Katika mazingira ya sasa hivi ya ajira yenye ushindani mkubwa wa kuvutia na kuhifadhi vipaji bora, Benki ya NMB imeendelea kuwa mwajiri kinara nchini na chaguo pendwa la wafanyakazi wa kada zote.
Kupitia uwekezaji wake endelevu katika maendeleo ya rasilimali watu, ustawi wa wafanyakazi, na kuboresha mahali pa kazi, NMB inazidi kuimarisha ufanisi wake kiutendaji huku ikiwavutia wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu.
Mafaniko haya ni miongoni mwa sababu za kutunukiwa ithibati ya kimataifa kama Mwajiri Bora wa Mwaka 2025 nchini, tuzo iliyotolewa na mamlaka ya kimataifa ya rasilimali watu ya Top Employers Institute mwanzoni mwa mwaka huu.
Waajiri Bora Duniani wa Mwaka 2025
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wake, kutambuliwa huku kimataifa ni kielelezo cha wazi cha dhamira ya NMB katika kusimamia rasilimali watu kwa viwango vipya vya juu vya ajira na ustawi wa wafanyakazi wake.
"Watu wetu ndio rasilimali yetu kuu. Tunaamini kuwa kujenga mazingira bora ya ajira, yanayohamasisha ustawi na maendeleo ya wafanyakazi, kunachangia moja kwa moja sio tu katika mafanikio ya biashara yetu bali pia katika kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha uaminifu wao kwetu,” alisema kiongozi huyo baada ya NMB kutangazwa kuwa miongoni mwa waajiri bora 2,400 duniani wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa wataalamu wa rasilimali watu wa NMB, ushindi huu unathibitisha kuwa katika uendeshaji wa kisasa wa taasisi, ustawi wa wafanyakazi si anasa bali ni mtaji wa kimkakati.
Wakizungumza kwa nyati tofauti, walisema mafanikio ya kiutendaji na uendeshaji inayoyapata benki hiyo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanyika kuchochea ukuaji wa vipaji, kuboresha mazingira ya kazi na kuwaendeleza kitaaluma.
Afya za Wafanyakazi na Ustawi Wao
Tofauti na taasisi nyingi, Benki ya NMB imeonesha kwa upekee kwamba uwekezaji madhubuti katika rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kazi ni msingi imara wa mafanikio ya kibiashara.
Hilo linathibitishwa na tafiti za kisayansi zinazoonyesha kuwa kuzipa kipaumbele afya za wafanyakazi na kujali ustawi wa wao si tu kunawahamasisha kushiriki kikamilifu katika utendaji na kuimarisha uhifadhi wa vipaji, bali pia huchochea ongezeko la tija, kukuza ubunifu, na kuimarisha uendelevu wa biashara.
Kwa mujibu wa Bw Joseph Ngalawa, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu – Huduma Shirikishi wa NMB, dhamira thabiti ya benki hiyo katika kuimarisha ubora wa mahali pa kazi ni kielelezo cha jinsi uwekezaji katika ustawi wa wafanyakazi unavyochangia kuongezeka kwa tija, ushirikishwaji wa dhati wa wafanyakazi, na ukuaji endelevu wa taasisi.
Programu za Afya na Ustawi wa Wafanyakazi
Kupitia programu mahiri za kuboresha afya na ustawi wa rasilimali watu, NMB si tu kwamba imeimarisha nafasi yake ya ushindani katika sekta ya huduma za kifedha, bali pia imeweka viwango vipya vya mafanikio ya muda mrefu ambavyo ni muhimu kwa taasisi yoyote yenye maono ya kimkakati.
“Kuwekeza katika ustawi wa wafanyakazi huleta manufaa makubwa kwa pande zote – wafanyakazi huwa na ari na morali wa kufanya kazi kwa bidii, huduma kwa wateja kuboreka zaidi, na waajiri kujenga misingi madhubuti ya mafanikio ya kudumu, “alisema Bw Ngalawa, katika mahojiano maalum yaliyofanyika mjini Moshi Jumamosi iliyopita.
Bw Ngalawa alibainisha mafanikio ya mipango ya ustawi wa wafanyakazi wa Benki ya NMB katika Lango la Mweka, chini ya Mlima Kilimanjaro, baada ya kuwapokea wafanyakazi waliopandisha tuzo ya ithibati ya Mwajiri kinara zaidi Africa kileleni mwa mlima huo.
Mashujaa wa Safari ya Mlima Kilimanjaro
Mapokezi hayo ya Mashujaa waliopeperusha bendera ya NMB mlimani yaliwashirikisha pia zaidi ya wafanyakazi 100 wa NMB. Benki ya NMB kila mwaka pia ina wafadhili wafanyakazi zaidi 150 kushiriki kwa hiari katika mbio za Kili Marathon ambazo ilikuimarisha ustawi wa wafanyakazi wake kimwili, kiafya, na kukuza mshikamano ndani ya taasisi.
Akiwapongeza wafanyakazi hao wanne, Bw Ngalawa alisisitiza kuwa mafanikio yao ya kupanda mlima mrefu kuliko yote barani Afrika ni ishara ya uthabiti, kujituma, na ari ya kuzishinda changamoto.
