinduzi wa Mtoa Huduma wa Kidigitali ‘Chatbot’ aliyepewa jina la NMB JIRANI.
 
Utambulisho na uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Oktoba 7, ambako Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema Huduma kwa Wateja ni Ajenda ya Kimkakati, inayohitaji uwekezaji wa hali ya juu kwa wafanyakazi na teknolojia ili kuendana na kasi ya kukua kwa taasisi yake hiyo.
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Bi. Zaipuna alisema katika kukidhi mahitaji ya wateja zaidi ya milioni 8 wa benki hiyo Sisi ni Huduma na NMB JIRANI inaenda kuleta masuluhisho mbalimbali kwa wateja na wasio wateja wao.
 
“NMB ni benki inayokua kwa kasi sana na hili limetusukuma kuifanya Huduma kwa Wateja kuwa ni Ajenda ya Kimkakati, mafanikio tuliyoyapata katika miaka mitano ya karibuni, yametusukuma kuyaangalia mafanikio hayo kwa namna ambavyo benki imegusa maisha ya watu kijamii na kiuchumi.
 
“Takwimu zinaonesha kuwa mikopo kwa wateja wa NMB imeongezeka sana tangu mwaka 2019 ilipokuwa Sh. Trilioni 3.6 hadi Sh. Trilioni 8 mwaka huu wa 2024 iliyoenda katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, biashara, mashirika na watu binafsi, kwahiyo tukahitaji kutanua wigo wa kuwahudumia.
 
“Benki imekuwa kwa kasi kimtandao, unaojumuisha matawi 231, mawakala wanaongezeka kutoka 6,000 mwaka 2019 hadi 44,000 hivi sasa, pia tulikuwa na akaunti za wateja milioni 3 mwaka 2019 na sasa zimefikia milioni 8. Menejimenti tukatafakari namna gani ya kuiendesha benki inayokuwa kwa kasi kama hii.
 
“Tukaona tufanye mapinduzi makubwa katika huduma kwa wateja na kuifanya hii kuwa ni Ajenda ya Kimkakati na unapoweka ajenda ya kimkakati, unahitiaji uwekezaji wa hali ya juu kwa wafanyakazi na teknolojia, hivyo mafunzo ya ndani miezi mitatu iliyopita na leo tunazindua kampeni hii pamoja na NMB JIRANI.
 
Bi Zaipuna akaongeza ya kuwa, hakutakuwa na gharama yoyote kuhudumiwa na NMB JIRANI, bidhaa iliyotokana na ukweli kuwa changamoto kubwa wanayopitia watoa huduma ikiwemo NMB ni maswali kutoka kwa wateja, ambapo Vituo vya Huduma kwa Wateja vimeshindwa kumaliza hilo kutokana na kuelemewa.
 
“Njia pekee ya kumaliza maswali ya wateja ilikuwa ni Vituo vya Huduma kwa Wateja, ambavyo mara kadhaa vimezidiwa, tukaona tuje na NMB JIRANI, ambaye ni muhudumu kwa njia ya kidijitali, atakayejibu maswali ya wateja na hata wasio wateja wetu.
 
“Iwe maswali kuhusu huduma zetu na masuluhisho yetu, ambako mteja ataingia kwenye tovuti yetu ya www.nmbbank.co.tz eneo la TUTAFUTE au kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp (0747 333 444), kisha JIRANI atajibu maswali kuhusu thamani ya pesa za kigeni, bima, mikopo na mengineyo.
 
Aliongeza ya kwamba ukuaji wa benki yake umeenda sambamba na mafanikio yanayojumuisha tuzo kubwa mbalimbali za kitaifa na kimataifa, zikiwemo Tuzo ya Mlipa Kodi Bora wa Mwaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyopewa kwa miaka miwili mfululizo.
 
Alibainisha kuwa ongezeko la thamani ya gawio kwa wanahisa na hata thamani ya hisa moja moja, vinaakisi uimara, umadhubuti na ubora wa NMB, ambayo mwaka 2019 ilitoa gawi la Sh. Bilioni 33, lililoongezeka hadi kufikia Sh. Bilioni 181 mwaka huu, huku thamani ya hisa moja ikipanda kutoka 2,300 hadi Sh. 5,440.
 
Bi Zaipuna aliishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuweka miongozo sahihi na mazingira bora, rafiki na wezeshi ya kutoa huduma za kibenkii nchini kiasi cha kuharakisha ukuaji kiuchumi kwa taasisi za fedha na kukuza pato la taifa kwa ujumla.
NMB debuts 'Jirani' Chatbot in commemoration of Customer Service Week 2024
 







 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

𝗠𝗕𝗢𝗪𝗘 𝗔𝗦𝗜𝗧𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗠𝗔𝗡𝗢 𝗬𝗔 𝗖𝗛𝗔𝗗𝗘𝗠𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗥𝗘𝗛𝗘 𝟮𝟯.

KAMATI YA UWT KUTOA MSAADA WA KISHERIA NCHINI

YANGA YAWASILI SALAMA ETHIOPIA

KIKOSI CHA CBE KIMEWASILI ZENJI KUVAANA NA YANGA