Washindi wa ‘NMB MastaBata’ waagwa Dar, watimkia Dubai
NA MWANDISHI WETU
WASHINDI wa fainali ya msimu wa sita wa kampeni ya kuhamasisha matumizi na malipo kwa njia ya kadi iliyoendeshwa na Benki ya NMB, ‘NMB MastaBata - La Kibabe,’ wameagwa na kuondoka jijijni Dar es Salaam Jumanne Februari 25 kwenda Dubai kwa ziara ya siku tano iliyolipiwa gharama zote na benki hiyo.
Hafla ya kuwakabidhi tiketi na kuwaaga washindi hao sita na wenza wao, imefanyika Makao Makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Masuluhisho ya Biashara Ndogo na za Kati wa Mastercard International, Ali Wehbe, ambaye aliipongeza NMB kwa ubunifu na mafanikio makubwa ya kampeni hiyo.
Msimu wa sita wa Kampeni ya Mastabata ulizinduliwa Novemba 9, 2024, NMB pamoja na Mastercard wakitenga zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh. Mil. 300, ikiwa ni muendelezo wa NMB MastaBata iliyoanza mwaka 2018.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema kampeni hiyo iliyodumu kwa miezi mitatu (Novemba 9, 2024 hadi Feberuari 12, 2025), ilikuwa ya mafanikio makubwa, huku wateja zaidi ya 1,256 walijishindia zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 300.
“Kampeni hii ilipata mafanikio makubwa sana, ambako miamala na malipo kwa pos na online yaliongezeka kwa asilimia 27 katika kipindi cha miezi mitatu hiyo ambayo tulipata washindi 1,200 wa kila wiki wa fedha taslimu Sh. 100,000 kila mmoja na washindi 30 wa droo za mwisho wa mwezi waliotwaa Sh. 500,000 kila mmoja.
“Pia kulikuwa na washindi 10 wa safari za utalii wa ndani katika Hifadhi za Taifa za Ngorongoro (watano) na Mikumi (watano), ambao wote waliambatana na wenza wao kufanya utalii, lakini pia katika kipindi hicho tuliendesha droo za kutafuta na kuwapata washindi 10 waliolipiwa ada za watoto na wategemezi wao za hadi Sh. Mil. 4 kila mmoja.
“Na baada ya ‘grand finale’ iliyofanyika katikati ya mwezi huu, leo tuko hapa kukabidhi tiketi na kuwaaga washindi 6 wa safari ya Dubai ambako watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Dubai ikiwa ni pamoja na safari ya Jangwani, Dubai Mall Aquarium Underwater Zoo, kote huko kwa gharama zilizolipiwa na NMB na MasterCard.
“Gharama hizo ni pamoja na tiketi za ndege za kwenda na kurudi, malazi, chakula na za kutalii Dubai. Kila mmoja miongoni mwetu anafahamu namna ambavyo Dubai inavyovutia na namna ambavyo mtu yeyote atakaefika pale atakua na nafasi kubwa ya kufurahia, kujifunza na kupata uzoefu mwingine wa maisha ya wenzetu,” alisema.
Mponzi aliwataka washindi hao na wateja wa NMB kwa ujumla kuendelea na utamaduni chanya wa kufanya malipo yasiyohusisha pesa taslimu, ambayo ni salama, rahisi na nafuu na kwamba licha ya kufikia ukomo wa NMB MastaBata, njia hizo za malipo zinapaswa kuendelea kutumika ili kujiepusha na viatarishi vya pesa taslimu, ikiwa ni pamoja na wizi na upotevu.
“Nitumie nafasi hii kuwatakia kila la kheri, muende na mrudi salama na muendelee kuwa mabalozi wazuri wa NMB na Mastacard kwa kuwasihi na wengine watumie kadi zao kufanya malipo, lakini hata kwa wale ambao sio wateja wa NMB, basi muwafikishie ujumbe wa kujiunga na benki yetu kwani kuna mazuri mengi kwa ustawi wa wateja wetu wote,” alibainisha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga washindi hao, Wehbe alisema Mastercard International inajivunia ushirikiano baina yao na NMB, huku akiipongeza benki hiyo kwa ubunifu na mafanikio ya ongezeko la watumiaji wa malipo kwa njia ya kadi, yaliyotokana na uwepo wa Kampeni ya MastaBata kwa miaka sita.
Aliwapongeza washindi wote wa kampeni hiyo, hususani wanafainali hao waliotimkia Dubai kwa ziara ya siku tano iliyogharamiwa kila kitu, huku akikiri kuvutiwa na mwamko wa Watanzania katika suala zima matumizi yasiyo ya pesa taslimu, yanayochagizwa na bunifu bora za Huduma Jumuishi za Kibenki kutoka NMB.
Kwa niaba ya washindi wenzake, Elizabeth Masanja aliishukuru Benki ya NMB kwa kujali na kuthamini wateja wao na kwamba binafsi amefurahia ushindi unaompeleka Dubai ambako anaamini atapata uzoefu chanya utakaomsukuma kukua kibiashara sio tu kutoka kwa wenzake alioambatana nao, bali wafanyabiasahara wa huko waendako.
Comments