YALIYOJIRI MKUTANO WA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, MSIGWA KATIKA BWAWA LA MWALIMU NYERERE


 *YALIYOJIRI LEO FEBRUARI 16, 2025 JNHPP, PWANI WAKATI KATIBU MKUU WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA AKITOA TAARIFA KUHUSU MASUALA MBALIMBALI YALIYOTEKELEZWA NA SERIKALI .*


#Juhudi za Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeifanya Tanzania kuwa kinara barani Afrika katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za bara la Afrika uliofanyika Januari 27 na 28 Jijini Dar es Salaam ni kielelezo tosha kuwa Tanzania tunafanya vizuri.


#Hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme nchini imefikia 78.4%. Serikali imepanga kufikisha 100% ndani ya kipindi cha miaka 5 kuelekea mwaka 2030. Hali ya uunganishaji umeme kwa wateja nchini imeendelea kuimarika, wateja milioni 5.2 wameshaunganishiwa ambapo lengo ni kupeleka umeme kwa wateja milioni 13.5 ifikapo mwaka 2030. 


#JNHPP imeanza kuzalisha umeme na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika. Uwezo wa uzalishaji wa umeme kutokana na mitambo iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa ni MW 3,796.71. Matumizi ya juu yaliyofikiwa ni MW 1,900.62 iliyofikiwa tarehe 14.2.2025, ikiwa ni ongezeko la MW 124.22 kutoka MW 1,776.4 za Novemba mwaka 2024.


#Matarajio ya uzalishaji umeme kufikia mwisho wa mwaka 2025 yatakuwa MW 4,081.71 (ongezeko litatokana na kukamilika kwa JNHPP mashine ya mwisho na MW 50 za umeme wa jua kwenye mradi wa Kishapu). Matarajio ni kuzalisha MW 7,992.5 ifikapo mwaka 2030.


#Serikali kupitia TANESCO, inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kusafirisha umeme kuunganisha mikoa yote kwenye Gridi ya Taifa. Mikoa ambayo haipo kwenye Gridi ya Taifa ni Katavi, Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara. 


#Mradi wa JNHPP umeongeza uwezo wa kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa ambapo wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 2021, mradi ulikuwa 33%, mpaka Februari 2025, mradi umefikia 99.80%. 


#Mpaka sasa, jumla ya mashine 8 kati ya 9 zimeshawashwa na kufanya jumla ya MW 1,880 kuongezeka kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme.


#Utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze  kV 400 wenye urefu wa KM 160, umefikia asilimia 99.5 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2021/22. 


#Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambacho ni sehemu ya mradi wa JNHPP umefikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 35.9 mwaka 2021/22. 


#Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia maji wa Rusumo wa MW 80 umefikia asilimia 99.7. Mradi umeanza kuzalisha umeme, kwa sasa Tanzania inanufaika na kiasi cha wastani wa MW 27 kutoka kwenye mradi huo.


#Mradi wa kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi Extension  MW 185 umefikia 97.6% na kuchangia MW 160 katika Gridi ya Taifa ukilinganisha na asilimia 88 ya utekelezaji ya mwaka 2021/22.


#Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mto Malagarasi (MW 49.5), wakandarasi wajenzi walishapatikana na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2027. 


#Mradi wa Umeme wa Jua ulioanzishwa Kishapu mkoani Shinyanga unatarajiwa kuzalisha jumla ya MW 150. Mradi umeanza ujenzi wa awamu ya kwanza itakayozalisha MW 50 na baadae MW 100 zitakazofikisha MW 150. Utekelezaji wa mradi huu kwa awamu ya kwanza umefikia asilimia 50. 


#Kuhusu mradi wa njia za kusafirisha umeme ya Tanzania - Zambia, ujenzi wa njia umeanza na umefikia 34.11% ukihusisha mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Iringa kupitia Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga (TAZA) yenye urefu wa KM 624 pamoja na vituo vyake vya kupoza umeme.


#Mradi wa usafirishaji wa umeme kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZA) Tanzania itaungana na mtandao wa Gridi wa Jumuiya ya Nishati katika ukanda wa Kusini mwa Afrika. Utekelezaji wake unaendelea na umefikia asilimia 34, unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.


#Kuhusu ubora na usalama wa maji, maabara za ubora wa maji nchini zenye hadhi ya Ithibati zimeongezwa kutoka Maabara moja (1) iliyopo mkoani Mwanza  hadi kufikia Maabara Saba (7).  


#Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati ikiwemo bwawa la Farkwa ambapo Dola za Marekani milioni 125.3 zimepatikana kutoka Benki ya AfDB kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na mtambo wa kusafisha na kutibu maji ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha mita za ujazo 128,000 kwa siku.


#Ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko umefika asilimia 79 ukihusisha ujenzi wa gati ambao umefikia asilimia 98; jengo la utawala asilimia 90; na ujenzi wa sehemu ya ubaridi wa kuhifadhia samaki asilimia 65.


#Uwekezaji huo utaimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 hadi tani 52,937.99 na kuchangia katika pato la Taifa. Aidha, jumla ya vizimba 274 vimekopeshwa kwa wananchi 1,250 ambapo jumla ya shilingi bilioni 5.6 zimetumika.


#Serikali imesambaza boti 160 kwa wanufaika 3,163;

Mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 167,256.16 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 813.53 mwaka 2020 hadi tani 181,655.70 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 878.88 mwaka 2024.


#Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka  2020/2021 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2023/2024. Kiasi hiki cha mauzo ya tani 14,701 kimechangia katika mfuko wa fedha za kigeni jumla ya dola za Marekani milioni 61,394,527.23. 


#Viwanda vyenye ithibati ya kuuza nyama nje ya nchi vimeongezeka kutoka viwanda vinne (4) mpaka kufikia viwanda saba (7) katika mwaka wa 2024/ 2025.


#Tarehe 21 na 22 Februari, 2025, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa Afrika wa Kahawa G25 utakaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili. Utazikutanisha nchi 25 za Afrika zinazozalisha Kahawa.


#Kaulimbiu ya Mkutano huu ni “Fungua Fursa za Ajira kwa Vijana kupitia Uimarishaji wa Tasnia ya Kahawa Barani Afrika. Lengo lake ni kuhamasisha nchi wanachama wa IACO kutumia fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa kahawa kutatua tatizo la ajira kwa Vijana.


#Takwimu zinaonesha kuna nchi 50 zinazozalisha kahawa duniani ambapo bara la Afrika lina nchi 25.  Tanzania uzalishaji wa kahawa ndani ya kipindi cha miaka 3 umeongezeka kutoka tani 55,000 hadi tani 85,000. 


#Tanzania imeshinda nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa 73 wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege barani Afrika, mikutano ya kamati, mkutano wa kikanda na maonesho inatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 24 mpaka 30 Aprili, 2025.


#Kazi ya ujenzi na ukamilishaji wa majengo ya mji wa Serikali imefikia asilimia 89.4. Majengo yakikamilika yatagharimu shilingi bilioni 738 ambapo takriban shilingi Bilioni 457 zimeshatumika.


#Pamoja na ujenzi wa majengo hayo, kazi ya  kujenga barabara za ndani ya mji wa Serikali Mtumba inaendelea vizuri na nyingi zimekamilika. Barabara hizo zina urefu wa kilometa 51.2. 


#Ujenzi wa uwanja wa Arusha umefikia asilimia 26 na ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 75. Aidha, Serikali inaendelea na ukarabati wa viwanja vya Uhuru na viwanja vya mazoezi vya Gymkhana, Law School na Maj. Gen. Isamuhyo vya jijini Dar es Salaam. 


#Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzikia wananchi katika majiji ya Dodoma na Dar es Salaam, na ujenzi wa Akademia ya Taifa ya Michezo pamoja na Hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Kwimba - Mwanza. 


#Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imesaini mkataba wa ujenzi wa uwanja wa michezo utakaogharimu shilingi Bilioni 352 katika eneo la Nzuguni/ Nanenane wenye uwezo wa kubeba watazamaji  32,000. Ujenzi unatekelezwa kwa muda wa miezi 24. 


#Natoa wito kwa jiji la Dodoma, taasisi zenye viwanja na wananchi kuanza kuwekeza kwenye hoteli zenye hadhi, maduka na maeneo ya burudani ili kulifanya eneo unapojengwa uwanja kuwa kitovu cha huduma za kijamii na lenye kuvutia zaidi. 


*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAMBO 5 YA KILA MWANANDOA KUFAHAMU

SALMA KIKWETE, WAWATA WAMPAISHA PROF. NDAKIDEMI