"Zoezi hili limedhihirisha kuwa NMB si tu mahali bora pa kazi, bali pia ni taasisi inayothamini na kuwekeza kikamilifu katika ustawi, maendeleo, na mafanikio ya rasilimali watu wake. Kwa kuzingatia hilo, NMB inaendelea kujenga mazingira yanayochochea ubunifu, ufanisi, na uimara wa wafanyakazi wake, hivyo kuimarisha nafasi yake kama mwajiri kinara nchini," Bw Ngalawa alibainisha.
Sifa za Utendaji Bora Ndani ya NMB
“Wafanyakazi wetu waliorejea kutoka kilele cha Mlima Kilimanjaro wametuonesha kuwa dhamira, mshikamano, na uthabiti ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo makubwa - sifa ambazo pia ndizo msingi wa utendaji bora wa benki yetu.
“Kama benki, tunaamini kuwa safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro ni kielelezo cha safari yetu ya kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa wafanyakazi wetu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Bw Ngalawa, Ithibati ya Mwajiri Bora Tanzania kwa Mwaka 2025 si tu ni heshima ya kusherehekewa, bali ni uthibitisho wa jitihada zao katika kuweka mifumo bora ya kazi, kushughulikia ustawi wa wafanyakazi, na kukuza utamaduni wa ushirikiano na heshima baina ya wafanyakazi wake.
Nishani hiyo, alifafanua, inaashiria kuwa Benki ya NMB imefanikiwa kuwa taasisi inayothamini rasilimali watu, kuwa na mazingira mazuri yanayohamasisha ubunifu, kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi kupitia sera bora, na kuendelea kukuza maendeleo yao kitaaluma.
“Tunapowekeza katika watu wetu, ni motisha tosha ya kufanikisha malengo yao binafsi na ya yale ya kitaasisi kwa ujumla.”
Tuzo ya Kuendelea Kupaa Juu Zaidi
Bw Ngalawa alisema katika safari ya kuwa taasisi kinara zaidi, wanawahimiza wafanyakazi kuyachukulia mafanikio haya yote kama chachu ya kuimarisha juhudi za kuboresha huduma kwa wateja na kuyafanya mazingira ya kazi kuwa mazuri zaidi.
Aidha, aliongeza kuwa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro ilibeba ujumbe wenye maana mkubwa: hakuna kizuizi kisichoweza kukabiliwa kama kuna mshikamano, nia njema na kujituma kwa dhati.
Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanadhihirisha thamani ya kufanya kazi kama timu, uvumilivu, na azma isiyotetereka katika kufanikisha malengo makubwa, ndani na nje ya mazingira ya kazi.
“Kwa pamoja, tutaendelea kupanda juu zaidi, tukiimarisha mazingira bora ya kazi, na kudumisha viwango vya juu vya ufanisi na uwajibikaji.”
Chakula cha Jioni cha Top Employers Institute Hispania
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Bw Emmanuel Akonaay, uthibitisho wa NMB kama Mwajiri Bora unaonesha jitihada zake za kuhakikisha ustawi wa watu wake, utamaduni shirikishi wa mahali pa kazi, na kuendelea kuboresha mbinu za usimamizi wa rasilimali watu.
Siku nne kabla ya safari ya kuelekea kilele cha Kibo, kilichopo kwenye urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari, tarehe 13 Februari, Bw Akonaay alipokea Nishani ya Mwajiri Kinara zaidi kwa niaba ya NMB katika hafla ya Top Employers Institute jijini Madrid, Hispania.
Wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Top Employers Institute, Bw David Plink, alieleza kufurahishwa kwake na mpango wa NMB wa kupeleka nishani yake hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro kama ishara ya mafanikio na ufanisi.
Bw Akonaay alimueleza kiongozi huyo kuwa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro haikuwa tu kusherehekea mafanikio ya NMB katika usimamizi wa rasilimali watu barani Afrika, bali pia juhudi za kuwahamasisha waajiri wengine kuwekeza katika ubora wa mahali pa kazi na ajira kwa ujumla.
Taasisi Inayozingatia Watu Kwanza
“Kutambulika kama Mwajiri Bora na kitendo cha kuipeleka nishani ya ithibati yake juu ya Mlima Kilimanjaro ni vielelezo tosha vya jitihada zetu za kuifanya benki yetu kuwa moja ya sehemu bora zaidi za kazi na kuendeleza vipaji duniani, na hii inadhibitisha kuwa sisi ni taasisi inayozingatia ustawi wa watu kwanza,” Bw Ngalawa alisema
Akifafanua zaidi, alieleza kuhusu programu mbalimbali zinazolenga ustawi wa wafanyakazi kwa upande wa afya ya mwili na akili, pamoja na kuwawezesha kifedha kupitia elimu ya matumizi bora ya mapato na uwekezaji wenye tija.
Alibainisha kuwa malengo haya ndiyo msingi mkuu wa kuanzishwa kwa Siku ya Ustawi wa Wafanyakazi wa NMB, ambalo jukwaa maalum linalohamasisha afya, furaha, na maendeleo ya rasilimali watu.
Uzinduzi wake ulikuwa sehemu ya kilele cha Mashindano ya Michezo ya Kikanda, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza Disemba mwaka jana, na yatakayokuwa yanafanyika kila mwaka kwa lengo la kujenga mshikamano, umoja, na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi wa NMB.
Comments