Na Yusuph Mazimu, Dar es Salaam
Mtu aliyebuni jina la nchi ya Tanzania, Mohammed Iqbal Dar mwenye asili ya India, amefariki dunia huko Birmigham, Uingereza akiwa na umri wa miaka 80.
Amefariki usiku wa kuamkia leo nchini Uingereza alikokua akiishi tangu mwaka 1965, baada ya kuhamia huko.
Kwa zaidi ya miaka 10 Iqbal Dar amekuwa akisumbuliwa na maradhi yaliyomfanya ashindwe kutembea.
Mohammed Iqbal ni nani?
Mohamed Iqbal Dar, alizaliwa August 8, 1944 mkoani Tanga, akisoma katika shule za Agha Khan na Mzumbe, alikopata elimu yake ya msingi na Sekondari. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi walioonekana wadadisi wa mambo shuleni, akishiriki mara kadhaa kwenye mashindano mbalimbali ya vipaji.
Pengine udadisi wake ulichochewa na mzazi wake, baba yake aliyekuwa daktari katika hospitali huko mikoa ya Tanga na Morogoro, alikokua anafanya kazi tangu mwaka 1930 aipokuja nchini.
Alipataje fursa ya kutunga jina la nchi ' Tanzania?
Katika miaka ya 1960's mwanzoni, mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yalikuwa katika harakati za kuunganisha mataifa hayo na kuwa taifa moja. Katika harakati hizo, likatolewa tangazo kwenye gazeti la serikali la The standard.
Sasa akiwa mwanafunzi shuleni Mzumbe, Iqbal alikutana na tangazo linalomtafuta mtu ambaye atatoa wazo la jina la nchi baada ya kuunganishwa kwa Zanzibar na Tanganyika.
Kijana huyu wakati huo akiwa mdogo wa chini ya miaka 20, alishiriki kwa kuwasilisha jina la Tanzania, na kuibuka mshindi na kuzawadiwa shilingi 200 pamoja na medali, alizokabidhiwa na waziri wa habari wa wakati huo, Sheikh Idriss Abdul Wakil.
Ushindi wake ulileta furaha kwa famili na shuleni kwake, alipongezwa kila kona.
Hatimaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni
muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati. Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.
Jina hili la "Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" lilibadilishwa baadae mnamo tarehe 28 Oktoba, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Alipataje jina la Tanzania?
Utunzi wa jina sio kitu rahisi sana. Hata majina ya watoto wetu wakati mwingine hutupa shida kutunga. Achilia mbali kutunga jina la nchi, nchi yenye watu karibu milioni 30 wakati huo. Kutunga jina linalosubiriwa kwa hamu mpaka na marais wa nchi zote mbili. Jina la Tanzania.
Kuna wakati alipohojiwa na vyombo vya habari, alisema kwake ilikuwa moja ya kazi rahisi kufanya. Anasema alichukua herufi tatu za kutoka jina la Tanganyika (TAN), herufi tatu za jina la Zanzibar (ZAN), herufi ya kwanza ya jina lake Iqbal (I) na imani herufi ya kwanza ya dheheu lake la kiislamu la Ahmadiyya (A).
Akaunganisha: TAN+NZAN+I+A akapata jina Tanzania, ambalo linatumika mpaka leo kama utambulisho wa taifa hilo la muungano wa nchi mbili Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo, barua ya ushindi kutoka Wizarani ilionyesha kulikuwa na orodha ya wananchi 16 akiwemo yeye kutambulika kama washindi wa utunzi wa jina la nchi. Iqbal Dar anajitambua mshindi pekee kwa kuwa ndiye aliyekabidhiwa zawadi za ushindi na kutambuliwa siku ya tukio.
Comments